SERIKALI
imetakiwa kuweka mkakati wa kuzilinda, kutunza na kuhifadhi barabara
zote zinazojengwa kwa kiwango cha lami nchini ili kuziwezesha kudumu kwa muda
uliokusudiwa na hivyo kuepuka gharama za ukarabati wa mara kwa mara.
Makamu Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu mheshimiwa Moshi Suleman Kakoso
amesema hayo mara baada ya kukagua barabara ya Dodoma – Babati yenye urefu wa
kilomita 263, ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami umekamilika.
“Hakikisheni ujenzi wa
barabara unaendana na uboreshaji wa huduma na maisha ya wananchi sehemu ambapo
barabara hizo zinapita ili kuchochea maendeleo”, amesema mheshimiwa Kakoso.
Makamu mwenyekiti huyo
amesema Kamati yake imeridhishwa na hatua zilizofikiwa za ujenzi wa barabara Dodoma
–Babati KM na daraja la Kelema linalounganisha Wilaya za Chemba na Kondoa
ambalo litawezesha barabara hiyo kupitika kwa uhakika wakati wote.
"Nimefurahishwa
na taarifa aliyoitoa Meneja mradi wa barabara hii kwamba pamoja na kujenga
barabara pia mkandarasi amechimba visima vya maji katika maeneo haya kwa ajili
ya kusaidia wananchi jambo ambalo ni jema na la kuigwa na makandarasi wengine”,
amesisitiza Makamu Mwenyekiti Kakoso.
Aidha, Makamu
Mwenyekiti ameitaka Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
(sekta ya ujenzi), kuwa na mpango endelevu wa kuweka kingo zinazoonesha
mipaka ya hifadhi ya barabara mapema na kwa uwazi ili kuepusha migogoro kwa
wananchi na ulipaji wa fidia zinazoweza kuepukika.
Ameongeza kuwa
Serikali ihakikishe inasimamia ipasavyo sheria zinazolinda barabara ikiwemo
kuweka alama za vivuko vya wanyama mahala panapostahili ili kudhibiti mifugo kukatiza
ovyo katika barabara.
Kwa upande wake Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi
Joseph Nyamhanga amesema katika kuhakikisha kuwa Serikali inailinda barabara ya
Dodoma - Babati tayari imeagiza uongozi wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa
wa Dodoma na Manyara kuhakikisha wanatenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa mizani
ili kudhibiti madereva wanaozidisha uzito usiokubaliwa kisheria.
Ameongeza kuwa Wizara inaendelea kutoa elimu kwa umma ili kuhamasisha utunzaji
wa miundombinu ya barabara kama kutomwaga mafuta barabarani,kutopitisha mifugo
na kutoiba alama za barabarani.
Kamati ya Bunge ya
Kudumu ya Miundombinu imefanya ziara katika mradi wa barabara ya Dodoma -
Babati (Km 263), na daraja la Kelema lenye urefu wa mita 205 lililopo wilaya ya
Chemba mkoani.
Dodoma na kuridhishwa na miradi hiyo ambapo wameitaka Serikali kupitia wizara ya ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), kuhakikisha inalinda na kutunza miundombinu hiyo ili idumu muda mrefu.
Muonejano wa Daraja hilo kwa chini.
Wajumbe wa Kamati wakipiga picha ya pamoja baada ya kukamilisha ziara yao.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment