Rais
Dkt John Magufuli Akisisitiza jambo alipokuwa akiwahutubia Wananchi wa eneo la
Stendi ya Mabasi Msamvu Mkoani Morogoro
akitokea Mkoani Dodoma leo Julai 27,2917 na kutoa maagizo kadhaa.
RAIS John Magufuli amewataka
watu wote waliobinafsishiwa viwanda mkoani Morogoro kuvirejesha Serikalini endapo
wameshindwa kuviendeleza ili wapewe wawekezaji wanaoweza kuviendeleza na
kuzalisha ajira.
Rais Magufuli ametoa wito huo
leo wakati baada ya msafara wake uliokuwa ukitoka Dodoma kuelekea Jijini Dar es
Salaam kusimamishwa na wananchi wa Morogoro katika eneo la Msamvu mjini humo.
“Ninarudia wito wangu
niliokwisha kuutoa huko nyuma, kwamba wenye viwanda hapa Morogoro ambao
wameshindwa kuviendesha, na leo nataja akiwemo Mbunge wa hapa wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), narudia akiwemo Mbunge wa hapa wa CCM ambaye alibinafsishiwa
viwanda vingi, kama ameshindwa kuviendesha avirudishe ili tuwape watu wengine kwa
sababu vijana hawa wanakosa ajira, nazungumza kwa uwazi kwa sababu msema kweli
ni mpenzi wa Mungu” amesisitiza , Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli amewaagiza
viongozi wa Manispaa ya Morogoro na viongozi wa Mkoa wa Morogoro kuwaacha
wafanyabiashara ndogondogo wa Mji huo waendelee kufanya biashara zao katika
eneo la kituo cha mabasi cha Msamvu mjini humo hadi pale utaratibu mzuri
utakapowekwa.
Alisema hayo baada ya wananchi
wa Morogoro katika eneo la Msamvu kumueleza kero ya kunyanyaswa na Manispaa
ambao wamekuwa wakiwafukuza katika maeneo wanayofanyia biashara hasa baada
kituo cha mabasi cha Msamvu kujengwa upya.
Magufuli amemuagiza Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Morogoro SACP - Ulrich Matei kuhakikisha Askari Mgambo
hawawasumbui wafanyabiashara ndogondogo na amewataka wafanyabiashara hao
kutofanya vurugu wakati utaratibu mzuri unaandaliwa kwa ajili yao.
Katika hatua nyingine Rais Magufuli
amewapongeza wakulima wa mazao Mkoani Morogoro kwa kuongeza uzalishaji wa mazao
na amewataja wakulima wa Wilaya ya Kilosa kwa kuongeza uzalishaji kutoka
asilimia 42 msimu uliopita hadi kufikia asilimia 82 katika msimu huu.
Kuhusu mradi wa ujenzi wa reli
ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) Rais Magufuli ametoa wito kwa
wananchi wa Morogoro kujitokeza kupata ajira wakati wa ujenzi, lakini amewataka
waliojenga katika hifadhi ya reli kuondoa majengo yao kwa hiari.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment