Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.

Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.





Nafasi Ya Matangazo

Saturday 30 December 2017

OFISI YA MAKAMU WA RAIS YAKANUSHA TANGAZO LINALOTANGAZA USHIRIKI WA MAKAMU WA RAIS KUPANDA MITI TAREHE 1 JAN.2018



WAZIRI MKUU AMWAGIZA AFISA MADINI AITISHE KIKAO KESHO SAA 4 ASUBUHI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Kanda ya Kusini, Ogesa Charles Tale afike eneo la mgodi wa dhahabu wa Namumgo na kuitisha kikao cha wananchi kesho (Jumapili) saa 4 asubuhi.

“Sasa hivi natoka kwenda Matambare, twende wote, lakini kesho saa 4 asubuhi uje hapa Namungo, uitishe mkutano wa hadhara na uwasikilize hawa wachimbaji wadogo na kisha uniletee maelezo ofisini kwangu,” alisema.

Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumamosi, Desemba 30, 2017), wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Namungo, wilayani Ruangwa baada ya kupokea mabango mawili kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo. Waziri Mkuu yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka, na ameamua kukagua miradi ya maji, ujenzi wa zahanati na kuzungumza na wananchi katika wilaya hii.

Waziri Mkuu alisema Serikali ya awamu ya tano imejikita kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi na alipomuuliza afisa huyo kama ameshawahi kupata nafasi ya kuwasikiliza wachimbaji wadogo, alijibiwa kwamba hajawahi kufanya hivyo.

“Hawa ndiyo nguvukazi ya mgodi, hawa ndiyo wanaingia kule chini kuchimba udongo, hawa ndiyo wanapata machungu ya kazi ya uchimbaji, kwa hiyo uje uwasikilize na uniletee taarifa kesho mchana,” alisisitiza.

Baada ya kuyasoma mabango yao, Waziri Mkuu aliwaita wakazi ambao waliyaleta mabango hayo na kuwataka waeleze kwa undani ni matatizo gani yanayowakabili. Bango la kwanza lilisema wananchi wananyanyaswa na viongozi kwa maslahi binafsi ya viongozi na la pili lilisema wamekatazwa wasiseme matatizo yao kwenye mkutano huo wa Waziri Mkuu.

Mkazi wa kijiji cha Mtondo, kata ya Nambilanje, Mussa Omari Kimatilo, alisema wananyanyaswa na uongozi wa kijiji pamoja na uongozi wa wenye machimbo ya dhahabu na kwamba wananyimwa uhuru wa kujieleza kila wanapokutana na viongozi hao.

“Tunanyanyaswa na uongozi wa machimbo, tunanyanyaswa na uongozi wa kijiji na tukilalamika hakuna wa kutusikiliza. Tumekaa na Rajani (mmiliki wa mgodi) amekubali kutulipa lakini wananchi hatuna uhuru wa kujieleza,” alisema.

Alidai hata Naibu Waziri wa Madini alipotembelea mgodi huo mapema mwezi huu, hakupewa fursa ya kukutana na wachimabji wadogo, na badala yake alipitishwa kijijini hapo na kuingizwa mgodini kisha akaondoka.

Naye Bahati Mikael, mkazi wa kijiji cha Namungo alisema kumekuwa na ukiritimba wa kutoa leseni kuhusu mgodi huo na kwamba tangu ilipotolewa rasmi mwaka 2014, bado hawajalipwa malipo yao.

“Hapa pana ukiritimba wa kutoa leseni ya uchimbaji. Mwekezaji amekuwa akichimba kinyemela; tangu mwaka 2006 alikuwa hajapewa leseni hadi mwaka 2014 ndipo alipopewa,” alisema.

Alipoitwa na Waziri Mkuu atoe ufafanuzi juu ya madai ya wakazi hao, Kaimu Afisa Madini wa kanda hiyo alisema eneo wanalodai wakazi hao ni la Mzee Kishor Rajani na inaeleweka hivyo na kwamba miaka ya nyuma walichimba kwa maelewano tu bila mikataba yoyote.

“Yale ya nyuma yalishapita kwa sababu hamkuwa na mkataba naye, mlifanya naye kazi kwa makubaliano ya mdomo tu. Sasa hivi mmeanza kuwekeana mikataba, zamani alikuwa anachukua asilimia kubwa lakini sasa hivi anachukua asilimia 17.5 na inayobaki amewaachia ninyi,” alisema Bw. Tale.

Waziri Mkuu anaendelea na ziara ya jimboni kwake.


TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MATUMIZI YA FEDHA ZA KIGENI KATIKA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ametoa maagizo kuhusu matumizi ya fedha za kigeni katika  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusisitiza kuwa utekelezaji wake uanze  tarehe 1 Januari, 2018.  Maagizo hayo ni kama ifuatavyo: -

                 i.         Bei zote hapa nchini zitangazwe kwa shilingi ya Tanzania. Bei hizi zinajumuisha kodi ya nyumba za kuishi na maofisi, bei ya ardhi, gharama za elimu na afya, bei za vyombo vya usafiri na vifaa vya kielektroniki.

                     ii.         Bei ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja wasio wakazi zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni. Bei hizi zinajumuisha gharama za usafirishaji kwenda nchi za nje kupitia Tanzania, gharama za mizigo bandarini kwenda nchi za nje, gharama za viwanja vya ndege na viza kwa wageni, na gharama za hoteli kwa watalii kutoka nje ya nchi. Walipaji wanaotumia fedha za kigeni watambuliwe kwa vitambulisho vyao kama pasi za kusafiria na nyaraka za usajili kwa makampuni.

                  iii.         Viwango vya kubadilishana fedha vitakavyotumika katika kuweka hizo bei katika sarafu mbili viwekwe wazi na visizidi vile vya soko. Ifahamike wazi kuwa ni mabenki na maduka ya fedha za kigeni tu yanayoruhusiwa kupanga viwango vya kubadilisha fedha kutokana na ushindani katika soko la fedha za kigeni.

                    iv.         Mkazi yeyote wa Tanzania asilazimishwe kulipia bidhaa au huduma yeyote hapa nchini kwa fedha za kigeni.

Aidha Dkt. Mpango ameviagiza vyombo vya dola viwachukulie hatua za kisheria wale wote watakaobainika kukiuka maagizo haya ya Serikali.


IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO




MKUCHIKA AWASILISHA FOMU YA TAMKO LA RASILIMALI NA MADENI-MTWARA

Waziri wa NchiOfisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Capt Mstafu George Mkuchika Akikabidhi Fomu za tamko la Rasilimali na Madeni kwa Katibu Msaidi wa Tume ya serkretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma Kanda ya Kusini Mayina Henjewele.
Waziri wa NchiOfisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Capt Mstaafu George Mkuchika akionesha Fomu ya tamko Mara baada ya kukabidhi Fomu zake na Kuhakikiwa.
Katibu Msaidizi Ofisi ya Tume ya Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Uma Kanda ya Kusini Mayina Henjewele akisoma Taarifa kuhusiana na Viongozi waliokwisha Wasilisha Fomu za tamko la Rasilimali na Madeni katika Mikoa ya Ruvuma,Lindi na Mtwara.
*****************
Waziri wa NchiOfisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Capt Mstaafu, George Mkuchika  amewataka Wabunge,madiwani na Viongozi wa Umma wanaojihusisha na Biashara na Halmashauri kuacha mara moja kutokana na Kwenda kinyume na sheria ya viongozi na watumishi wa umma.

Mkuchika ameyasema hayo wakati akirejesha fomu za tamko la Rasilimali na Madeni katika Ofisi ya sekretarieti ya maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kusini Iliyopo Mkoani Mtwara.

Mpaka Kufikia Sasa Jumla ya Viongozi 794 ndio wamerejesha fomu hizo za tamko la Rasilimali na Madeni kati ya Viongozi 1246 ambao wanatakiwa kuwasilisha kwa kanda hiyo.

Aidha Ofisi hiyo imetenga Siku ya Jumapili, Desemba 31,2017  kuanzia Mchana mpaka Jioni Kupokea fomu kwa Viongozi ambao hawajawasilisha.


Friday 29 December 2017

WAZIRI MPINA APOKEA RIPOTI YA KAMATI NDOGO ALIYOIUNDA KWA SIRI KUTATHMINI UTENDAJI WA SEKTA YA UVUVI KATIKA ZIWA VICTORIA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Luhaga Mpina (kulia) akipokea ripoti ya Kamati Ndogo ya kutathmini utendaji wa sekta ya Uvuvi katika Ziwa Victoria kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bonaventure Baya anayeshuhudia ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia uvuvi, Dk. Yohana Budeba hafla iliyofanyika Makao Makuu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dodoma jana.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati Ndogo ya kutathmini utendaji wa sekta ya Uvuvi katika Ziwa Victoria baada ya kukabidhi ripoti yako mjini Dodoma jana. Kushoto ni Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhandisi Bonaventure Baya Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi, Dk Yohana Budeba
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, MLuhaga Mpina akiwashukuru wajumbe wa Kamati Ndogo ya kutathmini utendaji wa sekta ya Uvuvi katika Ziwa Victoria baada ya kupokea ripoti hiyo mjini Dodoma jana. Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia uvuvi Dk. Yohana Budeba 
Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya kutathmini utendaji wa sekta ya Uvuvi katika Ziwa Victoria,  Bonaventure Baya (kushoto) akiteta jambo na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia uvuvi, Dk Yohana Budeba mara baada ya kukabidhi ripoti yake kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Luhaga Mpina hayuko pichani Dodoma jana.


HARAKISHENI UMEME KUKAMILISHA MRADI WA MAJI NAMAHEMA ‘A’ - MAJALIWA

 Mkurugenzi Mtendaji wa KALIF Construction, Ally Mohamed Libaba akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (katikati) wakati wakijaribu kuvuta maji kutoka kwenye pampu ya mradi wa maji wa kijiji cha Namakuku, Desemba 28, 2017. Wa kwanza kulia ni msimamizi wa mradi huo, Fadhil Ally Libaba.
Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mibure, wakati alipoenda kukagua ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho Desemba 28, 2017. Waziri Mkuu yupo jimboni kwake kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
***************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemtaka Meneja wa TANESCO wilaya ya Ruangwa,Samuel Pyuza ahakikishe umeme unapatikana mapema kwenye pampu ya maji ili kukamilisha mradi wa maji wa Namahema ‘A’.

Ametoa wito huo jana jioni (Alhamisi, Desemba 28, 2017) wakati akizungumza na wakazi wa vijiji vya Namahema ‘A’ na Namahema ‘B’ wilayani Ruangwa, mkoani Lindi waliofika kumsikiliza mara baada ya kukagua mradi wa maji ambao umechukua miezi sita tangu uanze. Mradi huo unatarajiwa kukamilika Januari 15, mwakani.

Mradi huo ambao hadi kukamilika kwake utagharimu sh. milioni 244.52, unatarajiwa kuwahudumia wakazi 2,257 wa vijiji hivyo viwili ambao walikuwa wanasongamana kupata maji kutoka kwenye kisima ambacho kilikuwa kinatumia pampu ya mkono. Kijiji cha Namahema ‘A’ kina watu 1,668 na Namahema ‘B’ kina watu 589.

Waziri Mkuu ambaye yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka, ameanza ziara fupi ya siku tatu, kukagua miradi ya maendeleo jimboni kwake katika wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

Jumla ya sh. milioni 189.93 zimeshatumika kwenye mradi huo ambazo ni sawa na asilimia 77.68 ya fedha ziliopangwa kutumika. Fedha za mradi huo zimetolewa na Serikali Kuu kupitia Mfuko wa Uwekezaji wa Maji wa Taifa (National Water Investment Fund).

Kazi ambazo zimekamilika hadi sasa ni ujenzi wa vituo vya kuchotea maji (DP) 32; ujenzi wa mtandao wa mabomba yenye urefu wa mita 6,460; tenki la kuhifadhia maji leye ujazo wa lita 50,000, ujenzi wa nyumba ya mitambo (pump house); ujenzi wa uzio (fence) kwenye nyumba ya mitambo; ujenzi wa uzio (fence) kwenye tenki la kuhifadhia maji; na ununuzi wa pampu na mota.


SERIKALI YAONGEZA MIAKA MIWILI YA UMILIKI WA LESENI ZA VITALU VYA UWINDAJI NCHINI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na wadau wa sekta ya uwindaji wa kitalii katika mkutano uliondaliwa na Wizara yake mjini Dodoma jana kwa ajili ya kujadili mikakati mbalimbali ya kuimarisha sekta hiyo ikiwemo utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuanzisha utaratibu mpya wa utoaji wa leseni za vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mej. Jen. Gaudence Milanzi na Naibu Katibu Mkuu, Dk. Aloyce Nzuki (kulia).  
*******************
Na Hamza Temba, Dodoma
Serikali imesikia kilio cha wadau wa sekta ya uwindaji wa kitalii nchini na kuamua kuongeza muda wa miaka miwili ya umiliki wa leseni za vitalu 95 vya uwindaji wa kitalii ambazo zilikuwa ziishe muda wake tarehe 31 Desemba mwaka huu (2017).

Uamuzi huo umefikiwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla wakati wa kikao cha majumuisho na watendaji wa Wizara hiyo muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkuano wa wadau wa sekta hiyo ulioandaliwa na Wizara hiyo mjini Dodoma jana.

Akizungumzia uamuzi huo Dk. Kigwangalla alisema, lengo ni kuwapa muda wawekezaji hao ili waweze kujiandaa na mabadiliko ya mfumo mpya wa utowaji wa leseni za vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada ikiwemo kurudisha baadhi ya gharama za uwekezaji walizoweka katika vitalu hivyo. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI. 


Wednesday 27 December 2017

WANANCHI WAITAKA SERIKALI KUTATUA CHANGAMOTO YA UMEME KWENYE VITUO VYA USAJILI VITAMBULISHO VYA TAIFA- MTWARA

 
Hawa ni baadhi ya wananchi wa Mbaya Mashariki wakisubiri kujaziwa fomu za maombi ya Vitambulisho vya Taifa ili wakapigwe picha, kuchukuliwa alama za kibaiolojia na saini ya kielektroniki wakati zoezi la Usajili likiendelea kwenye Kata yao. Wakitoa huduma hiyo ni Moza Mohamedi Lukwekwe (kulia) Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbaya na Asia Abdallah Nachuma (kushoto) ambaye ni mjumbe wa Mtaa wa Mbaya. Huduma hiyo ya kuwajazia wananchi fomu za maombi ya Vitambulisho imekuwa ikitolewa kwa wananchi wote wanaofika kwenye vituo kusajiliwa na hawajui kusoma na kuandika ili kurahisha zoezi. 
Mwenyekiti wa Mtaa wa Chiputaputa, Juma Hamisi Chambeya akiwagongea muhuri wakazi wa eneo lake kwenye fomu za maombi ya Vitambulisho kuthibitisha makazi ya wananchi hao wakati wa zoezi la kuwasajili Vitambulisho vya Taifa likiendelea. Kabla ya wananchi kugongewa muhuri wa Serikali ya Mtaa wananchi kwanza wanatakiwa kujaza fomu ya maombi yenye vipengele 72 na kutoa nakala ya viambatisho vyao msingi vinavyowatambulisha kabla fomu hiyo haijapitiwa kugongwa muhuri wa Serikali ya Mtaa/Kijiji anakoishi.
Sharifa Said (kushoto), Zubeda Abdallah (katikati) na Rahma Ally (kulia) wakijaza fomu za maombi ya Vitambulisho vya Taifa katika kituo cha Usajili kilichopo Shule ya Msingi Lilungu mkoani Mtwara, wakati zoezi la Usajili na Utambuzi wa Watu lenye kulenga utoaji wa Vitambulisho vya Taifa likiendelea Wilaya ya Mtwara.
Asha Bakari (kushoto) na  Asha Yasini (mwenye mtoto) wakazi wa Kata ya Mbaya Mashariki wakitafuta fomu zao walizojaza mwaka 2014 waliposhiriki zoezi la uandikishaji Vitambulisho vya Taifa; ili wakakamilishe hatua ya mwisho ambayo ni kuchukuliwa alama za kibaiolojia, Picha na Saini ya Kielektroniki. 
*****************
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeendelea na Usajili wananchi Vitambulisho vya Taifa mkoani Mtwara ambapo katika Wilaya ya Mtwara Idadi kubwa ya wananchi wamejitokeza kushiriki zoezi hilo huku baadhi wakilalamikia kukaa muda mrefu kwenye vituo vya Usajili na baadhi ya mashine kutokufanya kazi.

Athumani Salum mkazi wa Kata ya Magomeni amesema “zoezi kama zoezi ni zuri ila changamoto kubwa ni kukatika kwa umeme na hivyo kusababisha wananchi tusubiri muda mrefu kiasi cha kukatisha tamaa. Kwakuwa hili ni zoezi la kiserikali kwanini Serikali isisaidie umeme kutokatwa kwenye vituo? ”

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Rose Mdami ambaye alikuwepo kituoni hapo ameeleza changamoto ya umeme ni kubwa katika vituo vingi vya usajili hata hivyo kwa kushirikiana na uongozi wa Wilaya wameshachukua hatua za kutafuta magenereta ili kazi ziendelee kama kawaida.

“Si kweli kwamba mashine zote hazifanyi kazi katika mashine tulizonazo zipo baadhi ambazo zinatunza umeme muda mrefu na kwahizi ambazo hazifanyi kazi kwa kukosa umeme tunaendelea kuharakisha kupata magenereta ili kuamsha mashine ambazo zimeshindwa kufanya kazi ili wananchi wasisubiri muda mrefu” alisisitiza

Katika kituo cha Magomeni kilichopo shule ya Msingi Lilungu wananchi pia wamekutwa wakihangaika kutafuta fomu zao za usajili walizosajiliwa mwaka 2014 ambapo zoezi hilo lilifanyika kwa mara ya kwanza kwa hatua ya kujaza fomu tu bila kupigwa picha.

Akifafanua kuhusu wananchi hao Rose amesema kwa wale wananchi wanaofika kwenye vituo vya Usajili na ambao walisajiliwa mwaka 2014 na kujaza fomu za maombi ya Vitambulisho vya Taifa, pindi wanapofika kwenye vituo vya Usajili wanachukuliwa alama za kibaiolojia, picha na saini ya kielektroniki na kisha kuruhusiwa kuondoka kwakuwa taarifa zao msingi tayari zilishaingizwa kwenye mfumo tofauti na wale ambao ndio kwanza wanaanza Usajili.

Mkoa wa Mtwara unakusudiwa kusajili wananchi zaidi ya 800,000 kwa Wilaya za Mtwara, Tandahimba, Nanyumbu, Masasi na Newala. Usajili ambao unakusudiwa kumalizika mapema mwezi Machi, 2018 na kuwezesha wananchi katika mkoa huo kuanza kutumia Vitambulisho vitakavyozalishwa katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na uzalishaji mali.


CHEGENI AANZA KUTOA TIBA YA VYUMA KUKAZA BUSEGA

 MBUNGE wa Jimbo la Busega Dk. Raphael Chegeni akizungumza katika mkutano wa hadhara
Na Mwandishi wetu
MBUNGE wa Jimbo la Busega Dk. Raphael Chegeni amewataka vijana na akina mama jimboni Busega kuacha kubweteka na kudai vyuma vimekaza bali waongeze bidii kwa kuchapa kazi kwa nafasi ya kila mtu mmoja mmoja na ndani ya vikundi vyao. 

Ushauri huo ameutoa wakati akikabidhi vifaa vya kumwagilia maji mashambani kwa ajili ya kikundi cha vijana wa 'Hapa Kazi Tu' Busega cha Nyanhanga na fedha taaslimu shs Milioni 1, kwa kikundi cha  Inuka mama cha Nyashimo.

“Hii ni changamoto kwenu nendeni mkatumie mitaji hii kuwainua kimaisha na muwe mfano kwa vikundi vingine,”alisema Dk Chegeni. 

Aidha wakati wa mkutano wa hadhara amechangia sh milioni 10,  kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa kwa shule ya Sekondari ya Kata  ambayo imepewa jina la Chegeni Secondary School kwa heshima yake na kutambua mchango mkubwa anaoutoa katika kusukuma elimu wilayani humo.  

Jumla ya Sekondari 18 zilianzishwa kwa msaada mkubwa kutoka kwake akiwa mbunge na hakuna kiongozi yeyote aliyefanya makubwa upande wa elimu ukilinganisha na  yeye.

Wilaya ya Busega inakabiliwa na upungufu wa madarasa kwa wanafunzi 1,209 kwa mwaka ujao wa masomo. 

Dk. Chegeni amewataka wananchi na wadau wote kujitoa kutekekeza upatikanaji wa vyumba hivyo. 

Aidha amempongeza Rais Dk. John Magufuli kwa hatua ya serikali yake kuwajali watoto wanyonge wa kitanzania kwa kutoa elimu bure kwa darasa la kwanza hadi kidato cha nne na kuwataka wananchi kuunga mkono jitihada hizo za Rais.


Thursday 21 December 2017

NAIBU SPIKA TULIA ATIMIZA AHADI YAKE KWA WANA BUJELA

 Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dk. Tulia Ackson akikabidhi vifaa vya ujenzi kwaajili ya shule ya Sekondari ya Bujela iliyopo Wilayani Rungwe mkoani Mbeya ikiwa ni utekelezaji wa ahadi zake alizozitoa. 
 Wanafunzi wa Bujela  na walimu wao wakiwa katika picha na Naibu Spika.
 Naibu Spika Dk. Tulia Ackson akikabidhi mabati kwaajili ya ujenzi wa Kanisa.
 Dk Tulia akiwashukuru waumini wa Kanisa baada ya kukabidhi msaada wa Mabati.
Naibu Spika Dr Tulia Ackson amefanya ziara katika baadhi ya maeneo Wilayani Rungwe mkoa wa Mbeya ikiwa ni kutekeleza baadhi ya ahadi alizowahi kuzitoa katika kusaidia maendeleo, kwanza alianza kwa kutoa vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni tano katika shule ya sekondari Bujela

Akiwa katika shule ya Bujela Dr Tulia alisema “Ndugu zangu niwasihi jambo moja ambalo hata Rais Magufuli husisitiza, tusiingize siasa kwenye mambo ya maendeleo kwasababu  bila hivyo hatutapiga hatua, leo kama TULIA TRUST tuliahidi vifaa vyenye thamani ya Milioni tano na tayari tumetekeleza kwa kuja navyo vikiwemo bati, mbao, mchanga, saruji, chokaa, rangi, vioo, nondo."

“Tunafanya haya yote kwa ajili ya kuhakikisha tunawatengenezea watoto wetu mazingira mazuri ya kujisomea na baadae watuletee maendeleo sisi wazazi wao hivyo niwaombe viongozi wote tushikamane”  alisema Dr Tulia

Safari ikaendelea hadi katika Kanisa la Bujela ambalo liliharibiwa kwa upepo uliosababishwa na mvua huko pia  Dr Tulia alichangia jumla ya mabati 100 Kwa ajili ya kukamilisha ukarabati wa kanisa hilo ambalo tayari ujenzi wake ulianza kwa jitihada za waumini wenyewe kuchangishana kiasi cha fedha.

Dr Tulia aliwahimiza waumini pamoja na viongozi wa dini kuendelea kuliombea taifa la Tanzania amani pamoja na kumuombea Rais Magufuli ili aendelee kuiongoza nchi salama.


Wednesday 20 December 2017

RAIS MAGUFULI AONYA UPOTOSHAJI WA TAKWIMU

RAIS Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Watanzania na taasisi mbalimbali kutumia takwimu sahihi zinazotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na kujiepusha na takwimu za upotoshaji zinazosambazwa na baadhi ya watu kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 20 Desemba, 2017 katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu inayojengwa katika eneo la Makulu Mjini Dodoma.

Pamoja na wito huo Rais Magufuli ameitaka Ofisi ya Taifa ya Takwimu pamoja na vyombo vingine husika kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtu yeyote ama taasisi itakayotoa takwimu za upotoshaji.

“Kwa hiyo ndugu zangu Watanzania tumieni takwimu sahihi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, puuzeni takwimu za kupika zinazotolewa na baadhi ya watu kwenye mitandao, wapuuzeni hata wanaosema vyuma vimebana, vyuma vimebana kwa wanaotaka vya bure lakini wanaochapa kazi vyuma havijabana” amesisitiza Rais Magufuli.

Amebainisha kuwa uchumi wa Tanzania unakwenda vizuri ambapo katika nusu ya kwanza ya mwaka huu umekua kwa asilimia 6.8, mfumuko wa bei umeshuka hadi asilimia 4.4 kwa mwezi Novemba 2017 na akiba ya fedha za kigeni imefikia Dola za Marekani Bilioni 5.82 ambayo inaiwezesha nchi kununua bidhaa na huduma kwa miezi mitano, ikilinganishwa na wastani unaopaswa wa miezi miezi 4. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.


TANESCO YAHIMIZA MATUMIZI BORA NA ENDELEVU YA MTO PANGANI NA BWAWA LA NYUMBA YA MUNGU

NA K-VIS BLOG/Khalfan Said
MATUMIZI bora ya bonde la Mto Pangani, ndio njia pekee itakayosaidia kutunza vyanzo vya maji ambayo hutumika kuzalisha umeme kwenye vituo vya Pangani Hydro Systems, Meneja wa vituo hivyo, Mhandisi Mahenda S Mahenda amewaambia wahariri wa vyombo vya habari wanaotembelea bwawa la Nyumba ya Mungu lililoko mpakani mwa wilaya ya Mwanga na Simanjiro.

“Tanesco kama wadau wakubwa wa Mto huu, tumeona Mto umeingia mchanga na mchanga huo unatakiwa kuondolewa ili kuweza kuzalisha maji mengi zaidi kutoka bwawa la Nyumba ya Mungu na maji hayo yaweze kupatikana kwenye vituo na hatimaye kuzalisha umeme kama ambavyo inatakiwa.” Alisema Mhandisi Mahenda.
Pangani Hydro Systems ni mkusanyiko wa vituo vitatu vya kufua umeme vinavyofuatana ambavyo vimejengwa sehemu tofauti tofauti katika Mto Pangani.

Vituo hivyo ni pamoja na Nyumba ya Mungu, kituo cha Hale na kituo cha New Pangani Falls na vyote kwa ujumla wake huzalisha umeme wa Megawati 97 ambazo huingizwa kwenye Gridi ya Taifa, alisema Mhandisi Mahenda.

Kituo cha Nyumba ya Mungu, kilizinduliwa mwaka 1964 na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere, na kina mashine mbili za kufua umeme zilizofungwa tangu mwaka huo na kila moja inao uwezo wa kuzalisha Megawati 4 za Umeme na kufanya jumla ya Megawati 8

Hata hivyo changamoto kubwa inayokikabili kituo hicho na vituo vingine ambavyo vyote huendeshwa kwa kutumia nguvu za maji, ni mabadiliko ya tabia nchi na ongezeko la shughuli za kibinadamu kandokando ya Mto huo pamoja na kwenye bwawa lenyewe na hivyo kupelekea upungufu wa mara kwa mara wa maji ya kutosha kuendesha mitambo.

“Tunashirikiana na wenzetu wanaosimamia bonde la Mto Pangani, kwa kufanya doria za mara kwa mara ili kuwaelimisha wananchi matumizi bora na endelevu ya maji ya Mto huo ili kuleta manufaa kwa pande zote, amesema Mhandisi Mahenda.

Mhandisi Mahenda S. Mahenda(kulia), akifafanua mambo mbalimbali kwa wahariri kwenye bwawa la Nyumba ya Mungu Desemba 19, 2017


MKURUGENZI DCB BANK AMALIZA MUDA WAKE KWA MAFANIIKIO

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB anayemaliza muda wake, Edmund Mkwawa akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam jana.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB anayemaliza muda wake, Edmund Mkwawa (kulia) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Benki hiyo ambaye anataraji kuanza kazi rasmi Januari mosi 2018, Godfyey Ndalahwa. Mkwawa ameiongoza benki hiyo kwa miaka 15 Tangu kuanzishwa kwake, huku akijivunia mafanikio katika utendaji wake kwa kukuza Amana za wateja kutoka shilingi Bilioni 1.76 mwaka 2002 hadi shilingi bilioni 107 Mwezi Septemba 2017. (Picha na Mroki Mroki).
************ 
MAENDELEO YA BENKI YA BIASHARA YA DCB (DCB COMMERCIAL BANK PLC) TANGU ILIPOANZISHWA MWAKA 2002

Ndugu Wanahabari
Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutukutanisha hapa leo. Lengo la kuwaiteni ni kutoa taarifa kwa umma juu ya maendelo ya Benki ya Biashara ya DCB tangu kuanzishwa kwake ikiwemo mafanikio na malengo yake kwa kipindi kijacho kuanzia mwaka 2018.

Baadhi ya ajenda nitakazozipitia ni kutoa historia fupi ya benki na madhumuni ya uanzishwaji wake, taarifa ya utendaji kwa kipindi cha miaka 15, mahusiano na wanahisa wakuu ikiwemo manispaa ikiwemo mafanikio na changamoto iliyopata/ilizopata benki katika mahusiano hayo, msaada na uhusiano wa baadaye unaohitajika kutoka kwa wanahisa wakuu ikiwemo manispaa na mipango ya baadaye ya Benki yetu.

Awali ya yote, napenda kuwataarifu kuwa Benki ya Biashara ya DCB imekuwa mshindi wa kwanza katika mashindano ya uandaaji na uwasilishaji wa taarifa za mahesabu ya benki kwa mwaka 2016 kwa sekta za benki ndogo na za kati kwa ubora. Nafasi hii imeshikiliwa na benki yetu kwa mwaka wa pili mfululizo tangu mwaka 2015. Tuzo hii huandaliwa kila mwaka na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Mahesabu (NBAA).

Mashindano haya yalianza tangu mwaka 2011, na katika kipindi chote hicho DCB Commercial bank imeweza kufanya vizuri ambapo kwa miaka mitatu mfululizo (mwaka 2012 hadi 2014), Benki imeshika nafasi ya tatu (3) miongoni mwa benki zote kiujumla kwa ubora wa uandaaji na uwasilishaji wa taarifa za mahesabu ya kibenki. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.


Monday 18 December 2017

HALI YA UZALISHAJI UMEME VITUO VYA PANGANI HYDRO SYSTEM VIKO KATIKA HAKLI NZURI; MHANDISI MAHENDA


Mhandisi Mahenda S. Mahenda, Meneja wa Vituo vya uzalishaji umeme wa maji vya Pangani Hydro Systems, vinavyohusisha inahusisha vituo vitatu, New Pangani, kilichoko wilayani Muheza, Hale wilaya ya Korogwe, na Nyumba ya Mungu wilaya ya Mwanga, vyenye uwezo wa kuzalisha umeme jumla ya Megawati 97

NA K-VIS BLOG/Khalfan Said, Korogwe

VITUO vya uzalishaji umeme wa maji vya Pangani Hydro Systems, ambayo inahusisha vituo vitatu, New Pangani, kilichoko wilayani Muheza, Hale wilaya ya Korogwe, na Nyumba ya Mungu wilaya ya Mwanga, vyenye uwezo wa kuzalisha umeme jumla ya Megawati 97, viko katika hali nzuri, Meneja wa vituo hivyo, Mhandisi Mahenda S. Mahenda, amesema Leo Desemba 18, 2017.


Hata hivyo amesema, mashine moja kati ya mbili kwenye kituo cha Hale, haifanyi kazi na iko katika matengenezo. “Niwahakikishie tu kwamba matengenezo hayo ambayo bado hayajaanza hayataathiri upatikanaji umeme kwa sababu vyanzo vya umeme vimeongezeka.” Alisema.


Akifafanua zaidi Mhandisi Mahenda alisema, New Pangani Falls inazalisha umeme Megawati 68, Hale Megawati 21, na Nyumba ya Mungu Megawati 8 na uwezo wa vituo kutoa umeme wa kutosha.

Akizungumza na Wahariri wa vyombo vya habari waliotembelea vituo vya Hale na New Pangani Falls Mhandisi Mahenda, alisema, kituo cha Hale kilijengwa mnamo mwaka 1961 na kuanza kufanya kazi mwaka 1964 na kuwa kituo cha kwanza kabisa cha kuzalisha umeme wa maji katika historia ya nchio yetu.

“ Utaona umri wa mitambo hiyo ni miaka 53, na moja ya mashine hizo imeharibika na kufanya uwezo wa kituo wa kutoa Megawati 21, kupungua hadi Megawati 8, lakini niwahakikishie wananc hi licha ya upungufu huo, bado TANESCO inao uwezo wa kuzalisha umeme unaohitajika, kwani vyano vya umeme vimeongezeka.” Alisema.

 Valvu ya kupitisha maji yanayopelekwa kwenye mashine za kufua umeme, kwenye kituo cha nguvu za umeme cha Hale ikivuja. Mhandsi Mahedna alielezea hali hiyo kuwa haina taathira kubwa na inatokana na mashine hizo kuwa na umri mrefu Zaidi.
 Bwawa la maji Pangani Pangani Falls.

 Mhandisi Mahenda akifafanua mambo mbalimbali ya kiufundi kwenye chumba cha kudhibiti mifumo ya umeme cha New Pangani Falls.
 Exciter, moja kati ya mashine mbili ya kufua umeme kwenye kituo cha Hale, ambayo inafanya kazi. 
 Wahariri na wataalamu wa TANESCO, wakitembelea New Pangani Falls.
 Mhandisi Mkuu wa Pangani Hydro Systems, Lewis Loiloi, akitoa maeelzo kuhusu masuala ya kiusalama kwa wahariri wakiwa kwenye handaki, la New Pangani Falls.
Kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha New Pangani Falls cha 132 kV.