Na Anna Nkinda - JKCI
Jumla ya wagonjwa 11 wamefanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalum
ya matibabu ya moyo inayofanywa na madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo kutoka
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ushirikiana na madaktari wenzao wa
Taasisi ya Open Heart International ya nchini Australia.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo ambaye pia ni
Daktari bingwa wa upasuaji wa Moyo Bashir Nyangasa wakati akielezea jinsi kambi
hiyo ya upasuaji inavyoendelea kutoa matibabu kwa wagonjwa.
Dkt. Nyangasa alisema, “Kwa kushirikiana na washirika wetu wa OHI
tulianza kambi maalum ya upasuaji kuanzia tarehe 10/03/2017 hadi leo
tarehe 17/3/2017 tumefanya upasuaji kwa wagonjwa 11 ambao
wanaendelea vizuri, kati ya hao watoto ni tisa na watu wazima ni
wawili”,.
Dkt. Nyangasa alisema katika kambi hiyo ambayo inamalizika
tarehe 17/3/2017 walipanga kufanya upasuaji kwa wagonjwa 25 kati ya hao watoto
ni 15 na watu wazima ni 10.
Kuhusu uhitaji wa damu kwa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa Moyo
Dkt. Nyangasa alisema wagonjwa hao wanahitaji damu nyingi hivyo basi aliwaomba
wananchi wajitokeze kuchangia damu ambayo itatumika kwa wagonjwa.
“Tunaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kuchangia damu na
uchangiaji huu wa damu usifanyike mara moja bali uwe endelevu
kwani Taasisi inatoa huduma kwa wagonjwa wakati wote siyo wakati wa kambi
maalum za matibabu ya moyo pekee yake”, alisisitiza Dkt. Nyangasa.
Tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2017 JKCI kwa kushirikiana na
baadhi ya washirika wake wa nje ya nchi ambao ni Madaktari Afrika
wa Marekani, Hospitali za Apolo Bangalore na BLK zote za nchini
India na Open Heart International ya Australia wamefanya matibabu
ya moyo ya kufungua na bila kufungua kifua kwa wagonjwa wa moyo wanaotibiwa
katika Taasisi hiyo.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment