KAIMU Rais wa Shirikisho la Mpira Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace
Karia, ameipongeza Taifa Stars kwa mafanikio ya kushika nafasi ya tatu
katika michuano ya Kombe la Castle la Cosafa - inayoandaliwa na Baraza
la Soka kwa nchi za Kusini mwa Afrika.
“Haya
ni matunda ambayo tunayaota kila wakati kwa timu kupata ushindi.
Tunawapongeza wachezaji, benchi nzima la ufundi likiongozwa na Kocha
Salum Mayanga, pamoja na watendaji wote kwa mafanikio ya timu yetu ya
Taifa Stars,” amesema Karia alipozungumza na TFF TV online.
Amesema
kwamba timu hiyo imeonyesha uzalendo wa hali ya juu katika kutafuta
mafanikio na ana imani kwamba Tanzania itashiriki michuano mingi ya
kimataifa kwa kuwa ina wachezaji wengi makinda huku TFF ikiendelea
kuwakuza wengine kwa ajili ya kutimiza ndoto za furaha ya Watanzania kwa
sasa na hapo baadaye.
Taifa
Stars jana usiku Julai 7, mwaka huu iliifunga Lesotho katika mchezo wa
kutafuta mshindi wa tatu wa michuano ya Castle Cosafa kwa mapigo 4-2 ya
penalti katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Moruleng nchini Afrika
Kusini.
Katika
mchezo huo wa jana, mabao ya Taifa Stars jana yalifungwa na Himid Mao,
Abdi Banda, Simon Msuva na Raphael Alpha. Taifa Stars walikosa mkwaju
mmoja wa penalti uliopigwa na Shiza Kichuya kwa kugongesga mwamba wa
juu, lakini Lesotho walikosa mapigo mawili - moja likiwa limegonga
mwamba wa pembeni na jingine likipanguliwa na Kipa Said Mohammed.
Taifa
Stars inatarajiwa kurejea usiku wa kuamkia kesho Jumapili Julai 9,
mwaka huu saa 9.30 usiku kwa ndege ya Shirika la Ndege la Rwanda ambako
itajipanga kwenda Mwanza siku ya Jumatatu saa 12.00 jioni kwa ndege ya
Shirika la Ndege la Fast Jet.
Itakwenda
Mwanza kujiandaa na mchezo dhidi ya Rwanda unaotarajiwa kufanyika
Jumamosi Julai 15, mwaka huu katika mchezo wa kufuzu kwa fainali za
Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani
(CHAN).
Timu
hiyo ambayo kwa mwaka huu imecheza mechi tisa za kimataifa na kushinda
mitano; kutoka sare miwili na kufungwa mmoja wa nusu fainali za Cosafa,
itakuwa na kikosi cha wachezaji 20.
Wachezaji
wanne hawatakuwako kwenye kikosi ambao ni majeruhi Mbaraka Yussuf na
Shaban Idd Chilunda kadhalika nyota wa kimataifa ambao hawahusiki na
mechi za CHAN ambao ni Thomas Ulimwengu na Elius Maguri.
Tayari
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga amewaongeza nyota wawili
katika kikosi hicho ambao ni John Bocco na Kelvin Sabato kutoka Majimaji
ya Songea kujaza nafasi za Chilunda na Mbaraka.
Pia
amemwita kinda Athanas Mdamu ambaye ni mchezaji mwanafunzi kutoka
Shule ya kukuza vipaji ya Alliance ya Mwanza ili kumpatia uzoefu kwenye
timu ya taifa ya wakubwa. Mdamu ataungana na timu huko Mwanza yaliko
makazi yake.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment