WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amewataka vijana wafanye kazi kwa bidii na maarifa kwa sababu kazi
ndiyo msingi wa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Pia amewasihi
wananchi wanaoishi katika maeneo ya mipakani wahakikishe suala la kulinda
mipaka hiyo linapewa kipaumbele ili kuimarisha amani na utulivu nchini.
Waziri Mkuu ametoa
kauli hiyo leo (Jumamosi, Machi 24, 2018) wakati akizungumza na wananchi
alipowasili katika uwanja wa ndege wa Nachingwea.
Waziri Mkuu ambaye
yuko wilayani Ruangwa kwa ziara ya kikazi ya siku mbili amesema ili vijana
waweze kupata maendeleo lazima wafanye kazi kwa bidii.
Pia Waziri Mkuu
ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wananchi wanaoishi katika maeneo ya mipakani
washirikiane na Serikali katika kuimarisha ulinzi na usalama.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amekagua ukarabati wa kituo cha afya cha Kata ya Mbekenyera
na kuwaeleza wananchi dhamira ya Serikali ya kuwahudumia.
Amesema Serikali
imetoa sh. milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya kujifungulia, maabara,
wodi ya wanawake na wanaume na chumba cha upasuaji.
“Serikali imeamua kuimarisha sekta ya afya kwa
kujenga na kuboresha vituo vya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za
afya karibu na makazi yao.”
Aidha,
Waziri Mkuu amewataka wananchi hao waendelee kuiunga mkono Serikali yao, ambayo
imedhamiria kuwatumikia ili waweze kupata maendeleo.
Pia,
Waziri Mkuu amekabidhi gari la kubeba wagonjwa katika kituo hicho. Gari hilo
limetolewa na Rais Dkt. John Magufuli ili kuimarisha huduma za afya kituoni
hapo.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment