Mwenyekiti
wa Kikundi Kazi, Bw. Peniel Lyimo (Katikati) akizungumza na wajumbe wa
Kikundi Kazi
(Hawapo pichani) wakati wa mkutano wa wadau wa kujadili uwekezaji
katika sekta ya kilimo uliofanyika katika Hoteli ya Court Yard, Dar es
Salaam. Wanaomsikiliza Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw.
Francis Assenga na Mkuu wa Kilimo na Fedha Vijijini
wa FSDT, Bw. Mwombeki Baregu (Kulia).
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga akizungumza juu ya umuhimu wa wadau
katika kuchagiza uwekezaji katika sekta ya kilimo nchini.
Mkuu
wa Kilimo na Fedha Vijijini wa FSDT, Bw. Mwombeki Baregu (Kulia)
akizungumza wakati wa
mkutano huo. Pichani ni Mwenyekiti wa Kikundi Kazi, Bw. Peniel Lyimo
(Katikati) na Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis
Assenga.
Mkurugenzi
wa Hazina na Utafutaji Fedha wa TADB, Bw. Albert Ngusaru akiwasilisha malengo ya mkutano huo.
Waumbe wa Kikundi Kazi cha Kuchagiza Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo nchini wakifuatilia mada
mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa.
Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya FSDT, Balozi Mwanaidi Maajar (Kulia) akitoa mchango wakati wa
Kikao Kazi cha Kuchagiza Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo nchini. Kushoto ni
Mkurugenzi wa Hazina na Utafutaji
Fedha wa TADB, Bw. Albert Ngusaru.
Na Mwandishi wetu
Benki ya Maendeleo ya Kilimo
Tanzania (TADB) kwa kushirikiana na Mfuko wa Kukuza Sekta ya Fedha (FSDT)
imewakutanisha pamoja wadau kutoka sekta mbalimbali za maendeleo nchini
kujadili masuala mbalimbali yatakayosaidia uwekezaji mkubwa katika sekta ya
kilimo Tanzania.
Akizungumza katika kikao kazi
hicho mwenyekiti wa Kikundi Kazi, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya
Kilimo, Bw. Peniel Lyimo alisema kuna haja ya dhamira ya dhati na
uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo nchini ili kusaidia juhudi za Serikali
za kuinua ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini.
Bw. Lyimo alisema kuwa ufinyu
mkubwa wa upatikanaji wa fedha mikopo kwa ajili ya maendeleo ya kilimo nchini
unachangiwa kwa kiasi kikubwa na mikopo mingi kutoka taasisi za fedha kuelekezwa
zaidi kwenye upande wa biashara za bidhaa hali inayorudisha nyuma mapinduzi
katika sekta ya kilimo nchini.
“Kuna haja ya kutafuta
suluhisho la changamoto za upatikanaji wa fedha mikopo kwa ajili ya Kuchagiza
na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha
kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini,”
alisema.
Akizungumzia umuhimu wa kikao
kazi hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga alisema
kikao hicho kinalenga kuwaleta wadau kutoka sekta mbalimbali ili kujadili kwa
kina njia sahihi za kuchagiza uwekezaji wenye tija katika kilimo nchini.
Bw. Assenga alisema kuwa kwa
kushirikiana na wadau mbali mbali wa maendeleo kutachagiza kusaidia uwekezaji
mkubwa kwenye Sekta ya Kilimo, na kuleta mapinduzi ya kilimo nchini.
“Kimsingi Kikao hiki kinalenga
kuanzisha mtandao mpana wa majadiliano na wadau mbalimbali, zikiwemo Wizara
zinazohusika na Kilimo na Taasisi mbali mbali za Serikali na Binafsi, ili
kukubaliana vipaumbele na namna ya kushirikiana katika kufanikisha utekelezaji
wa majukumu ya TADB katika kuleta mapinduzi ya kilimo nchini,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa
Kilimo na Fedha Vijijini wa FSDT, Bw. Mwombeki Baregu alisema kuwa FSDT
inalenga kushirikiana na wadau ili kuchagiza ushirikishaji mpana wa washirika
mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ili kuongeza uwekezaji katika sekta ya
kilimo nchini.
“Miongoni mwa vikwazo katika
kufikia ushirikishwaji wa fedha nchini Tanzania hasa katika uwekezaji katika
kilimo ni pamoja na ukosefu wa miundombinu sahihi ya soko na upatikanaji wa
fedha na huduma na bidhaa zake maalum katika kilimo, hivyo tunaamini kwa
kushirikiana na wadau tunaweza kutatua changamoto hizi,” alisema Bw. Baregu.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment