WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameumaliza mgogoro
wa mpaka wa ardhi baina ya vijiji vya wilaya za Kiteto na Kilindi uliodumu kwa muda
mrefu.
Mgogoro huo ambao ulianza kusuluhishwa tangu
mwaka 1997, umepata suluhu kwenye mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Waziri Mkuu
na kuwajumuisha Wakuu wa Mikoa hiyo miwili, Wabunge wa Kiteto na Kilindi, wenyeviti
wa Halmashauri na madiwani wa kata mbili za mpakani pamoja na wananchi wa kata
hizo.
Waziri Mkuu pia amewataka wanasiasa na
viongozi wengine kutowavuruga wananchi na badala yake wawaongoze vizuri na
kutoa maelekezo kwa mujibu wa sheria za nchi.
Ametoa
agizo hilo leo (Jumatano, Januari 18, 2017) wakati akizungumza na wananchi wa wilaya za
Kiteto na Kilindi katika kijiji cha Lembapili wilayani Kiteto, mkoani Manyara ambako
ni kuna mpaka wa wilaya hizo mbili alipokwenda kutatua mgogoro huo.
Amesema
viongozi wa wilaya hizo lazima wafuate sheria na wawaelekeze wananchi umuhimu
wa kuzingatia sheria za nchi ikiwa ni pamoja na kuheshimu mipaka iliyowekwa kwa
mujibu wa sheria ili kuepusha migogoro.
Akizungumzia
kuhusu mgogoro huo wa mpaka, Waziri Mkuu amesema nchi ilishaweka mipaka ya
mikoa na wilaya zake yote tangu zamani na kumbukumbu zipo zikiwemo za mpaka wa
wilaya hizo tangu mwaka 1961 kwa tangazo la Serikali namba 65 na
hakuna mabadiliko. Hivyo, aliwasisitiza wauheshimu na kuufuata.
Amesema
Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itakwenda
kuweka alama vizuri na viongozi wa wilaya hizo watashirikishwa. Alama hizo
zitawekwa na kifaa maalumu, hivyo amewataka wahusika watoe ushirikiano.
Waziri
Mkuu amesema katika kipindi ambacho Serikali itakuwa ikiweka alama hizo, wananchi
waendelee na shughuli zao hadi hapo zoezi litakapokamilika na wala wasibughudhiwe.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa siku nane kwa watu
wote wanaomiliki silaha katika wilaya za Kilindi na Kiteto wazipeleke kwenye
vituo vya Polisi ili zisajiliwe upya na kisha Wakuu wa Mikoa wafanye operesheni
maalum na atakayekutwa anamiliki silaha kinyume cha sheria achukuliwe hatua.
“Wakuu
wa Mikoa fanyeni ukaguzi maalum na atakayekutwa anamiliki silaha kinyume na
utaratibu achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria. Pia kuna watu wana mitambo ya
kutengenezea bunduki hapa, nao pia waisalimishe haraka,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Bw. William Lukuvi amesema mwanzoni mwa Februari wataalamu
wake watakwenda katika mpaka huo ili kuanza kuweka alama vizuri.
Amesema
baadhi ya viongozi huwa wana tabia ya kuzuia watendaji kutekeleza majukumu yao,
hivyo ametumia gursa hiyo kuwaomba viongozi wa wilaya hizo watoe ushirikiano.
Amesema
moja ya majukumu aliyopewa na Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli ni kuhakikisha
ndani ya miaka hii mitano anamaliza migogoro ya ardhi nchini ukiwemo huo wa Kilindi
na Kiteto.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment