Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.

Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.





Nafasi Ya Matangazo

Wednesday 31 January 2018

NOTISI YA SIKU 30 KWA WALIOVAMIA KIWANJA CHA SERIKALI NJIRO ARUSHA



WAJANJA WALITAKA KUPIGA BILIONI 400 UTENGENEZAJI PASIPOTI MPYA ZA TANZANIA

Rais Dkt. John Magufuli leo, Januari 31,2018 amezindua mfumo wa uhamiaji mtandao (e-Immigration) ambao utasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi, kudhibiti ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali na kuimarisha utoaji wa huduma za kiuhamiaji kwa raia wa Tanzania na wageni wanaoingia na kuishi hapa nchini kwa madhumuni mbalimbali.

Uzinduzi wa mfumo huo umefanyika katika ofisi kuu ya uhamiaji Jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Seif Ali Iddi, na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.

Wengine ni Jaji Mkuu wa Tanzania,Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Tulia Ackson Mwansasu, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili,Dkt. Ali Hassan Mwinyi na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.

Kabla ya kuzindua mfumo wa uhamiaji mtandao, Rais Magufuli amekagua teknolojia iliyotumika katika mfumo huo ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa alama za vidole na baadaye kupatiwa pasipoti mpya ya kielekektronikia (e-Passport) ambayo pia imeanza kutolewa leo.

Rais Magufuli amempongeza Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Idara ya Uhamiaji kwa kufanikisha mchakato uliofanikisha uwepo wa mfumo wa uhamiaji mtandao na kuanza kutoa pasipoti mpya ya kielektronikia kwa gharama nafuu ya Shilingi Bilioni 127.2 ikilinganishwa na makadirio yaliyowekwa awali ya Shilingi Bilioni 400.

“Hapa tumeokoa fedha nyingi za Watanzania, kuna watu walikuwa wamejiandaa kutupiga na kuchukua hizo Shilingi Bilioni 400, lakini tukatumia vyombo vyetu mbalimbali, tukafanya uchunguzi na tumefanikiwa kutekeleza mradi huu kwa gharama nafuu” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, kwa kutambua kazi nzuri inayofanywa na idara ya uhamiaji baada ya kupokea maelekezo yake ya kutakiwa kufanya mabadiliko makubwa, Mhe. Rais Magufuli ameahidi kutoa Shilingi Bilioni 10 kwa ajili ya kujenga ofisi ya makao makuu ya idara hiyo Mjini Dodoma.

“Kamishna Jenerali Dkt. Anna Makakala na timu yako mnafanya kazi nzuri, ndio maana nimewanunulia nyumba 103 kwa ajili ya wafanyakazi na leo nitawapa fedha nyingine Shilingi Bilioni 10 mkajenge ofisi nzuri ya makao makuu, nyinyi endeleeni kuchapa kazi, endeleeni kukamata wahamiaji haramu na endeleeni kukusanya mapato vizuri” amesema Rais Magufuli.

Mapema akitoa taarifa ya mfumo wa uhamiaji mtandao, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala amesema mfumo huo ni muunganiko wa mifumo mbalimbali ambayo imesanifiwa kufanya kazi kwa pamoja, kutoa taarifa kwa watumiaji na wadau wa huduma za kiuhamiaji na kwamba kupitia mfumo huo idara ya uhamiaji inatarajia kutoa pasipoti za kielektronikia (e-Passport), viza za kielektronikia (e-Visa), vibali vya ukaazi vya kielektronikia (e-Permit) na udhibiti wa mipaka wa kielektronikia (e-Border Management) kwa awamu nne hadi ifikapo mwisho wa mwaka huu 2018, pamoja na kutoa pasipoti ya kielektronikia ya Afrika Mashariki ya Tanzania.

Balozi wa Ireland hapa nchini,  Paul Sherlock ameipongeza Tanzania kwa kufanikisha mradi huu na kueleza kuwa mfumo huu wa uhamiaji mtandao ni alama muhimu ya Taifa.


KUTOKA BUNGENI MJINI DODOMA LEO

MBUNGE wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete akizungumza Bungeni Mjini Dodoma leo Januari 31,2018 wakati wa Mkutano wa 10 wa Bunge unaoendelea Mjini Dodoma. /Picha: Katuma Masamba-Daily News Digital.
 Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Checke akiongoza Kakao cha Bunge Mini Dodoma leo.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Anghelina Mabula akijibu maswali Bungeni mjini Dodoma leo. 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira Na Walemavu, Jenista Mhagama akizungumza jambo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju Bungeni mjini Dodoma leo. 
 Mmoja tea wabunge akiuliza swali Bungeni mjini Dodoma leo.
 Naibu wa Waziri wva Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni akijibu maswali Bungeni mjini Dodoma leo. 

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Willium Ole Nasha, akijibu Maswali Bungeni Mjini Dodoma leo. 
 Wabunge wakifuatilia kikao cha Bunge Mini Dodoma leo. 
Wageni waliotembelea Bungeni Mini Dodoma leo wakiwa Bungeni


MLIOPOTEZA VYETI FUATENI UTARATIBU KUPATIA VYETI VINGINE

Na Katuma Masamba, Dodoma
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amesema, mhitimu aliyepoteza cheti anapaswa kufuata taratibu zote ili aweze kupatiwa cheti kingine.

Amezitaja taratbu hizo kuwa ni pamoja na kutoa taarifa polisi kuhusu upotevu wa cheti na kupata hati ya upotevu, kutangaza gazetini kuhusu upotevu wa cheti  kwa lengo la kuutarifu umma ili kusaidia kupatacheti kilichopotea.

“Lengo la kutoa taarifa polisi ni ni kupata msaada wa kiuchunguzi ili kusaidia kukipata cheti kilichopotea,” amesema Nasha.

Akijibu swali la Mbungewa Mafinga Mjini, Cosato Chumi aliyetaka kujua taratibu zinazotumika kwa mtu aliyepoteza cheti cha taaluma, Nasha amesema endapo cheti kilichopotea hakikupatikana hata baada ya kutangazwa, mhusika atalazimika kujaza fomu ya omb la cheti mbada;a au uthibitisho wa matokeo na kuiwasilisha Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) na kwenye tovuti  ya baraza hilo.

Amesema NECTA pia hufanya uchunguzi wa uhalali wa umiliki wa ccheti husika na kutoa huduma stahiki. Wahitimu waliofanya mitihani kuanzia mwaka 2008 ambao vyeti vina picha hupatiwa vyeti mbadala  huku waliofanya mitihani kabla ya mwaka huo hupatiwa uthibitishowa matokeo.

Nasha pia amebainisha kuwa cheti mbadala kinachotolewa ni halisi, lakini huongezwa maandishi yanayosomeka ‘DUPLICATE’ kuonesha kuwa cheti hicho kimetolewa mara ya pili.


UANGALIZI HAFIFU WA WATOTO CHANZO CHA KUPOTEA KWA WATOTO

Na Katuma Masamba, Dodoma
Uangalizi hafifu wa watoto kutoka kwa wazazi,  walezi na jamii kwa ujumla umetajwa kuwa moja ya sababu ya wimbi la upoteaji wa watoto katika maeneo mbalimbali nchni ikiwemo jiji la Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni ameyasema hayo wakati akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Fakharia Shomar Khamis aliyetaka kujua sababu zinazopelekea kuongeza kwa tatizo la watoto kupotea na mkakati wa kuondoa tatizo hilo.

Masauni amesema, sababu zingine ni mazingira magumu wanayoshi baadhi ya watoto, imani za kishirikina, visasi kati ya familia na kupotea kwa bahati mbaya.

Amesema, Serikali  kupitia Jeshi la Polisi imekuwa ikifanya jitihada za kudhibiti matukio ya kupotea kwa watoto kwa kutoa elimu kupitia programu ya Polisi Jamii kwa watoto shuleni na wazazi kupitia mihadhara ya kijamii na vyombo vya habari.

“Jitihada hizo zimekuwa zikizaa matunda kwa kuongeza elimu ya usalama wetu kwanza miongoni mwa jamii na hvyo kuongeza umakini wa kuwalinda watoto,” amesema Masauni.

Amesema kuanzia kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka jana kwa mkoa wa Dar es Salaam pekee jumla ya watoto waliopotea ni 184 ambapo kati yao 176 walipatikana na wanane wanaendelea kutafutwa.


Tuesday 30 January 2018

MATOKEO YA MITIHANI KIDATO CHA NNE 2017 HAYA HAPA

Baraza la Mitihani la Taifa (NEC), leo limweka hadharani matoneo ya mitihani ya kidato cha Nnne kwa watahiniwa waliofanya mitihani yao Novemba 2017. 
TAARIFA KAMILI YA MATOKEO HII HAPA 






MENO YA KIBOKO YAINGIZIA SERIKALI MILIONI 30.9

Na Hellen Mlacky 
WIZARA ya Maliasili na Utalii kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeuza meno ya viboko vipande 12,467 vyenye uzito wa tani 3.5 (kilo 3,580.29 ) kwa Sh milioni 30.9 katika mnada wa hadhara uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Aliyeibuka mshindi katika mnada huo ni Lorey Kilasi wa kampuni ya Ontour Tanzania Ltd ambaye alilipa asilimia 25 ya fedha hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kabla ya mnada huo, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ulinzi wa Wanyamapori TAWA, Mabula Misungwi alisema mnada huo ulishirikisha kampuni 19 zenye leseni daraja la kwanza.

“Sisi hapa ni kama waangalizi kwa sababu anayefanya kazi hii ya mnada ni Kamati Maalum inayojumuisha watu kutoka Wizara ya Fedha na ndiyo wasimamizi wakuu…Utaratibu ni kwamba meno yanakusanywa na yanaletwa hapa kidogo kidogo na mara ya mwisho uuzaji kama huu ulifanyika 2004” alisema.
Alisema meno hayo siku za nyuma kuna kampuni zilizokuwa zimesajiliwa zinafanya kazi hiyo ya ununuzi ila kwa sasa utaratibu umebadilika badala ya kuziuzia moja kwa moja unafanyika mnada wa hadhara.

“Mnada huu unahusisha wafanyabiashara wa nyara waliopewa leseni ya nyara daraja la kwanza mwaka 2017... meno haya yanatumika kama urembo, wengine wanayasaga kutengeneza sanamu na soko lake kubwa lipo Ulaya” alisema.

Alisema mnunuzi huyo aliyeshinda amelipa asilimia 25 ya malipo hayo papo hapo na asilimia 75 iliyobakia atatakiwa kulipa ndani ya siku 14 zijazo baada ya mnada huo.

Mapema Mwenyekiti wa mnada huo kutoka Wizara ya Fedha, Karerema Kwaleh alitangaza kwamba meno hayo yatauzwa kwa wastani wa uzito wa nusu kilo bila kugawanywa au kuchambuliwa wakati wa mnada na wanunuzi wataruhusiwa kuondoa bidhaa kwenye eneo la mnada baada ya kulipia ada na kodi husika kikamilifu na kupewa hati ya kumiliki nyara hizo.


REA III YAZINDULIWA KIBONDO, KAKONKO

 Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa Nne kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Br. Gen. Mstaafu Emanuel Maganga (wa Tano kushoto), Mbunge wa Muhangwe ambaye ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Atashasta Nditiye (wa pili kushoto), Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago (wa Kwanza kushoto) wakifunua kitambaa kuashiria uzinduzi wa Mradi wa usambazaji umeme vijijini Awamu ya Tatu katika wilaya za Kibondo na Kakonko.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati), Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Br. Gen. Mstaafu Emanuel Maganga (wa Tano kulia), Mbunge wa Muhangwe ambaye ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Atashasta Nditiye (wa Tano kushoto), Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago (wa Tatu kushoto) Wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa mradi wa Usambazaji mradi wa umeme vijijini Awamu ya Tatu katika wilaya za Kakonko na Kibondo mkoani Kigoma.
 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa Tatu kulia), akimkabidhi kifaa cha UMETA mmoja wa wananchi katika kijiji cha Mabamba wilayani Kibondo. Kifaa hicho kitamwezesha kuwasha umeme ndani ya nyumba bila kufunga nyaya za umeme. Wa Pili kulia ni Mbunge wa Muhangwe ambaye ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Atashasta Nditiye.
 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa kwanza kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Dkt. Alexander Kyaruzi (wa pili kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Dkt Gidion Kaunda (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Mhandisi Bengiel Msofe (wa kwanza kushoto), wakisaini vitabu vya wageni katika Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Kibondo mara walipofika wilayani humo kwa ajili ya uzinduzi wa mradi wa usambazaji umeme vijijini uliofanyika wilayani Kibondo mkoani Kigoma.
Baadhi ya wananchi katika kijiji cha Mabamba wilayani Kibondo wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ( hayupo pichani) wakati alipofika kijijini hapo kuzindua mradi wa usambazaji umeme vijijini awamu ya Tatu.
**************
Na Teresia Mhagama, Kigoma
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amezindua mradi wa usambazaji umeme vijijini Awamu ya Tatu katika wilaya za Kakonko na Kibondo mkoani Kigoma ambapo vijiji 69 vya wilaya hizo vitaunganishiwa umeme.

Uzinduzi huo umefanyika katika kijiji cha Mabamba wilayani Kibondo na kuhudhuriwa na Mkuu wa mkoa wa Kigoma, watendaji wa Wilaya , Halmashauri, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mbunge wa Muhambwe, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mbunge wa Buyungu na wananchi.

Akizindua Mradi huo, Dkt. Kalemani alisema kuwa katika wilaya ya Kibondo vijiji 40 vitasambaziwa umeme na katika wilaya ya Kakonko jumla ya vijiji 29 vitapata umeme na kueleza kuwa vijiji vitakavyosalia vitasambaziwa umeme kuanzia mwezi Julai, 2019.

Aliongeza kuwa, Mkandarasi atakayesambaza umeme katika wilaya hizo ni kampuni ya Urban & Rural Engineering ambapo jumla ya shilingi bilioni 25 zitatumika katika kazi hiyo.

Dkt. Kalemani alitumia fursa hiyo kuwaagiza watendaji katika Halmashauri nchini kutenga fedha kwa ajili ya kufunga miundombinu ya umeme katika Taasisi za Umma na sehemu zinazotoa huduma za kijamii kama Shule, Vituo vya Afya, Visima vya Maji, sehemu za Ibada na masoko ili mkandarasi atapofika katika eneo husika aweze kuweka umeme.

Aidha, alitoa maagizo kwa wakandarasi wa umeme vijijini kukamilisha kazi ndani ya wakati, wasiruke vijiji na pia waajiri vijana wa eneo husika wakati wa utekelezaji wa mradi.

Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Br. Gen. Mstaafu Emanuel Maganga aliishukuru Serikali kwa utekelezaji wa mradi huo ambao mwananchi anagharamia shilingi 27,000/= ili kuunganishwa umeme huku gharama nyingine zikibebwa na Serikali.

Aidha, alitoa maagizo kwa watendaji wa Wilaya na Halmashauri za mkoa wa Kigoma kuhakikisha kuwa wanamsimamia Mkandarasi huyo katika hatua zote za utekelezaji wa mradi ili afanye kazi kulingana na mkataba wake.

Mbunge wa Muhambwe ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye pamoja na kupongeza juhudi za Serikali kupeleka Umeme katika Vijiji hivyo, aliisisitiza REA kuhakikisha kuwa vijiji ambavyo bado havijaingizwa katika mpango wa kupelekewa Umeme katika mzunguko wa kwanza, navyo pia visambaziwe nishati hiyo.

Aidha, Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago alizungumzia gharama za kufunga nyaya za umeme ndani ya nyumba ambazo alieleza kuwa ni kubwa, " nakushauri Waziri wa Nishati, uwaelekeze wakandarasi wanaofanya kazi ya kufunga nyaya za umeme waache kuweka gharama za kutisha," alisema.


Monday 29 January 2018

MAWAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO WA TANZANIA NA RWANDA WAJADILI UJENZI WA RELI YA ISAKA- KIGALI

Mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania,  Dkt Philip Isdor Mpango (wa pili kushoto) na Waziri wa Fedha na Mipango ya Uchumi wa Rwanda, Gatete Claver (wa pili kulia) ukiendelea kuhusu upatikanaji wa fedha za mradi wa Reli ya Isaka Shinyanga hadi Kigali nchini Rwanda katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango wa Tanzania, Doto James (kulia) na mwenzake wa Rwanda , Caleb Rwaunganza wakisaini maagizo kutoka kwa Mawaziri wa Wizara hizo mbili kuhusu hatua za upatikanaji wa fedha za mradi wa Reli ya Isaka Shinyanga hadi Kigali nchini Rwanda Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango wa Tanzania,  Doto James (kulia) na mwenzake wa Rwanda, Caleb Rwaunganza wakibadilishana taarifa walizosaini za maagizo kutoka kwa Mawaziri wa Wizara hizo mbili kuhusu hatua za upatikanaji wa Fedha za mradi wa Reli ya Isaka Shinyanga hadi Kigali nchini Rwanda Jijini Dar es Salaam. (Picha na WFM)

Benny Mwaipaja, WFM
Mawaziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania na Rwanda wamekutana Jijini Dar es Salaam kujadili namna ya kupata fedha za Ujenzi wa Reli yenye Kiwango cha Kimataifa (SGR) kutoka Isaka Shinyanga hadi Kigali Rwanda ikiwa ni mwendelezo wa mikutano kuhusu suala hilo iliyoanza kuanzia Januari 20, 2018.

Katika Mkutano huo wamejadili kuhusu njia ambayo inaweza kuwa rahisi kupata fedha ikiwemo ya kutumia Sekta binafsi, Serikali kukopa au kumweka mwekezaji ambapo wamekubaliana kupitia upya taarifa zilizo wasilishwa mezani za pande hizo mbili na kufanya maboresho na pia kuzungumza na Benki ya Dunia (WB), Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa pamoja ili wakati wa kikao kijacho waweze kujadili suala hilo kwa kuangalia vigezo na masharti ya kupata fedha. 

Kikao hicho ambacho ni cha watalamu kimewakutanisha Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania,  Dkt. Philip Isdor Mpango na Waziri kutoka Rwanda Gatete Claver pamoja na Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Eugene Kayihura na Makatibu wakuu wa wizara hizo na wajumbe wengine. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango wa Tanzania, Doto James na mwenzake wa Rwanda, Caleb Rwaungaza, wamesaini maagizo hayo ya Mawaziri kwa ajili ya utekelezaji.

Ikumbukwe kuwa mapema mwezi huu, Rais Dkt. John Magufuli na Rais wa Rwanda Paul Kagame walikubaliana kutekeleza mradi huo wa ujenzi wa Reli kutoka Isaka Shinyanga hadi Kigali Rwanda na wakatoa maagizo ya kuanza utekelezaji kwa kuangalia namna ya kupata fedha za mradi huo.


TBA WAPEWA SIKU 3 WAWE WAMEMALIZA UBOMOAJI JENGO LA TANESCO UBUNGO

KATIBU Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga ameipa siku tatu Wakala wa Nyumba chini (TBA), kuhakikisha inamaliza kazi ya uvunjaji wa jengo la ghorofa 10 la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).


Nyamhanga alitoa agizo hilo ikiwa ni takribani siku 63 tangu TBA kuanza ubomoaji wa jengo baada ya Rais John Magufuli Nevemba 15 kuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuvunja jengo hilo na Ofisi ya Wizara ya Maji kwa kuwa zimejengwa katika hifadhi ya barabara.

Rais Magufuli alisema hakuna kumuonea mtu huruma au aibu katika kipindi hiki na kwamba kama Serikali imeenda kinyume na taratibu ivunjiwe kama walivyovunjiwa wananchi wengine.

Katibu mkuu alisema ubomoaji wa jengo hilo umechukua muda mrefu hivyo ikifika Februari mosi hahitaji kuona jengo hilo likiwepo hivyo kuruhusu shughuli nyingine za ujenzin ziendelee.

“Wametoa maelezo ya kwanini wamechelewa kumaliza ubomoaji nimewaelewa ila ikifika Februari mosi sihitaji kuona sehemu iliyobakia tunataka ujenji wa barabara ya kupishana uanze,” alisema.

Nyamhanga alisema mkandarasi amefanikiwa kuhamisha miundombinu mbalimbali ambayo ipo katika eneo litakalojengwa barabara za kupishana (interchange) hivyo kinachosubiriwa ni TBA kumalizika uvunjaji.

.Alisema baada ya kukagua amegundua kuwa kati ya ghorofa 10 nane zimeshavunjwa hivyo ameawaagiza kumalizia ghorofa mbili zilizobakia ili mradi wa barabara za ya kupishana eneo la Ubungo uanze kama inavyotakiwa.

“Nimekagua ubomoaji naona maendeleo ni mazuri hivyo nimewaagiza ikifika kesho kutwa Alhamis wawe wamemaliza ili kazi zingine ziendelee kwani wakandarasi wanawasubiri,” alisema.

Alisema dhamira ya Serikali ni kuona mradi wa barabara za kupishana unamalizika kwa wakati kama walivyokubaliana ambao ni miezi 36.

Mhandisi Nyamhanga alisema kwa mujibu wa mkataba kati ya Wakala wa Barabara Tanzania Tanroads na Mkandarasi kampuni ya China Civil Engeneering Contract Corporation (CCECC) ujenzi wa barabara hiyo utagharimu zaidi ya sh. bilioni 177.

Aidha, Nyamhanga alisema ujenzi wa barabara ya kilomita 16 njia nne kutoka Kimara hadi Kiluvia unatarajiwa kuanza mapema mwezi Machi.

Alisema ni imani yake kuwa hatua zinahitajika ili kupatikana mkandarasi zitachukuliwa haraka kwani fedha zipo.

“Pamoja na ujenzi wa barabara za kupishana hapa Ubungo Serikali imedhamiria kuifungua Dar es Salaam ambapo mwezi Machi ujezi wa barabara ya njia nne utaanza kutoka Kimara hadi Kiluvia,” alisema.

Akizungumzia hatua zilizofikiwa hadi sasa kuhusu ujenzi huo Meneja wa Tanroads mkoa wa Dar es Salaam, Julius Ndyamukama alisema uchambuzi wawakandarasi wenyewe uwezo wa kutekeleza mradi umefanyika, usanifu umefayika na zabuni imetolewa kwa kampuni iliyokidhi vigezo ili kuwasilisha gharama za mradi.

Ndyamukama alisema kesho wanatarajia watarejeshewa majibu na ndani ya siku 14 hatua zote zitakamilika ili ujenzi uanze.

Meneja huyo alisema katika upanuzi wa barabara hiyo kutajengwa madaraja matatu katika maeneo ya Kilivia, Kibamba na Mpiji pamoja na kuwepo barabara za mchepuko.

Aidha, alisema katika mradi huo kutakuwa na barabara za kupishana eneo la Mlonganzila ili kurahisisha kufika katika Hospitali ya Mlonganzila.

“Hatua zote zikimalizika ndio tutao taarifa rasmi kuwa ujenzi utagharimu shilingi ngapi kwa sasa tunakamilisha hatua muhimu, “ alisema.


Wednesday 24 January 2018

WATOTO 15 WENYE MATATIZO YA MOYO WAFANYIWA UPASUAJI WA BILA KUFUNGUA KIFUA

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Taasisi ya  Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart-SACH) ya nchini Israel na Kituo  cha Moyo  cha Berlin (Berlin Heart Center) cha nchini Ujerumani  wamefanya upasuaji  wa bila kufungua kifua (Catheterization) kwa watoto 15 wenye matatizo ya Moyo.

Upasuaji huo unaotumia  mtambo wa Cathlab umefanyika katika kambi maalum ya matibabu iliyoanza Januari 20 na itamalizika Januari 25 maak huu. 
Matibabu yaliyofanyika ni ya kuzibua matundu kwenye moyo na kutanua mishipa ya moyo kwa watoto wenye umri wa kuanzia mwezi mmoja hadi miaka 18. 
Kambi  hii ilienda sambamba na uchunguzi wa moyo kwa watoto 32 ambapo watoto 20 watafanyiwa matibabu katika kambi hii na wengine 12 waliobaki watatibiwa na madaktari wetu wa ndani kuanzia wiki ijayo.
Tumepanga kufanya matibabu kwa watoto 20 tunaamini hadi kambi itakapomalizika watoto wote hawa watakuwa wamepata matibabu. Watoto 15 waliopata matibabu wengine wameruhusiwa na waliobaki hali zao zinaendelea vizuri na wataruhusiwa pindi afya zao  zitakapoimarika.
Aidha kambi hii imeenda sambamba na utoaji wa elimu ya upasuaji wa moyo wa bila kufungua kifua kwa watoto na jinsi ya kuwahudumia watoto waliofanyiwa upasuaji huo. Mafunzo haya yamewajengea uwezo wafanyakazi wetu wakiwemo madaktari, wauguzi, wataalam wa kutoa dawa za usingizi na wataalam wengine wa chumba cha upasuaji. Mafunzo hayo  yatawasaidia  kuongeza ufanisi katika  kazi zao. 
Tangu mwaka 2015 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ilianza kushirikiana na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart- SACH) na Berlin Heart Center hadi sasa jumla ya watoto 46 wamefanyiwa upasuaji wa moyo nchini Israel. Gharama za matibabu ya watoto hawa zinagharamiwa na Taasisi hizi za Israel na Ujerumani kwa makubaliano ya kirafiki na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete. 
Kwa upande wa watoto waliotibiwa katika kambi maalum za matibabu zilizofanyika hapa nchini ni  79 mchanganuo wake ni kama ifuatavyo: Mwaka 2015 walitibiwa watoto  11, mwaka 2016 watoto 48,  mwaka 2017 watoto 20.
Tunawashukuru sana wenzetu hawa wa SACH na Berlin Heart Center kwa kuona umuhimu wa kutoa huduma ya matibabu bila malipo  kwa watoto wenye matatizo ya moyo.  Watoto waliotibiwa wamepona na wale ambao ni  wanafunzi   wanaendelea na masomo yao. 
Kwa upande wa wazazi na walezi tunawaomba wasisahau kupima afya za watoto wao pale watakapoona kuna hali ya tofauti katika ukuaji wa mtoto kwani magonjwa mengi ya moyo yanaanzia utotoni. Mtoto akianza kuuguwa magonjwa ya moyo wazazi wengi wanadhani ni matatizo ya kifua baada ya kumfikisha Hospitali na kufanyiwa vipimo  ndipo inagundulika mtoto anasumbuliwa na magonjwa ya moyo. 
Kwa wamama wajawazito wafanye uchunguzi (Fetal Echocardiography) wa kuangalia kama mtoto aliyeko tumboni anamatatizo ya moyo au la. Kupitia kipimo hiki  mtoto akigundulika kuwa  na tatizo la moyo ataweza kupatiwa  matibabu kwa wakati  na hivyo kuwa na afya njema kama watoto wengine.


Kama mnavyofahamu matibabu ya moyo ni ya gharama hivyo basi tunaendelea kuwahimiza wananchi  kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ambao utawasaidia kulipa gharama za matibabu pindi  watakapouguwa na kuhitaji kupata matibabu. Kwa wale wasiojiweza kabisa kambi kama hizi zinatumika na Taasisi kuwahudumia bila malipo yoyote yale.


Tuesday 23 January 2018

MBUNGE WA CHALINZE AKANUSHA YALIYOANDIKWA KATIKA MTANMDAO WAKE WA INSTAGRAM


Monday 22 January 2018

RAIS MAGUFULI APOKEA HATI ZA UTAMBULISHO KUTOKA KWA MABALOZI SITA

 Rais Dkt. John Magufuli akimsikiliza Balozi mteule wa Ugiriki hapa nchini Konstantinos Moatsos wakati alipokuwa akijitambulisha kabla ya kuwasilisha Hati zake za Utambulisho Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Rais Dkt. John Magufuli akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi wa Mali hapa nchini Fafre Camara Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Rais Dkt. John Magufuli akimtambulisha Waziri wa Mambo ya Nje Balozi Dkt. Augustine Mahiga kwa Balozi wa Ethiopia hapa nchini Dina Mufti Said Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Ethiopia hapa nchini Dina Mufti Said Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Rais Dkt. John Magufuli akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi wa Argentina hapa nchini Martin Gomez Bustillo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais Dkt. John Magufuli akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi wa Ufilipino hapa nchini Uriel Norman Garibay Ikulu jijini Dar es Salaam
**************
RAIS Dkt. John Magufuli amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mabalozi 6 walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini.

Mabalozi waliowasilisha hati zao leo, Ikulu jijini Dar es Salaam ni Konstantinos Moatsos – Balozi wa Ugiriki hapa nchini mwenye makazi yake Nairobi nchini Kenya, Fafre Camara – Balozi wa Mali hapa nchini mwenye makazi yake Addis Ababa nchini Ethiopia na Dina Mufti Sid – Balozi wa Ethiopia hapa nchini mwenye makazi yake Nairobi nchini Kenya.

Wengine ni Elizabeth Taylor – Balozi wa Colombia hapa nchini mwenye makazi yake Nairobi nchini Kenya, Martin Gomez Bustillo – Balozi wa Argentina hapa nchini mwenye makazi yake Nairobi nchini Kenya na Uriel Norman Garibay – Balozi wa Ufilipino mwenye makazi yake Nairobi nchini Kenya.

Rais Magufuli amewapongeza Mabalozi wote kwa kuteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini na ameahidi kuwapa ushirikiano utakaowezesha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na nchi zao kukua zaidi.

Rais Magufuli amewahakikishia kuwa Tanzania inatambua uwepo wa fursa mbalimbali za kibiashara na kiuchumi katika nchi hizo pamoja na ujuzi na uzoefu katika nyanja mbalimbali, na kwamba ni matarajio yake kuwa ujio wao utasaidia kuongeza manufaa ya kiuchumi na kubadilishana uzoefu.


Pia Rais Magufuli amewaomba Mabalozi hao kufikisha salamu zake kwa viongozi wa nchi zao na amewakaribisha kutembelea Tanzania.