Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionyesha Kamumusi Kuu ya Kiswahili baada
ya kuizindua kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma Juni 19, 2017. Kulia ni
Mwenyekiti wa Bunge na Mbunge wa Ilala, Mussa Azan Zungu. Kushoto ni
Balozi wa Kiswahili Afrika, Mama Salma Kikwete. Wapili kushoto ni Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe wakati alipozindua Kamusi Kuu
ya Kiswahili kwenye ukumbi wa Bunge Mjini Dodoma Juni 19, 2017.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inatambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili kwa ustawi wa Taifa na katika kulinda umoja wa Kitaifa.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumatatu, Juni 19, 2017) wakati akizungumza na
wabunge, viongozi wa Serikali na wananchi waliohudhuria uzinduzi wa Kamusi Kuu ya Kiswahili uliofanyika kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma.
“Serikali inatambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili kwa ustawi wa nchi yetu na katika kulinda umoja wa Kitaifa. Hakika
lugha ya Kiswahili ndiyo inayotufanya tuwe Watanzania. Hivyo,
tunaithamini sana na kwetu hii ni lulu na tunu ya Taifa,” amesema.
Waziri
Mkuu amesema uzinduzi wa Kamusi hiyo unaenda sambamba na azma ya
Serikali ya kutumia Kiswahili kwenye shughuli zote za kitaifa kama vile
mikutano, mijadala, semina na ufundishaji shuleni.
Waziri
Mkuu alitumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe
Magufuli kwa kuhimiza matumizi ya Kiswahili kwenye mikutano na matukio
muhimu ya kitaifa, kama vile dhifa za kitaifa anazowaandalia wageni wake
kutoka nje ya nchi.
“Hata
alipokuwa kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa
Afrika wa mwaka 2017, Mheshimiwa Rais alitumia Kiswahili kuhutubia
mkutano huo. Amekuwa akifanya hivyo, hata kwenye mikutano ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki. Lengo lake ni kuitangaza lugha hii ya Kiswahili,”
alisema.
Aliwasihi
wazazi kote nchini wahakikishe kuwa watoto wao wanapata kamusi hiyo
kama moja ya nyenzo zao za kujifunza lugha ya Kiswahili. “Vilevile,
ninashauri, makundi mengine kama vile waheshimiwa wabunge, wanahabari,
wakalimani, wafasiri, waandishi na wahariri wa vitabu, maofisa
mawasiliano wa kwenye ofisi zetu, muone umuhimu wa kununua Kamusi hii,
ili iwasaidie kujiimarisha kwenye matumizi ya Kiswahili fasaha na
sanifu,” aliongeza.
Mapema, akizungumza
katika hafla hiyo fupi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,
Dkt. Harrison Mwakyembe alisema Kiswahili ni lugha ya pili inayotumiwa
na watu wengi zaidi barani Afrika lakini pia ni lugha ya 10 kati ya
lugha 6,000 zinazozungumzwa na watu wengi duniani.
Kwa upande wake, Katibu
Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Dk. Seleman Sewangi
alisema kazi ya kuandaa kamusi hiyo ilianza Agosti 12, 2011 na
kukamilika mwaka 2015 ambapo toleo la kwanza lilichapishwa.
Alisema
kamusi hiyo imekusanya maneno mengi makuu (vidahizo) kuliko kamusi
zilizotangulia na kwamba ya sasa ina maneno hayo 45,500.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment