SERIKALI imesema hadi ifikapo mwaka 2021 umeme wa uhakika wa megawati 5,000 utaanza kupatikana nchini baada ya kukamilika kwa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia
nguvu za maji katika maporomoko ya maji ya Mto Rufiji. Anaandika Greyson Mwase, wa WNM- Rufiji.
Naibu Waziri wa
Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani amesema umeme huo utazalishwa katika emneo la Stiegler’s Gorge lililopo
Rufiji mkoani Pwani ambao utaongeza umeme wa kiasi cha Megawati 2100
katika gridi ya taifa.
Dk. Kalemani
aliyasema hayo Juni 29, mwaka huu
katika ziara ya Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele aliyeambatana na
wataalam wa masuala ya ujenzi wa mitambo
ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji kutoka Ethiopia kwenye eneo la mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia
maporomoko ya maji ya Mto Rufiji ya Stieglers Gorge wilyani Rufiji mkoani Pwani.
Dk Kalemani alisema
kuwa kupatikana kwa umeme wa uhakika ifikapo mwaka 2021 kutachochea ongezeko la
viwanda hivyo kuongezeka kwa fursa za ajira na biashara na kukuza uchumi wa
nchi.
Alisema mradi huo mkubwa
ni moja ya mikakati ya Serikali kuhakikisha nishati inakuwa na mchango mkubwa
katika kufikia malengo ya
Dira ya Maendeleo ya Taifa yenye lengo la kuhakikisha kuwa nchi inatoka
katika orodha ya nchi maskini duniani na kuingia katika orodha ya nchi zenye
uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Alisisitiza kuwa
mbali na mradi huo mkubwa, serikali imeweka mikakati ya kutumia vyanzo vingine
vya nishati kama vile Gesi, Makaa ya Mawe, Jotoardhi, Upepo ili kuhakikisha
kuwa nchi inapata umeme wa uhakika.
Akielezea mafanikio
ya mradi huo mbali na upatikanaji wa umeme wa uhakika, Dk. Kalemani alisema
kuwa mradi huo utachochea ukuaji wa shughuli za uvuvi katika mkoa wa Pwani.
Alitaja mafanikio
mengine kuwa ni pamoja na kukuza sekta ya Utalii katika mkoa wa Pwani pamoja na kuzuia mafuriko
ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika mto Rufiji na kuathiri
makazi ya wakazi waishio pembezoni na
mto huo.
Akielezea hatua
iliyofikiwa ya maandalizi ya ujenzi wa mradi huo mkubwa, Dk. Kalemani alisema
baada ya timu ya wataalam kutoka Tanzania na Ethiopia kufanya ziara katika eneo
la mradi hatua inayofuatia ni wataalam kukaa vikao mbalimbali kujadili namna
bora ya kutekeleza mradi pamoja na kubadilishana uzoefu.
Alisema mara baada ya
ujenzi wa mradi huo kukamilika, moja ya kazi zitakazofanywa ni pamoja na ujenzi
wa njia ya kusafirisha umeme hadi Chalinze yenye urefu wa kilomita 200 na njia
ya kusafirisha umeme kutoka eneo la
Mradi hadi Singida yenye urefu wa
kilometa 800.
Waziri Kalemani
aliwataka wananchi na taasisi mbalimbali kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano ikiwa ni pamoja na kulinda vyanzo vya
maji hususan katika mto Rufiji.
Naibu Waziri wa
Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani akishuka kwenye helikopta, mara bada ya
kuwasili katika uwanja mdogo wa
Stieglers Gorge, Rufiji mkoani Pwani kabla ya kuanza kwa ziara ya Waziri
wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka
Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele aliyeambatana na wataalam wa masuala ya
ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa
kutumia maji kutoka Ethiopia pamoja na
wataalam wa masuala ya umeme na ujenzi
wa mabwawa kutoka Tanzania
Waziri wa Maji,
Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia,
Dk. Seleshi Bekele (kushoto) akieleza jambo kwa Mhaidrolojia Mwandamizi kutoka
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),
Stanislaus Kizzy (kulia) katika ziara hiyo. Anayesikiliza katikati ni Naibu
Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani.
Kaimu Kamishna wa
Nishati na Masuala ya Petroli, Mhandisi Innocent Luoga (kushoto) akielezea
maandalizi ya mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za maji wa Stieglers
Gorge kwa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Ethiopian
Construction Design and Supervision kutoka Ethiopia,
Dk. Negede Kassa (kulia) katika ziara hiyo.
Naibu Waziri wa Nishati
na Madini Dk. Medard Kalemani akishuka kwenye
boti kwa ajili ya kuelekea kwenye eneo la Stieglers Gorge kutakapojengwa
mradi huo.
Waziri wa Maji,
Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia,
Dk. Sileshi Bekele ( wa tatu kushoto)
akieleza jambo katika ziara hiyo.
Waziri wa Maji,
Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia,
Dk. Seleshi Bekele (wa saba kulia) na Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk.
Medard Kalemani (wa nane kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na timu ya wataalam kutoka Tanzania na Ethiopia katika ziara hiyo.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment