WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepiga marufuku usafirishaji wa chakula
kwenda nje ya nchi kuanzia leo.
“Kuanzia leo, ni
marufuku kwa mtu yoyote kusafirisha mazao ya chakula kwenda nje ya nchi bila ya
vibali. Serikali inahamasisha uwekezaji kwenye ujenzi
wa viwanda nchini. Kama tutatoa vibali, ni lazima mtu alazimike kusaga nafaka
ili kutoa ajira nchini,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Juni 26, 2017) wakati
akitoa nasaha kwenye Baraza la Eid lililofanyika kitaifa kwenye msikiti wa
Masjid Riadha, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro mara baada ya kuswali sala ya Eid.
“Jana nimeona kwenye televisheni taarifa kuhusu malori 10 yaliyokamatwa
Tarakea yakiwa na mahindi tayari kuvushwa mpaka. Mheshimiwa RC akasema chakula
hicho ni lazima yarudishwe kwa
ajili ya usagaji.”
“Mimi nasema kuanzia leo, yeyote atakayekamatwa akitorosha chakula
kwenda nje ya nchi, chakula hicho
kitataifishwa na kupelekwa ghala la Taifa na gari lake tutalitaifisha na
litaishia Jeshi la Polisi. Tunafanya hayo kwa lengo
la kuwalinda Watanzania tusikumbwe na baa la njaa.”
Akitoa tahadhari kuhusu uuzwaji wa chakula nje ya nchi, Waziri Mkuu
amesema kumekuwa na wimbi kubwa la usafirishaji wa chakula kwenda nje ya nchi
bila kibali. “Hilo ni kosa kubwa kwa sababu litasababisha nchi yetu kupata baa
la njaa huko mbele,” amesema.
Amesema mipaka ya Tarakea, Holili, Mwanga, Horohoro, Siha, Namanga na Sirari
imekuwa inapitisha kiasi kikubwa cha mazao ya chakula kwenda nje ya nchi jambo
ambalo ni hatari sana. “Hii ni kwa sababu chakula cha ndani
hakitoshelezi mahitaji. Kwa sababu nchi zote za
jirani hazina chakula cha kutosha. Tusipokuwa makini, tutabaki tunalia
njaa."
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi wafanyabiashara wa ndani,
wachukue mahindi kutoka maeneo yenye mavuno mengi na kuyapeleka kwenye sehemu
zenye mavuno kidogo. “Watanzania tushirikiane, kama ni biashara tutoe huku
kwenye mavuno mengi na tuyapeleke Shinyanga na Geita ambako wanayahitaji au
tukanunue Sumbawanga na kuyapeleka kwenye mikoa mingine yenye upungufu,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa dini waisadie Serikali katika
mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kupitia kwenye nyumba za ibada. “Naomba
tuendelee kushirikiana kupambana na janga hili la dawa za kulevya kwa ustawi wa
nchi yetu. Naamini viongozi wa dini mnayo nafasi kubwa katika mapambano haya,
kwa kuwafunda vijana wetu kuishi katika maadili ya kidini na kutojiingiza
kwenye janga hilo.”
Alisema
Serikali kwa upande wake
itaendeleza mapambano hayo bila ajizi wala mzaha. “Tunaomba wananchi
wote watuunge mkono kwa kutoa taarifa sahihi za wanaojihusisha na uzalishaji,
utengenezaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya pindi tu wanapowabaini.”
Wakati huo huo, akitoa
tafsiri ya Qur’aan tukufu kwenye Baraza la Eid, Sheikh wa Mkoa wa Arusha,
Sheikh Shaaban Juma alisema kila nguzo katika Uislamu inapaswa kufuatwa na
kwamba mtu akiharibu nguzo moja tu anakuwa ameharibu nguzo zote tano.
Alisema
siku ya kiyama, watatokea watu wenye thawabu kama milima ya Usambara ama
Upareni na akawataka Waislamu wote nchini wadumu katika kutenda mema ili wapate
thawabu.
Mapema, akitoa khutba
katika swala ya Eid el Fitr iliyoswaliwa
kwenye msikiti huohuo wa Masjid Riadha, Sheikh Mlewa Shaban alisema sikukuu ya
Eid ni siku ya kujiepusha na madhambi kama ulevi, kamari na lugha chafu, bali
aliwataka waumini wote waitumie siku hiyo kuwapa furaha maskini, yatima na
wajane.
“Mtu
asiseme mwezi wa Ramadhan umepita, sasa narudia mambo yangu ya zamani. Adhabu
za Mwenyezi Mungu hazina mipaka na wale waliotulizana watapata thawabu yao,
kumbukeni neema na Mwenyezi Mungu na mcheni Mwenyezi Mungu.”
“Kitu
tunachopaswa kufanya kila wakati ni kumcha Mwenyezi Mungu. Lazima tupendane,
tuondoe tofauti zetu na tuujenge Uislam. Hatuwezi kuujenga uislam kama
hatupendani. Lazima tuilinde ibada yetu kwa sababu hatuna garantii, ni lini
tutaondoka,” alisema.
Sherehe
hizo zilihudhuriwa na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir
bin Ally; Wajumbe wa Baraza la Ulamaa, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof.
Jumanne Maghembe; Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mama Anna Mghwira; IGP Mstaafu, Bw.
Said Mwema; Mbunge wa Moshi Mjini, Bw. Jaffary Michael; Wakuu wa Wilaya za Mkoa
huo na viongozi mbalimbali wa dini na Serikali.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment