RAIS Dkt. John Pombe Magufuli amewataka
Watanzania na taasisi mbalimbali kutumia takwimu sahihi zinazotolewa na Ofisi
ya Taifa ya Takwimu na kujiepusha na takwimu za upotoshaji zinazosambazwa na
baadhi ya watu kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 20 Desemba, 2017 katika hafla ya uwekaji
wa jiwe la msingi la jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu inayojengwa katika eneo
la Makulu Mjini Dodoma.
Pamoja
na wito huo Rais Magufuli ameitaka Ofisi ya Taifa ya Takwimu pamoja na
vyombo vingine husika kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtu yeyote ama taasisi
itakayotoa takwimu za upotoshaji.
“Kwa
hiyo ndugu zangu Watanzania tumieni takwimu sahihi kutoka Ofisi ya Taifa ya
Takwimu, puuzeni takwimu za kupika zinazotolewa na baadhi ya watu kwenye
mitandao, wapuuzeni hata wanaosema vyuma vimebana, vyuma vimebana kwa wanaotaka
vya bure lakini wanaochapa kazi vyuma havijabana”
amesisitiza Rais Magufuli.
Amebainisha
kuwa uchumi wa Tanzania unakwenda vizuri ambapo katika nusu ya kwanza ya mwaka
huu umekua kwa asilimia 6.8, mfumuko wa bei umeshuka hadi asilimia 4.4 kwa
mwezi Novemba 2017 na akiba ya fedha za kigeni imefikia Dola za Marekani
Bilioni 5.82 ambayo inaiwezesha nchi kununua bidhaa na huduma kwa miezi mitano,
ikilinganishwa na wastani unaopaswa wa miezi miezi 4. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.
Rais Magufuli ameongeza kuwa Serikali imeendelea kufanya mambo makubwa ya
maendeleo ya nchi ikiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) kutoka Dar es Salaam
hadi Dodoma utakaogharimu Shilingi Trilioni 7.6, kutoa fedha za dawa ambazo
zimeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 31 hadi 269, kutoa Shilingi Bilioni 23.876
kwa ajili ya elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari kila mwezi,
mradi wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge), kuongeza mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu
kutoka Shilingi Bilioni 373 hadi Shilingi Bilioni 483 na mengine mengi.
“Hizi
ndio takwimu sahihi, na nyinyi Ofisi ya Taifa ya Takwimu mkiona mtu anapotosha
ukweli huu mkamateni mpelekeni mahakamani akajifunze kupata takwimu sahihi”
“Haya
tunayoyafanya wale ambao walikuwa wanapata fedha za bure lazima watapiga kelele
kuwa vyuma vimebana, lakini tunabana vya bure ili kuwaletea wananchi maendeleo,
na kwa kweli tutabana sana” amesema Rais
Magufuli.
Rais Magufuli amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt.
Albina Chuwa na wafanyakazi wote wa ofisi hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya na
pia ameishukuru Benki ya Dunia, Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID) na Shirika la Maendeleo la Canada
kwa ufadhili wake waliowezesha kujengwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Mjini Dodoma
na Ofisi nyingine iliyojengwa Zanzibar pamoja na kusaidia shughuli nyingine za
Ofisi hiyo.
Ujenzi
wa jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu Mjini Dodoma lenye ghorofa nne na ukubwa
mita za mraba 7,100 ulianza Machi 2017 na unatarajiwa kukamilika Januari 2018
kwa gharama ya Shilingi Bilioni 11.6.
Katika
taarifa yake kwa Rais Magufuli Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya
Takwimu Dkt. Albina Chuwa amesema kwa kutambua umuhimu wa takwimu katika
kupanga, kutekeleza na kusimamia masuala mbalimbali ya maendeleo na ustawi wa
jamii, ofisi yake imepiga hatua kubwa katika ukusanyaji na utoaji wa takwimu
bora na hivyo kuiwezesha kushika nafasi ya pili barani Afrika ikitanguliwa na
Ofisi ya Takwimu ya Afrika Kusini.
Hafla
hiyo imehudhuriwa na Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu, Mabalozi,
Mwakilishi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia Bella Bird na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Dodoma wakiongozwa na Mkuu wa
Mkoa Dkt. Binilith Mahenge.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment