Rais
Dkt. John Magufuli leo, Januari 31,2018 amezindua mfumo wa uhamiaji mtandao (e-Immigration) ambao utasaidia
kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi, kudhibiti ukusanyaji wa
maduhuli ya Serikali na kuimarisha utoaji wa huduma za kiuhamiaji kwa raia wa
Tanzania na wageni wanaoingia na kuishi hapa nchini kwa madhumuni mbalimbali.
Uzinduzi
wa mfumo huo umefanyika katika ofisi kuu ya uhamiaji Jijini Dar es salaam na
kuhudhuriwa na Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu
Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt. Ali
Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Seif Ali Iddi, na Waziri
Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Wengine
ni Jaji Mkuu wa Tanzania,Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid,
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Tulia Ackson
Mwansasu, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili,Dkt. Ali Hassan Mwinyi na Rais
Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.
Kabla
ya kuzindua mfumo wa uhamiaji mtandao, Rais Magufuli amekagua teknolojia
iliyotumika katika mfumo huo ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa alama za vidole na
baadaye kupatiwa pasipoti mpya ya kielekektronikia (e-Passport) ambayo pia imeanza kutolewa leo.
Rais Magufuli amempongeza Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Dkt. Mwigulu
Lameck Nchemba na Idara ya Uhamiaji kwa kufanikisha mchakato uliofanikisha
uwepo wa mfumo wa uhamiaji mtandao na kuanza kutoa pasipoti mpya ya
kielektronikia kwa gharama nafuu ya Shilingi Bilioni 127.2 ikilinganishwa na
makadirio yaliyowekwa awali ya Shilingi Bilioni 400.
“Hapa
tumeokoa fedha nyingi za Watanzania, kuna watu walikuwa wamejiandaa kutupiga na
kuchukua hizo Shilingi Bilioni 400, lakini tukatumia vyombo vyetu mbalimbali,
tukafanya uchunguzi na tumefanikiwa kutekeleza mradi huu kwa gharama nafuu”
amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha,
kwa kutambua kazi nzuri inayofanywa na idara ya uhamiaji baada ya kupokea
maelekezo yake ya kutakiwa kufanya mabadiliko makubwa, Mhe. Rais Magufuli
ameahidi kutoa Shilingi Bilioni 10 kwa ajili ya kujenga ofisi ya makao makuu ya
idara hiyo Mjini Dodoma.
“Kamishna
Jenerali Dkt. Anna Makakala na timu yako mnafanya kazi nzuri, ndio maana nimewanunulia
nyumba 103 kwa ajili ya wafanyakazi na leo nitawapa fedha nyingine Shilingi
Bilioni 10 mkajenge ofisi nzuri ya makao makuu, nyinyi endeleeni kuchapa kazi,
endeleeni kukamata wahamiaji haramu na endeleeni kukusanya mapato vizuri”
amesema Rais Magufuli.
Mapema
akitoa taarifa ya mfumo wa uhamiaji mtandao, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt.
Anna Makakala amesema mfumo huo ni muunganiko wa mifumo mbalimbali ambayo
imesanifiwa kufanya kazi kwa pamoja, kutoa taarifa kwa watumiaji na wadau wa
huduma za kiuhamiaji na kwamba kupitia mfumo huo idara ya uhamiaji inatarajia
kutoa pasipoti za kielektronikia (e-Passport),
viza za kielektronikia (e-Visa),
vibali vya ukaazi vya kielektronikia (e-Permit)
na udhibiti wa mipaka wa kielektronikia (e-Border
Management) kwa awamu nne hadi ifikapo mwisho wa mwaka huu 2018, pamoja na
kutoa pasipoti ya kielektronikia ya Afrika Mashariki ya Tanzania.
Balozi
wa Ireland hapa nchini, Paul Sherlock ameipongeza Tanzania kwa kufanikisha
mradi huu na kueleza kuwa mfumo huu wa uhamiaji mtandao ni alama muhimu ya
Taifa.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment