Mkurugenzi
wa Mawasiliano na Teknolojia wa DAWASCO, Kiula Kingu akifafanua jambo
kwa wanahabari wakati wa uzinduzi wa mfumo mpya wa mawasiliano katika
simu za mikononi inayowawezesha kupata taarifa zote muhimu za shirika
hil kwenye simu. Pamoja naye ni Meneja Uhusiano wa DAWASCO, Everlasting
Lyaro.
KATIKA kuhakikisha inarahisisha upatikanaji wa huduma ya majisafi na kwenda na mfumo wa
kisasa wa mawasiliano ya kiteknolojia, Shirika la MajiSafi na Majitaka Dar es
Salaam (DAWASCO) limezindua mfumo mpya wa mawasiliano ambao unalenga
kumrahisishia mteja kupata na kutoa taarifa zinazohusu huduma hiyo kwa haraka
zaidi.
Huduma hiyo mpya sasa itapatikana kwa wakazi wote wa jiji la Dar es
Salaam na Mkoa wa Pwani. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam,
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Teknolojia (TEHAMA) wa DAWASCO, Kiula Kingu
amesema lengo kuu la mfumo huu ni kumweka mteja karibu kihuduma na kila
mwananchi ana uwezo wa kutumia mfumo huo katika simu yake kupitia mitandao yote
ya simu za mikononi nchini.
Kingu ameongeza kuwa ili mteja kunufaika na mfumo huu anatakiwa
kuhakikisha ana simu ya mkononi ya “Smartphone” ambayo itamwezesha kupakua
mfumo huo mpya wa DAWASCO, kisha kujisajili kwa kuingiza akaunti namba yake ya
DAWASCO ambapo baada ya kufuata hatua zote za kujisajili mteja atatumiwa neno
la siri ambalo litamwezesha kuingia na kupata taarifa husika. “Sisi Dawasco
tumeona haja ya kujiboresha na kwenda sawa na teknolojia kwa kumletea mteja
wetu mfumo rahisi ambao utamwezesha kupata taarifa zetu kupitia simu yake ya
mkononi muda wowote,”alisema Bw. Kingu.
Naye, Meneja Uhusiano wa DAWASCO, Everlasting Lyaro, amewataka wananchi
wa Dar es Salaam na Pwani kupakua mfumo huu kwani ni rahisi kuutumia na hauna
gharama zozote. Anasema ni mfumo ambao utamrahisishia mteja kupata taarifa
muhimu zinazohusu huduma ya maji zikiwamo ankara ya mwezi, taarifa za lini
mteja alifungiwa huduma ya maji, muda ambao alifanya malipo, lini mita yake ya
maji ilisomwa na taarifa nyingine
nyingi.
“Nawasihi wateja wetu na wananchi wote kupakua mfumo huu mpya katika
simu zenu za mkononi ili kuweza kufurahia huduma zetu, hakuna gharama zozote
ambazo utatozwa. Kupitia mfumo huu utaweza kupata taarifa zote muhimu za huduma
ya majisafi zikiwemo taarifa za mivujo ya maji na ankara za maji za kila
mwezi,”amefafanua Lyaro.
Anasema kwa sasa wateja hawana haja ya kutumia muda mrefu katika
ufuatiliaji wa kuunganishwa huduma ya maji, bali kilichorahisishwa ni mteja
kuweka taarifa zake sahihi kwenye mfumo huo na DAWASCO itatumia taarifa hizo
kumtafuta mteja na kukamilisha taratibu nyingine hadi kuhakikisha mteja anapata
huduma ya maji.
Katika kutimiza agizo la Waziri
wa Maji na Imwagiliaji, Mhandisi Greyson Lwengwe la kuhakikisha wakazi wa Dar
es salaama, Miji ya Kibaha na Bagamoyo wanapata
huduma ya maji safi, DAWASCO imekua ikijitahidi kuwafikia wananchi kwa
njia na mbinu tofauti, kampeni tofauti kama 'mama tua ndoo ya maji kichwani'
huku maunganisho ya maji kwa mkopo yakisaidia upatikanaji na uboreshaji wa
huduma ya maji kwa maeneo mengi ya jiji la Dar es Salaam.
Mpaka sasa takribani watumiaji 25,000 wa mitandao ya simu jijini Dar es
Salaam wameshapakua mfumo huu na lengo la DAWASCO ni kuwafikia wakazi wengi
zaidi kwa kipindi kifupi.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment