“Kwa
masikitiko nimepokea taarifa ya kifo cha Mwenyekiti Mstaafu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma Dkt. Walid Amani Kabourou
kilichotokea usiku wa kuamkia leo tarehe 07 Machi, 2018 katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.
Dkt. Walid Amani
Kabourou atakumbukwa kwa mchango wake alipokuwa kiongozi katika nyadhifa
mbalimbali ndani ya CCM, na alipokuwa Mbunge wa Kigoma Mjini na Mbunge wa Bunge
la Afrika Mashariki.
Natoa pole
kwa familia yake, wana CCM wote, wananchi wa Kigoma, ndugu jamaa, marafiki na
wote walioguswa na msiba huu”
Hii
ni sehemu ya salamu za rambirambi alizotuma Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia
Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga
kufuatia kifo cha Dkt. Walid Amani Kabourou.
Pamoja
na salamu hizo, Rais Magufuli ameiombea familia ya Marehemu na wote
walioguswa na msiba huu kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu
katika kipindi hiki cha majonzi na amemuombea Marehemu apumzike mahali pema
peponi, Amina.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment