Rais Dkt. John Magufuli akizungumza na wananchi wa eneo la Tegeta kwa Ndevu jijini
Dar es salaam, baada ya wananchi hao kusimamisha msafara wake alipokuwa
safarini akirejea jijini Dar es salaam kutokea Mkoani Dodoma, Julai 27, 2017.
Sehemu ya wananchi wa eneo la Tegeta kwa Ndevu jijini Dar es salaam, wakimshangilia Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliposimama kuzungumza nao, alipokuwa safarini akirejea jijini Dar es salaam kutokea Mkoani Dodoma, Julai 27, 2017.
Rais Magufuli amewasili Jijini Dar es
Salaam leo tarehe 27 Julai, 2017 akitokea Mkoani Dodoma ambapo akiwa katika
eneo la Tegeta Wilaya ya Kinondoni amezungumza na wananchi waliosimamisha
msafara wake na kuwahakikishia kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua
mbalimbali za kukabiliana na kero na kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa
wananchi.
“Kwa
sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa Tegeta, nianze kwa kuwashukuru
sana, kwa kura nyingi mlizonipa ili niwe Rais wa Awamu ya Tano, nawashukuru
CCM, nawashukuru CHADEMA, nawashukuru CUF, nawashukuru ACT na hata wale ambao
hawana chama kwani wote kwa umoja wenu mlitanguliza maslahi ya Taifa na kumpa kura
mtu ambaye atalisaidia Taifa, na mimi nitafanya kazi kwa nguvu zangu zote na
kwa kumtanguliza Mwenyezi Mungu ili Watanzania wote hasa wanyonge ambao siku
zote walikuwa wakionewa” amesema Rais
Magufuli
Baadhi ya juhudi alizozitaja kufanyika tangu
aingie madarakani ni pamoja na kuondoa ada kwa wanafunzi wa shule za msingi na
sekondari, kuongeza mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka Shilingi Bilioni
371 hadi kufikia Shilingi Bilioni 483, kukabiliana na vitendo vya rushwa na
ufisadi na kulinda mali za umma hasa madini.
“Kwenye
madini tumeibiwa sana, nchi yetu ni kati ya nchi zinazoongoza kwa kuibiwa,
tumeibiwa kwa miaka 18, sasa imetosha” amesema
Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli ameipongeza Tume ya
Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa kuzuia
udahili wa wanafunzi wote wa mwaka kwanza katika vyuo vikuu 19 na kuzuia
udahili wa wanafunzi wa kozi 75 katika vyuo vikuu 22 kutokana na dosari
zilizobainika wakati wa ukaguzi wa ubora vyuo hivyo uliofanyika Oktoba 2016.
“Ndugu
zangu nchi hii ilishakuwa kila kitu hewa hewa, tumegundua wafanyakazi hewa
zaidi ya 19,500, kulikuwa na mikopo hewa ya wanafunzi, na naipongeza TCU kwa
kufungia baadhi ya vyuo kudahili wanafunzi, nafanya yote haya kwa ajili yenu,
nataka tuwe na nchi nzuri” amebainisha Rais Magufuli.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment