Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na Serikali ya Kenya zimefanya mazungumzo ya pamoja na kutatua vikwazo
vilivyokuwa vikiikabili sekta ya biashara baina ya nchi hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo,
Jijini Dar es Salaam Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Balozi Dkt. Augustine Mahiga ametoa taarifa juu ya kumalizika kwa tofauti za
kibiashara baina ya nchi hizo.
“Bidhaa za Tanzania zilizowekewa
vikwazo na nchi ya Kenya ni unga wa ngano pamoja na gesi ya kupikia
(LPG). Aidha juhudi, za Serikali ya Tanzania kuona vikwazo hivyo vinaondolewa
na Serikali ya Kenya kwa wakati hazikuzaa matunda, hivyo Serikali ya Tanzania
nayo iliweka vikwazo kwa bidhaa za maziwa na sigara kutoka Kenya kuingia katika
soko la Tanzania,” amefafanua Dkt. Mahiga.
Amesema kuwa kutokana na mahusiano mazuri ya
udugu yaliyopo kati ya Tanzania na Kenya na kwa kujali manufaa mapana ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki viongozi wakuu wa nchi hizo mbili, Rais wa Jamhuri
ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. John Pombe Magufuli walikubaliana kuzungumza na kutoa vikwazo vya biashara
hizo.
Aidha, Dkt. Mahiga amesema, nchi hizo
zimekubaliana kuunda Tume ya pamoja ambayo itakuwa na jukumu la kuepusha
tofauti za kibiashara kati ya Tanzania na Kenya pamoja na kutolea ufumbuzi
changamoto za kibiashara kati ya nchi hizo mbili pindi zinapojitokeza.
Tume hiyo itaongozwa na Mawaziri wa mambo ya
Nje wa Tanzania na Kenya na kujumuisha mawaziri wanaohusika na masuala ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki, Biashara, Fedha, Mambo ya Ndani ya Nchi, Kilimo,
Uchukuzi na Utalii wa nchi hizo.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment