BUNGE limepitisha Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/18 kwa asilimia 73.
Bajeti hiyo ambayo ni Shilingi Trilion 31
iliwasilishwa Juni 8 mwaka huu na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip
Mpango.
Akitangaza matokeo ya upitishwaji wa Bajeti
hiyo, Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas Kashililah alisema idadi ya wabunge wote
waliokuwepo 356 na kwamba waliopiga kura za ndiyo ni 260 huku kura za hapana
zikiwa 95.
“Kwa matokeo haya,Bunge limepitisha Makadirio ya
Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/18 kwa kupigiwa kura na
wabunge 260 sawa na asilimia 73,” alisema Dkt. Kashililah.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa kwa matokeo
hayo, Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai aliipongeza Serikali kwa niaba ya
Bunge pamoja mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu na watendaji wote
waliofanikisha mchakato huo.
“Mchakato huu umepitia katika hatua nyingi,
ninawaomba wabunge tuendelee kushiriki pia katika utekelezaji wake,” alisema.
Alisema Bajeti ya mwaka huu ni ya mfano kwa kuwa
Serikali imewasikiliza wananchi na kwamba hata hivyo matatizo ya nchi hayawezi
kumalizika kwa bajeti moja.
“Kwa hiyo tutaendelea kusema na kuishauri
Serikali ili nchi yetu iendelee kupiga hatua,” alisema.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment