AGIZO la kuhakikisha Halmashauri
zote nchini zinachukua dawa za viuadudu zinazozalishwa kwa katika kiwanda cha
dawa hizo kilichopo Kibaha, Pwani imeanza kutekelezwa kwa Halmashauri za mikoa 14
kutakiwa kufika katika kiwanda hicho na kuchukua dawa hizo. Anaandika Frank Shija-MAELEZO
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa
na Kaimu Msemaji wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
–Idara Kuu ya Afya, Catherine Sungura, imesema kuwa Viuadudu hivyo vitaanza
kugaiwa katika Halmashauri za Mikoa 14 yenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya
ugonjwa wa Malaria.
“Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anapenda kuwatangazia
Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuwa Viuadudu vitaanza kugaiwa leo
Juni 26, 2017 kwa Halmashauri za Mikoa 14 yenye kiwango kikubwa cha
maambukizi ya ugonjwa Malaria” ilisema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo Mikoa
inayoanza kupata mgao huo, na iwango cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria
kwenye mabano kuwa ni pamoja na Kagera (41%), Geita (38%), Kigoma (38%), Ruvuma
(23%), Tabora (20%), Mtwara (20%), Mara (19%), Morogoro (14%), Shinyanga (17%),
Lindi (17%), Pwani (15%), Mwanza (15%), Katavi (14%) na Simiyu (13%).
Taarifa hiyo imebainisha kuwa
mikoa mingine ambayo haijatajwa itagaiwa Viuadudu katika awamu ijayo.
Aidha taarifa hiyo imewakumbusha
Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kufanya upuliziaji wa Viuadudu kwa kuzingatia
Miongozo ya Wizara ya Afya. Hii itawezesha kupata matokeo tarajiwa ya
kutokomeza mbu ili kudhibiti ugonjwa wa Malaria nchini.
“Wizara ya Afya inapenda
kumshukuru kwa dhati na kumpongeza Mhe.Rais Dkt. Magufuli kwa kuongeza chachu
katika Mapambano dhidi ya Malaria Nchini,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Rais John Pombe Magufuli alitoa
agizo hilo akiwa katika hafla ya uzinduzi wa barabara ya Bagamoyo – Makofi –
Msata wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Pwani iliyoanza tarehe
21 hadi 23, mwezi Juni 2017, ambapo alitoa siku 7 kwa Halmashauri zote nchini
kuhakikisha zimechukua dawa hizo ambazo yeye amezilipia.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment