Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.

Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.

Nafasi Ya Matangazo

Friday, 27 April 2018

WIZARA YA HABARI YAOMBA BILIONI 33.349 MWAKA 2018/2019

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe akiwasilisha Bungeni hotuba ya makadirio ya bajeti ya mwaka 2018/2018 Jijini Dodoma, Wizara imeomba kuidhinishiwa kiasi cha Sh bilioni 33.349 kwa mwaka 2018/2019
Makatibu Wakuu wa Wizara ya Habari wakifuatilia
Watendaji kutoka Taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, wakifuatilia hotuba ya Bajeti ya Wizara yao iliyosomwa Bungeni jijini Dodoma leo.
Maofisa mbalimbali wa kutoka Wizara ya Habari wakifuatilia

Baadhi ya Watendaji kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, wakiwa pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha CUF, Prof. Ibrahim Lipumba (katikati) Bungeni leo.


Baadhi ya Watendaji kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, wakiwa pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha CUF, Prof. Ibrahim Lipumba (katikati) Bungeni janaWasanii na wadau mbalimbali wa habari wakiwa Bungeni Jijini Dodoma leo
Wasanii na wadau mbalimbali wa habari wakiwa Bungeni Jijini Dodoma leo


Wednesday, 25 April 2018

Rais Magufuli ahutubia Bunge la Afrika Mashariki Mjini Dodoma

Rais John Magufuli akisalimiana na Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Martin Ngoga


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa amesimama wakati wa Wimbo wa Taifa ulipokuwa ukipigwa katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma kabla ya kwenda kuhutubia Bunge la Afrika Mashariki linalofanyika kwa mara ya kwanza katika makao makuu ya Serikali mjini Dodoma.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwasili katika ukumbi wa Bunge wa Msekwa kwa ajili ya kuhutubia Bunge la Afrika Mashariki mjini Dodoma.Rais Dkt. John Magufuli amewataka Wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutilia mkazo ajenda zitakazoimarisha zaidi umoja, upendo, ushirikiano na mshikamano baina ya nchi wanachama ili kufanikisha jukumu muhimu la kupambana na umasikini wa wananchi na kukuza uchumi.

Rais Magufuli amesema hayo, Aprili 24, 2018 wakati akihutubia Bunge la Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani, katika ukumbi wa Pius Msekwa uliopo ndani ya viwanja vya Bunge Mjini Dodoma ambako Bunge hilo linafanyia vikao vyake kwa mara ya kwanza katika mji huo.

Rais Magufuli amesema Wabunge hao wanao wajibu wa kushughulikia migogoro ambayo imekuwa ikigharimu maisha ya wananchi, vikwazo vya biashara na uwekezaji, na kutilia mkazo ujenzi wa viwanda vitakavyochakata na kuzalisha bidhaa zitokanazo na rasilimali lukuki zilizopo ndani ya Afrika Mashariki ili manufaa ya rasilimali hizo yawanufaishe wananchi.

Ametaja miongoni mwa mambo yanayopaswa kutiliwa mkazo na nchi zote kuwa ni kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na uzalishaji wa umeme wakutosha na wenye gharama nafuu, ambavyo ni muhimu katika ujenzi wa viwanda.

“Tafiti zinaonesha gharama za usafiri kwenye ukanda wetu ni mara 4 hadi 5 ukilinganisha na gharama za Asia Mashariki, Marekani na Ulaya na zinachangia kuongezeka kwa gharama za bidhaa kwa asilimia 40.

“Umeme pia umeonekana kuwa sio mwingi, utafiti uliofanywa na taasisi ya Power Africa mwaka 2015 umeonesha kuwa nchi zote 6 za Jumuiya ya Afrika Mashariki zina takribani megawati 6,500 tu za umeme, hiki ni kiwango kidogo mno kuweza kuhimili mahitaji ya uchumi wa kisasa” amesisitiza Rais Magufuli.

Katika kutekeleza azma hiyo Rais Magufuli ametoa wito kwa nchi wanachama kubadilishana uzoefu wa namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza na kutekeleza miradi muhimu ya maendeleo, na pia ameshauri nchi wanachama zisitegemee misaada pekee na badala yake zifikirie kutekeleza miradi kwa fedha zake zenyewe ili kuokoa muda na kupunguza gharama za miradi husika.

Rais Magufuli amezungumzia juhudi zinazofanywa na Tanzania katika kufikia dhamira hiyo kuwa ni pamoja na kuanza ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge) kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma ambayo itaunganisha hadi nchi za Burundi, Rwanda na Uganda, kujenga meli katika ziwa Victoria, kutekeleza mradi wa uzalishaji wa umeme katika mto Rufiji (Stieglers’ Gorge), kununua ndege 6, kujenga barabara, kupanua bandari ya Dar es Salaam, ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania, kuboresha viwanja vya ndege 11 na amepongeza juhudi mbalimbali zinazofanywa na nchi nyingine wanachama wa Afrika Mashariki.

“Nataka kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wa Afrika Mashariki kuwa Serikali ninayoiongoza itaendelea kushirikiana na Bunge hili katika masuala mbalimbali ya kuiunganisha jumuiya yetu, na ninawaomba nanyi mtekeleze wajibu wenu wa kuwaunganisha na kuwaelimisha wananchi ili waone umuhimu wa jumuiya hii” amebainisha Rais Magufuli.

Kwa upande wake Spika wa Bunge la Afrika Mashariki Martin Ngoga amemshukuru Rais Magufuli kulihutubia Bunge hilo na amempongeza kwa jitihada zake za kujenga nidhamu ya utumishi wa umma, kuzidisha mapambano dhidi ya rushwa, kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, kukuza uwekezaji na biashara ikiwemo ujenzi wa viwanda na kuonesha uongozi mahiri, na ametoa wito kwa Watanzania kuunga mkono juhudi hizo.

Pamoja na Wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, viongozi wengine waliohudhuria wakati Mhe. Rais Magufuli akihutubia bunge hilo ni Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Naibu wa Pili wa Waziri Mkuu wa Uganda Mhe. Kirunda Kivejinja, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Mawaziri, Mabalozi wanaowakilisha nchi mbalimbali hapa nchini, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Monday, 23 April 2018

Rais Magufuli afungua jengo la PSPF, Ofisi ya makao makuu NMB Dodoma


 Jengo la ghorofa 12 la PSPF DODOMA PLAZA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 23 Aprili, 2018 amefungua jengo la mfuko wa hifadhi ya jamii wa PSPF, ofisi ya makao makuu ya benki ya NMB Mjini Dodoma na matawi mawili ya benki hiyo. 

Jengo la PSPF lenye ghorofa 11 lina ukubwa wa mita za mraba 15,741.60, limejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 30.56 na ndani ya jengo hilo ndimo benki ya NMB imefungua ofisi zake za makao makuu, tawi la benki kwa wateja maalum, na tawi la benki kwa wateja binafsi lililopewa jina la Kambarage kwa lengo la kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere.

Mkurugenzi Mkuu wa PSPF Bw. Adam Mayingu amesema jengo hilo ambalo tayari limeshapata wapangaji kwa asilimia 98 wengi wao wakiwa ofisi za umma, linatarajiwa kuzalisha Shilingi Bilioni 4.7 kila mwaka na litarejesha fedha za uwekezaji ndani ya miaka 8 na kwamba katika juhudi hizo hizo za kuunga mkono Serikali kuhamia Dodoma PSPF inatekeleza mradi mwingine wa ujenzi wa nyumba 500 kwa ushirikiano na mfuko wa hifadhi ya jamii wa Watumishi Housing.

Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya NMB Bi. Ineke Bussemaker amesema benki hiyo yenye matawi 218 ndio benki kubwa inayoendeshwa kwa faida hapa nchini na ikiwa na kiwango kidogo cha mikopo chechefu, imekuwa ikichangia katika bajeti ya nchini kupitia kodi na gawio ambapo katika miaka mitatu iliyopita imechangia Shilingi Bilioni 16.525 kila mwaka na katika sherehe hizo amechangia Shilingi Milioni 50 kwa maendeleo ya Dodoma.

Akizungumza kwa niaba ya Mke wa Baba wa Taifa Mhe. Mama Maria Nyerere, Mtoto wa Baba wa Taifa Bw. Makongoro Nyerere ameishukuru benki ya NMB kwa kutambua mchango wa Baba wa Taifa na kuamua tawi hilo liitwe jina lake la “Kambarage” na pia ametoa wito kwa vijana kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Mhe. Rais Magufuli.

“Mhe. Rais wewe chapa kazi, hawa wanaokushambulia hata wakati wa Baba wa Taifa walikuwepo na wengine walikimbilia nchi nyingine, wewe chapa kazi” amesisitiza Bw. Makongoro Nyerere.

Akihutubia kabla ya kufungua rasmi miradi hiyo, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza PSPF kwa kuwekeza katika jengo ambalo tayari limeshapata wapangaji na pia ameipongeza mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kuitikia wito wa kuwekeza katika viwanda 16 ambavyo vitazalisha ajira na kuchangia katika uchumi wa nchi.

Mhe. Rais Magufuli pia ameipongeza benki ya NMB kwa kazi nzuri inayofanya na kwa kuwafikishia huduma Watanzania wengi, lakini ametaka katika mwaka huu wa 2017/18 benki hiyo inayomilikiwa na Serikali kwa asilimia 32 iongeze gawio.

“Mwaka 2012/13 Benki ya NMB ilitoa gawio kwa Serikali la Shilingi Bilioni 10.805, mwaka 2013/14 ikatoa Shilingi Bilioni 14.301, mwaka 2014/15 ikatoa Shilingi Biliongi 16.525, mwaka 2015/16 ikatoa gawio hilohilo la Shilingi Bilioni 16.525 na mwaka 2016/17 ikatoa tena gawio hilohilo la Shilingi Bilioni 16.525, yaani miaka mitatu mfurulizo mnatoa gawio lilelile wakati mnatuambia faida ya benki imekua, nataka mnaoiwakilisha Serikali kwenye NMB mkaliangalie hili na gawio la mwaka 2017/18 liongezeke” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amejibu ombi lililotolewa na Mbunge wa Dodoma Mjini Mhe. Anthony Mavunde la kupunguzwa kwa tozo ya kodi katika mchuzi wa zabibu, na amewataka wadau wanaohusika wakiwemo wabunge kufanyia kazi ombi hilo kwa zao la zabibu na mazao mengine ya kilimo na mifugo hapa nchini ili tozo za kodi zisisababishe bidhaa za wazalishaji wa Tanzania kushindwa kushindana na bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka nje ya nchi.

Mhe. Rais Magufuli pia amemshukuru Mtoto wa Baba wa Taifa Bw. Makongoro Nyerere kwa ujumbe wake kwa Watanzania hasa vijana na amemhakikishia kuwa Serikali anayoiongoza ipo imara na itaendelea kuwa imara kusimamia misingi ya kulijenga Taifa.


WAZIRI MHAGAMA AMTAKA MSAJILI WA VYAMA KUCHUKUA HATUA KWA VYAMA VINAVYOKIUKA SHERIA NA MIONGOZO ILIYOPO.

Waziri wa Nchi Ofisi anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amemuagiza Msajili wa vyama vya Siasa kuchukua hatua kwa vyama vinavyokiuka sheria na miongozo ya vyama vya siasa.
Ametoa kauli hiyo leo (Aprili 23, 2018) alipokuwa akitoa maelezo ya ufafanuzi juu ya hoja za ofisi yake, zilizoainishwa katika Ripoti ya Mthibiti na Ukaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa fedha unoishia Juni 30, 2018 alipokutana na  waandishi wa habari Bungeni Dodoma.
Waziri Mhagama ameelekeza kuhakikisha vyama vyenye mapungufu upande wa hesabu zao basi wawasilishe kwa Msajili wa vyama ndani ya wiki 3 hadi 4.
“Namtaka Msajili wa Vyama achukue hatua za Kisheria pasi kusita kwa chama chochote kinachokiuka sheria ya vyama vya siasa Na. 2 ya mwaka 1992”.alisema Waziri Mhagama
Aidha amemtaka Msajili wa Vyama vya siasa nchini kuhakikisha anaweka miongozo na mpango kazi ili vyama vilivyozoea kutowasilisha hesabu zao viache mara moja kwa mujibu wa sheria.
Waziri Mhagama aliongezea kuwa taarifa ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ilibaini mapungufu kadhaa katika uendeshaji wa vyama vya siasa ikiwemo; Upungufu katika hesabu zilizowasilishwa chini ya viwango vya Kimataifa vya uandaaji wa hesabu katika sekta za umma na baadhi ya vyama kushindwa kuwasilisha hesabu zao kwa CAG kwa ukaguzi
Pamoja na hayo alibainisha kuwepo kwa vyama vya kisiasa visivyotumia rejista ya mali za kudumu ambapo vyama vinne ikiwemo;CHADEMA, NLD,ADC na Demokrasia Makini havina Daftari la kudumu la mali zao ikiwa ni kinyume na sheria zilizopo.
“Msajili wa Vyama nakuagiza kutoa maelekezo kwa kila chama cha siasa chenye usajili wa kudumu kuwa na regista ya mali zake ndani ya wiki tatu kuanzia leo kwani kukosa daftari la mali za kudumu ni kinyume na kifungu Na.14(1)(b)(ii) ya sheria ya vyama vya siasa Na.5 ya mwaka 1992.”alisisitiza Waziri.
Sambamba na hilo Waziri alimtaka Msajili wa Vyama vya siasa kuhakikisha vyama vyote  vinafuata miongozo yote ya kihasibu ili kuondokana na mapungufu ya kukosekana kwa nyaraka za malipo kama ilivyobainishwa na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ambapo alibaini vyama vitatu kati ya tisa vina nyaraka pungufu ikiwemo CHADEMA, SAU na ADC.
“Msajili wa vyama ahakikishe vyama vya siasa vinatekeleza miongozo yote kihasibu pamoja na kanuni za fedha, ambazo zinaelekeza nyaraka ziwe na viambatisho sahihi kwani ripoti ilibainisha vyama vitatu vilikuwa na malipo yenye nyaraka pungufu zenye thamani ya shilingi 735,978,559 ambapo ni kinyume na miongozo ya kihasibu na kukosa uhalali wa malipo hayo.”alisisitiza Waziri Mhagama.
AWALI:
Kifungu cha 14(1)(a) na (b)(i) cha Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258 [RE: 2015] kinaelekeza kuwa, kila chama cha siasa kinapaswa kutunza taarifa za mapato na matumizi, ikiwamo taarifa za mali zake. Vile vile, kinapaswa kuwasilisha kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, taarifa ya hesabu zake zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), pamoja taarifa ya mali zake.

Hivyo, Kifungu hicho kinampa mamlaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya ukaguzi wa hesabu za kila chama cha siasa chenye usajili wa kudumu. Katika mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni, 2017, CAG amefanya ukaguzi wa hesabu za Vyama vya Siasa kumi ikiwemo; CCM, CHADEMA, NLD, TLP, Demokrasia Makini (MAKINI), TLP, DP, SAU, AFP, CCK na ADC kati ya vyama vya siasa kumi na tisa vyenye usajili wa kudumu. Vyama vya Siasa tisa (9) havikuwasilisha hesabu zake kwake kwa wakati kwa ajili ya ukaguzi, hivyo hakukaguliwa.


SPIKA EALA AIPONGEZA TANZANIA KWA MAENDELEO

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Spika wa Bunge la Afrika ya Mashariki,  Mhe.Martin Ngoga kabla ya mazungumzo yao, Bungeni mjini Dodoma, Aprili 23, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katikia picha ya pamoja na Spika wa Bunge la Afrika ya Mashariki, Mhe. Martin Ngoga (watatu kushoto) baada ya mazungumzo, Bungeni mjini Dodoma, Aprili 23, 2018. Wengine pichani ni  Wabunge wa Bunge la Afrika ya Mashariki, kutoka kushoto  ni Dkt. Abdullah Hasnuu Makame, Fancy Nkuhi na Mariam Ussi Yahya.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wabunge wa Bunge la  Afrika ya Mashariki wanaoiwakilisha  Tanzania, Ofisini kwake mjini Dodoma Aprili 23, 2018.  Kutoka kushoto ni Josephine Lemoyan,  Happiness Lugiko, Mhandisi Habibu Mnyaa, Mariam Ussi Yahya, Alhaj Adam Kimbisa, Fancy Nkuhi na Dkt. Abdullah Hasnuu Makame. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wabunge wa Bunge la Afrika ya Mashariki wanaoiwakilisha Tanzania baada ya kuzungumza nao, Ofisini kwake mjini Dodoma, Aprili 23, 2018. Kutoka kushoto ni Mhandisi Habibu Mnyaa, Josephine Lemoyan, Dkt. Abdullah Hasnuu Makame, Alhaj Adam Kimbisa,  Mariam Ussi Yahya, Happiness Lugiko na  Fancy Nkuhi.
 ***************
SPIKA wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Dkt. Martin Ngoga ameishukuru na kuipongeza Serikari ya Tanzania kwa ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo wa reli kwa sababu inaleta manufaa hata kwa nchi jirani.

"Miradi hiyo ambayo kwa sasa inatekelezwa kwa kasi si kwamba inachochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania, bali hata wa nchi nyingi za jirani kwa kuwa nazo zitanufaika na miradi hiyo kwani si nchi zote zina bandari".

Dkt. Ngoga ameyasema hayo leo (Jumatatu, Aprili 23, 2018) alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Bungeni mjini Dodoma.

Amesema tayari wamejadili ripoti iliyotokana na ziara iliyofanywa na wabunge hao katika upande wa korido ya kusini na korido ya kaskazini ambapo wametoa mapendekezo yatakayofanyiwa kazi na baraza la mawaziri.

"Tayari tumeshajadili miswada miwili inayohusu Itifaki ya Sarafu Moja ambayo ni mswada wa taasisi ya Fedha na mswada wa Takwimu yote ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2017."

Pia Spika huyo amesema wamefurahia uwepo wao nchini, ambapo mbali na shughuli zao za kibunge pia kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma wameshiriki kampeni ya kukijanisha Dodoma kwa kupanda miti 1,000 kwenye eneo la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Kwa upande wake, Waziri Mkuu amesema amefarijika na uamuzi wa Bunge la EALA kufanya vikao vyake katika nchi wanachama kwa sababu unatoa fursa ya kujua mazingira ya nchi hizo pamoja na maendeleo yake.

Amesema nchi wanachama wanamatumaini makubwa na bunge hilo katika kuimarisha na kuboresha maendeleo ya mataifa yao, hivyo amewatakia mjadala mwema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewakaribisha wabunge hao na marafiki zao kuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali nchini ikiwemo ya viwanja, utalii, kilimo na madini.

Kwa mara ya kwanza vikao vya Bunge la Afrika Mashariki, (EALA) vinafanyika Dodoma katika ukumbi wa Bunge wa Msekwa uliopo ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vikao hivyo vilianza Aprili 17, 2018 na vinatarajiwa kumalizika Aprili 29, 2018.


Sunday, 22 April 2018

HATI YA KIWANDA CHA NYAMA SHINYANGA YAREJESHWA SERIKALINI

Mkurugenzi wa Ubinafsishaji  na Ufuatiliaji kutoka Hazina, Jones  Mwalemba  (kushoto) na Balozi  Fouad Mustafa kutoka kampuni ya Albwardy Investment Group wakikabidhiana hati ya Kiwanda cha Nyama Shinyanga. Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina (aliyekaa keti) alishuhudia makabidhiano hayo mjini Dodoma jana.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina (mwenye miwani) akishuhudia utiaji saini wa hati ya makabidhiano ya Kiwanda cha nyama cha Shinyanga. Hati hiyo zilisainiwa na Mkurugenzi wa Ubinafsishaji na Ufuatiliaji Jones Mwalemba(aliyekaa upande wa kushoto) kutoka Hazina kwa upande wa Serikali na Balozi Fouad Mustafa (aliyeinama upande wa kulia) kwa upande wa Kampuni ya Albwardy Investment Group aliyemwakilisha mmiliki wa Kampuni hiyo bwana Ali Saeed Juma Albwardy.
Hati ya kiwanda cha nyama cha Shinyanga iliyorejeshwa Serikalini na Kampuni ya Albwardy Investment Group baada ya kuuziwa kinyemela na kampuni ya Tripple S Beef kinyume na mkataba iliyoingia na Serikali, baada ya kampuni hiyo kushindwa kukiendesha kiwanda kwa miaka 11 tangu kilipokabidhiwa.

Na John Mapepele, Dar es Salaam

Kampuni ya Albwardy Investment Group imerejesha Serikalini hati ya kiwanda cha nyama cha Shinyanga na eneo la kupumzishia mifugo la kiwanda hicho iliyouziwa kinyemela na kampuni ya Triple S Beef Limited kutokana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina kutoa siku saba kwa wawekezaji Triple S Beef kusalimisha hati hizo kwa kushindwa kukiendeleza kwa miaka 11.

Akizungumza mara baada ya kusaini hati za makabidhiano ya hati hizo ofisini kwake jana, Waziri Mpina alitoa siku 14 kwa Salim Said Seif ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Tripple S Beef kujisalimisha Serikalini kwa kuvunja mkataba na serikali ambao ulimtaka kutommilikisha mwekezaji mwingine.

Hati hiyo zilisainiwa na Mkurugenzi wa Ubinafsishaji na Ufuatiliaji Jones Mwalemba kutoka Hazina kwa upande wa Serikali na Balozi Fouad Mustafa kwa upande wa Kampuni ya Albwardy Investment Group aliyemwakilisha mmiliki wa Kampuni hiyo bwana Ali Saeed Juma Albwardy.

Waziri Mpina alisema Kampuni ya Tripple S Beef ilinunua kiwanda hicho kwa shilingi milioni 63 tu mwaka 2007 na kukiza kinyemela kwa shilingi bilioni 8 kwa Kampuni ya Albwardy Investment Group mwaka 2015 kwa mujibu wa maelezo ya mwakilishi wa kampuni hiyo, balozi Fouad Mustafa.

Aidha alisema kiwanda hicho kilijengwa kwa bilioni 8.2 na kina ukubwa wa eneo la hekta 32 huku likiwa na ziada ya eneo lenye hekta 444 zakuhifadhia mifugo.

Aidha Mpina alisema mkakati wa Serikali kwa sasa ni kuvifufua viwanda vyote vya nyama nchini na kuvitangaza kwa wawekezaji makini ili waweze kuwekeza ili mifugo iliyopo iweze kupata soko la uhakika na viwanda vilipe kodi za serikali hatimaye kuliingizia taifa mapato.

“Tunaposema Serikali ya awamu hii ni ya viwanda tuna maanisha kwa vitendo na kuhakikisha viwanda vyote vinafanya kazi katika kiwango kinachositahili ili kujenga uchumi wa nchi yetu” alisistiza Mpina

Aliongeza kuwakwa kuwa hati za kiwanda cha Shinyanga zimekabidhiwa leo zabuni itatangazwa hivi karibuni ya kumpata mwekezaji mahiri, pamoja na kiwanda hicho viwanda vingine vitakavyotangazwa kupata mwekezaji mahiri ni pamoja na kiwanda cha nyama Mbeya na kiwanda cha Ngozi cha Mwanza.

Alisema Serikali itavitangaza viwanda hivyo pamoja kuvitengea maeneo makubwa ya kuhifadhia mifugo kabla ya kuichinjwa ili kuinua ubora na thamani ya nyama katika masoko ya kimataifa.

Akitoa taarifa ya Umilikishwaji wa kiwanda hicho, Mkurugenzi wa Ubinafsishaji na Ufuatiliaji Jones Mwalemba kutoka Hazina alisema kiwanda kilianza ujenzi wake mwaka 1975 na kwamba kimegharimu dola za kimarekani milioni 3.5 na kilijengwa na Serikali kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.

Alisema mwaka 2007 kiwanda hicho kilibinafsishwa kwa mwekezaji Tripple S Beef Limited lakini kutoka na matatizo ya uendeshaji kiwanda hicho kilifungwa mwaka 2017 na kukabidhiwa kwa Serikali.

Awali Waziri Mpina alipofanya ziara ya kushitukiza hivi karibuni katika kiwanda cha nyama cha Shinyanga aliagiza kwamba ifikapo Juni 30 mwaka huu kiwanda hicho kiwe kimempata mwekezaji ambaye ataanza kazi mara moja ya uchinjaji ili kutoa ajira na kuliingizia taifa mapato.

Alitoa siku saba kwa wawekezaji waliokuwa wanaendesha kiwanda hicho kusalimilisha hati za kiwanda na eneo mara mmoja ili Serikali iweze kufanya taratibu za kufufua kiwanda hicho.

Aidha amemuagiza Msajili wa Hazina kuanza uhakiki wa mali zote za kiwanda hicho baada ya kubainika wizi uliokithiri katika kiwanda hicho.

Pia Mpina ameamuru mmliki wa Kampuni inayolinda kiwanda hicho kukamatwa mara moja na kufikishwa katika mikono ya sheria kwa ajili ya kujibu mashitaka wa wizi wa mali za kiwanda hicho ambapo alimtaka Mkuu wa Mkoa kuhakikisha kuanzia sasa kiwanda hicho kilindwe na vyombo vya Serikali badala ya makampuni binafsi.


Friday, 20 April 2018

NDITIYE: SHULE ZA SEKONDARI KIBONDO ZAONGOZA UFAULU KITAIFA

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (Mb) akipokea Mwenge wa Uhuru baada ya kuwasili kwenye jimbo lake la Muhambwe Wilayani Kibondo mkoani Kigoma


Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kushoto) akishiriki uzinduzi wa Kituo cha Afya cha Mabamba kilichopo kwenye jimbo lake la Muhambwe wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru za kitaifa uliofanyiwa na kiongozi wa kitaifa wa mbio hizo Bwana Charles Kabeho (wa tatu kushoto) kwenye kata ya Mabamba wilayani Kibondo, Kigoma


Mkuu wa Wilaya ya Kibondo,Loyce Bura (kulia) akipokea  Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Woilaya ya Kakonko, Kanali Hossea Ndagala kwenye kijiji cha Mkubwa kilichopo mpakani mwa Wilaya ya Kibondo na Kakonko.


Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akigawa chandarua kwa wanawake wenye watoto baada ya uzinduzi wa kituo cha Afya cha Mabamba kilichopo kwenye jimbo lake la Muhambwe wilayani Kibondo, Kigoma wakati wa mbio za Mwenge wa uhuru za kitaifa


Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye, Mbunge wa jimbo la Muhambwe wilayani Kibondo, Kigoma akipiga ngoma kuburudisha wapiga kura wake wakati wa kupokea mbio za Mwenge wa Uhuru za kitaifa uliowasili kwenye Wilaya hiyo.

Shule za sekondari za Wilaya ya Kibondo zaongoza kwa ufaulu wa elimu katika ngazi ya kitaifa kwa miaka miwili mfululizo na kushika nafasi kati ya shule kumi bora za kitaifa na kuzishinda wilaya nyingine zote nchini.Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (Mb) wakati akipokea mbio za mwenge wa Uhuru ulipowasili Wilaya ya Kibondo kwenye jimbo lake la Muhambwe ukitokea Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma. Amesema kuwa Wilaya ya Kibondo imeongoza kwa ufaulu wa shule za sekondari kwa miaka miwili mfululizo ya masomo mwaka 2016 na 2017 ambapo kidato cha pili wameshika nafasi ya nane kitaifa na kidato cha nne wameshika nafasi ya tisa kitaifa na kuzibwaga sekondari nyingine zilizopo kwenye jumla ya Wilaya 187 nchini.

Nditiye amefafanua kuwa shule hizo zimezawadiwa kiasi cha shilingi milioni 680 na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Mpango wa Elimu kwa Matokeo (E4P) ambao umeleta chachu, ari na ushindani kwenye kiwango cha ufaulu kwenye shule mbalimbali nchini. Amefafanua kuwa fedha hizo zimetumika kugharamia upatikanaji wa miundombinu mbalimbali kwenye shule ya sekondari ya Malagarasi na ya Wasichana ya Kibondo.

Ameongeza kuwa ushindi huo umeleta chachu na mwamko zaidi kwa wanafunzi, walimu, wazazi, walezi na wadau wa elimu kwenye Wilaya hiyo ambapo wamejipanga kuchangia ujenzi wa miundombinu mbali mbali kwenye shule za Wilaya hiyo ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi ambapo imeendana na kauli Mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu isemayo, “Elimu ni Ufunguo wa Maisha, Wekeza Sasa kwenye Elimu kwa Maendeleo ya Taifa”.

Mhandisi Nditiye amesema kuwa Wilaya ya Kibondo inaunga mkono jitihada za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muunano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli za kutoa elimu bure nchini kote kwa shule za msingi na sekondari ambapo wazazi hawalipi ada yeyote hivyo inawawezesha kushirikiana kuendeleza miundombinu ya shule na mahitaji ya huduma nyingine ili wanafunzi waweze kujisomea na hivyo kuongeza ufaulu wao.

Naye kiongozi wa kitaifa wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu Bwana Charles Kabeho amewataka wazazi na walezi kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha kuwa wanamuunga mkono Mhe. Rais wa nchini yetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata sare za shule, vitabu vya masomo mbali mbali na miundombinu mingine ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa manufaa ya wanafunzi na walimu. 

Amefafanua kuwa azma ya Dkt. Magufuli ni kuwa na nchi ya viwanda na kufikia uchumi wa kati ambapo haya yote hayawezekani pasipo kuwa na taifa lenye rasilimali watu yenye elimu, ujuzi na maarifa ya kuendesha na kusimamia viwanda vyetu.

Bwana Kabeho amemshukuru na kumpongeza Mhandisi Nditiye kwa kutambua umuhimu wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa na kujumuika na wananchi wa jimbo lake la Muhambwe lililopo kwenye Wilaya ya Kibondo. “Mheshimiwa Nditiye, natambua majukumu uliyonayo katika kipindi hiki cha Bunge la bajeti ambalo linaendelea mkoani Dodoma lakini umejali na kuja kujumuika nasi katika kuzindua miradi mbali mbali ya maendeleo kwenye Wilaya hii,” amesema Kabeho.

Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa zimepokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Kibondo Mheshimiwa Loyce Bura kwenye kijiji cha Mkubwa mpakani mwa Wilaya ya Kibondo ukitokea kwenye Wilaya ya Kakonko. Mwenge umetembezwa kwenye Wilaya ya Kibondo na kuzindua miradi mbali mbali ya maendeleo yenye jumla ya thamani ya shilingi 1,512,000,000 ikiwemo kituo cha Afya cha Mabamba, kiwanda cha kusindika na kuzalisha unga wa muhogo, ofisi ya ushauri wa kibiashara, hoteli na kugawa asiimia kumi ya mapato ya Halmashauri hiyo kwa vikundi vya waasiriamali wanawake, vijana na walemavu kiasi cha shilingi milioni 58.

Mwenge umekabidhiwa kwenye Wilaya ya Kasulu ili kuendelea na mbio zake na kuzindua miradi mbali mbali ya maendeleo nchini ambapo makabidhiano hayo yamefanyika kwenye kijiji cha Mvugwe mpakani mwa Wilaya ya Kibondo na Kasulu.