Na Octavian Kimario-WHUSM Dodoma.
Wazo la kuwarudisha nchini Dinosaria halina
tija kutokana na ugumu wa Kiteknolojia na gharama ikilinganishwa na faida za
kuchukua hatua hiyo.
Akijibu swali la Mbunge wa Mchinga, Hamidu
Hassan Bobali lililo uliza,Ni nini kauli ya mwisho ya Serikali kuhusu faida
ambayo wananchi wa Lindi na Tanzania kwa ujumla wananufaika kutokana na mabaki
hayo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo
Makani amesema Tanzania itaendelea kusisitiza kupata manufaa kutokana na uwepo
wa Dinosaria wake huko Berlin-Ujererumani.
“Kufuatia majadiliano ya kina yaliyohusisha wataalamu
wabobezi katika masuala ya Malikale kutoka pande zote mbili imekubalika kuwa
Serikali ya Ujerumani itaendesha shughuli za utafiti zaidi huko Tendaguru na
katika maeneo jirani ili kuwezesha uchimbaji wa mabaki ya Dinosaria wengine
yanayoaminika kuwepo katika maeneo hayo pamoja na kuanzisha Kituo cha
Makumbusho ili shughuli za Utalii zifanyike katika eneo hilo na kuvutia watalii
kutoka nchini na nje ya nchi” alisisitiza Makani.
Kuhusu Serikali kupunjwa mapato yatokanayo na
viingilio katika Makumbusho ya Elimu Viumbe ya Berlin, Makani amesema jambo
hilo halina ukweli wowote kwani ni ngumu kufahamu ni kiasi gani hupatikana kama
kiingilio kuwaona Mijusi kutoka Tanzania kwakuwa Makumbusho hiyo ina kumbi
nyingi zenye masalia kutoka nchi mbali mbali za Afrika na gharama za kuendesha
Makumbusho hiyo hutolewa na Serikali ya Ujerumani.
Ameeleza kuwa Serikali ya Ujerumani
itafadhili zoezi la uimarishaji idara inayohusika na Malikale katika Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam na kuwezesha upatikanaji wa wataalamu wa kutosha wa fani
husika ilikuendeleza Utalii wa Malikale nchini.
Mijusi mikubwa (Dinosaria) ilichimbwa katika
Kilima cha Tendaguru,mkoani Lindi kati ya waka 1909 na mwaka 1913 na kupelekwa
katika makumbusho ya Elimu Viumbe ya Berlin nchini Ujerumani.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment