WAZIRI wa Mambo ya Ndani
ya Nchi, Mwigulu Nchemba, anataraji kufungua Mkutano wa Maafisa wa Jeshi la
Zimamoto na Uokoaji Tanzania Bara utakaofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa
LAPF, mjini Dodoma.
Mkutano huo wa siku mbili
utakaofanyika Julai 13 na 14 ndio Kikao cha juu cha Jeshi ambacho huwahusisha
Makamanda wa Mikoa yote ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania Bara, Maafisa
Waandamizi wa Makao Makuu na Wakuu wa Vitengo vyote vya Jeshi la Zimamoto na
Uokoaji.
Kauli mbiu ya Mkutano wa
huo ni “KUOKOA MAISHA NA MALI NI WAJIBU WETU ILI KULETA MAENDELEO YA TAIFA,
ZINGATIA UTOAJI HUDUMA WENYE MAADILI NA UADILIFU ILI KULETA TIJA”
Taarifa iliyotolewa na Msemaji
wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, ASF. Puyo Nzalayaimisi ilisema Mkutano huo wa mwaka unalenga kutathimini
kwa pamoja utendaji wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika maeneo yake yote na
kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto zilizopo, kurekebisha dosari
zilizojitokeza na kujiwekea malengo ya kuboresha utendaji kazi kwa ujumla
katika mwaka unaofuata.
Nzalayaimisi alisema mada
kuu ya Mkutano huo itatolewa na Kamishna
Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye ambapo mada hiyo
itaendana na dhana nzima ya Sera na Dira ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Aidha Maamuzi na
mikakati mbalimbali itakayotolewa na Mkutano huu itakuwa na umuhimu wa pekee katika
kuandaa na kutoa miongozo mbalimbali ya utendaji katika kufanikisha utekelezaji
wa majukumu ya Jeshi hili kama dira inavyosema kuongoza katika utoaji huduma
bora ifikapo mwaka 2025.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment