Mkuu wa Idara ya ardhi na makazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa, Jeswald Ubisimbali akifafanua jambo kuhusu utekelezaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika Halmashauri hiyo kupitia mradi wa ushiriki wa wananchi katika kilimo (CEGO) unaosimamiwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID).
**************
HALMASHAURI
ya Mufindi Mkoani Iringa kwa kushirikiana na Shirika la PELUM Tanzania kupitia
mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika sekta ya kilimo (CEGO) limepitisha Mpango
wa Matumizi ya Ardhi kwa vijiji vinne vya Halmashauri hiyo, hatua inayolenga kuongeza
wigo wa ushirikishaji wa jamii katika usimamizi wa rasilimali za ardhi.
Akizungumza katika mahojiano
maalum na Mwandishi wa Habari hii, Mkuu
wa Idara ya Ardhi na Makazi Wilaya ya Mufindi, Jeswald Ubisimbali alivitaja
vijiji vilivyopitisha Mpango huo kuwa ni Magunguli, Isaula, Usokami na Ugesa.
Ubisimali alisema
zoezi hilo limesaidia kwa kiasi kikubwa juhudi za Serikali katika kumaliza
migogoro ya ardhi katika maeneo hayo sambamba na kuongeza idadi ya vijiji
vilivyofanyiwa mpango wa matumizi ya Ardhi Wilayani humo.
“Kumekuwa na migogoro
ya ardhi katika wilaya ya Mufindi baina ya wakulima, wafugaji, na wawekezaji
wakubwa jambo ambalo limechangia kuzorotesha shughuli za maendeleo hivyo kupita
kwa Mipango ya matumizi ya ardhi kwenye vijiji vinne hemu ya mafanikio makubwa
kwa Serikali” alisema Ubisimbali.
Alisema kuwa kupitia
Mpango huo, Halmashauri ya Wilaya kwa kushirikiana na Shirika la PELUM Tanzania
limefanikiwa kupima zaidi ya vipande 500 katika kila kijiji kilichoanishwa
katika Mpango huo ikijumuisha makazi,
mashamba na Taasisi.
Aidha alisema mara
baada ya ya mipango hiyo kupita, Halmashauri ya Wilaya kwa kushrikiana na Shirika
la PELUM Tanzania linatarajia kuandaa hati miliki za kimila kwa kwa taasisi na wananchi
wote waliopimiwa maeneo yao kukabidhiwa hati zao kuonyesha umiliki halali wa
maeneo yao.
Ubisimbali alisema
kuwa Wilaya ya Mufindi ina jumla ya vijiji 121 ambapo ni vijiji 43 pekee ndivyo
vimefanyiwa Mpango wa matumizi ya Ardhi na hivyo kulitaka Shirika la PELUM
Tanzania kuendelea kutafuta miradi mingine ili kuweza kusaidia vijiji vingine
vilivyobaki katika mpango huo.
Alisema kutokufanyika
kwa Mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji vilivyobaki inasababishwa na
Halmashauri kuwa na bajeti finyu ikiwemo ukusanyaji wa mapato kutokufikia
malengo jambo linalochangia kuendelea kuwepo kwa migogoro ya ardhi kwenye
baadhi ya vijiji wilayani humo.
Ubisimbali alisema
vijiji 13 katika Wilaya hiyo ndiyo vyenze vilivyopo kwenye migogoro mikubwa ya
ardhi baina ya wananchi na wawekezaji
zikiwemo Kampuni za Mufindi Paper Mills, Green Resource Limited na SAO HILL
FOREST na hata hivyo jitihada mbalimbali zinafanywa na Halmashauri hiyo ili
kutatua changamoto hiyo.
Wilaya ya Mufindi ni
moja kati ya Wilaya sita zinazonufaika na mradi wa CEGO unaotekelezwa katika
Halmashauri sita nchini ikiwemo Morogoro Vijijini, Mvomero, Kongwa, Bahi,
Kilolo na Mufindi kupitia mashirika wanachama ya TAGRODE-Iringa,
UMADEP-Morogoro na INADES-Dodoma.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment