Mkurugenzi
wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Ephraim Kwesigabo akizungumza na
waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati akitangaza Mfumuko wa Bei
wa Taifa wa mwezi Desemba, 2017. Kulia ni Kaimu Meneja wa Takwimu za Bei na
Ajira, George Milinga.
Baadhi
ya waandishi wa habari wakifuatilia maelezo ya Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na
Takwimu za Jamii, Ephraim Kwesigabo (hayupo pichani) wakati akitangaza Mfumuko
wa Bei wa Taifa wa mwezi
Na Emmanuel Ghula
MFUMUKO
wa Bei wa Taifa kwa mwezi Desemba, 2017 umepungua hadi asilimia 4.0 kutoka asilimia
4.4 ilivyokuwa mwezi Novemba, 2017.
Akizungumza
na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na
Takwimu za Jamii, Ephraim Kwesigabo amesema kupungua kwa mfumuko wa bei
kunatokana na kupungua kwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa
mwezi Desemba, 2017 ikilinganishwa na kasi ilivyokuwa kwa mwezi Novemba, 2017.
“Mfumuko
wa Bei wa Taifa umepungua kutoka asilimia 4.4 mwezi Novemba, 2017 hadi kufikia
asilimia 4.0 mwezi Desemba , 2017 kutokana na kupungua kwa kasi ya upandaji wa
bei za bidhaa na huduma,” amesema Kwesigabo.
Mkurugenzi
huyo amesema baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kupungua kwa Mfumuko wa
Bei ni pamoja na unga wa muhogo uliopungua kwa asilimia 1.9, nyama kwa asilimia
3.4, samaki kwa asilimia 15.1, karanga kwa asilimia 3.5, mbogamboga kwa
asilimia 2.9, njegere kwa asilimia 7.5, viazi mviringo kwa asilimia 6.7, mihogo
mibichi kwa asilimia 16.8 na viazi vitamu kwa asilimia 12.5.
Amesema
Fahirisi za Bei zimeongezeka hadi 109.21 mwezi Desemba, 2017 kutoka 108.94
mwezi Novemba, 2017.
Kwesigabo amesema Mfumuko wa Bei kwa bidhaa za vyakula nyumbani na
migahawani kwa mwezi Desemba, 2017 umepungua hadi asilimia 6.7 kutoka asilimia
7.9 mwezi Novemba, 2017. Huku Mfumuko wa Bei ambao haujumuishi vyakula na
nishati kwa mwezi Desemba, 2017 ikipungua kidogo hadi asilimia 1.3 kutoka
asilimia 1.4 mwezi Novemba, 2017.
Amesema
wastani wa Mfumuko wa Bei wa Taifa (kutoka Januari hadi Desemba, 2017)
uliongezeka hadi asilimia 5.3 mwaka 2017 kutoka wastani wa asilimia 5.2
ilivyokuwa mwaka 2016 (kutoka Januari hadi Desemba, 2016). Kuongezeka kwa
wastani wa Mfumuko wa Bei wa Taifa kulichangiwa hasa na kuongezeka kwa kasi ya
kupanda kwa bei za bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula.
Wastani wa
Mfumuko wa Bei wa bidhaa za vyakula uliongezeka hadi asilimia 9.6 mwaka 2017
kutoka asilimia 7.6 mwaka 2016.
Kwesigabo
amesema Mfumuko wa Bei nchini Tanzania una mwelekeo unaofanana na baadhi ya
nchi nyingine za Afrika Mashariki ambapo nchini Kenya Mfumuko wa Bei wa mwezi
Desemba, 2017 umepungua hadi asilimia 4.50 kutoka asilimia 4.73 mwezi Novemba,
2017 na nchini Uganda umepungua hadi asilimia 3.3 mwezi Desemba, 2017 kutoka
asilimia 4.0 mwezi Novemba, 2017.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment