SERIKALI imepokea kwa masikitiko taarifa za
kushambuliwa na kujeruhiwa baadhi ya waandishi wa habari katika mvutano
uliotokea juzi jijini Dar es Salaam kati ya wafuasi wa pande mbili
zinazokinzana za Chama cha Wananchi (CUF).
Taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari Maelezo
kupitia kwa Mkurugenzi Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk
Hassan Abbasi ilisema kuwa serikali imepokea kwa masikitiko tarifa ya
kushambuliwa kwa waandishi wa habari waliokuwa kazini katika mkutano wa Chama
cha Wananchi CUF.
Taarifa hiyo ilisema kuwa ofisi ya Maelezo ilifuatilia
suala hilo na kubaini licha ya baadhi yao kujeruhiwa na kuripoti polisi, wapo
waandishi ambao vifaa vyao vya kazi pia vililengwa katika shambulizi hilo.
“Tunachukua fursa hii kulaani kitendo cha
kuumizwa wanahabari tena waliokuwa wamealikwa kuhudhuria mkutano huo. Ifahamike
kuwa uandishi wa habari ni taaluma adhimu na nadhifu inayopaswa kuheshimiwa,
kuenziwa, kulindwa na kutoingizwa katika migogoro ya pande zinazofarakana
katika jamii,”ilisema sehemu ya tarifa hiyo.
Kifungu cha 7 (1) (a) cha Sheria ya Huduma za
Habari Na. 12 ya mwaka 2016 kinaainisha uhuru wa wanahabari katika kukusanya
habari kwa muktadha wa kuwepo katika maeneo ya matukio kama hakuna sababu
nyingine za kuzuiwa. Misingi ya uhuru huu wa kitaaluma pia imesisitizwa katika
Ibara za 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 na 19 ya Mkataba
wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966 ambao nchi yetu
imeuridhia.
“Tunawatakia nafuu ya haraka wanahabari
waliojeruhiwa na wenzao wengine waliopatwa na jakamoyo katika tukio hilo,”ilisema
tarifa hiyo ya Mkurugenzi.
Aidha Dk Abbas katika tarifa hiyo amesema kwa
kuwa suala hilo tayari limeripotiwa polisi, aliwaomba wadau wote wa habari na
wanasiasa kwa sasa kutulia na kuviachia vyombo husika vilifanyiekazi ili hatua
stahiki za kisheria zichukuliwe.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment