Rais wa Dkt. John Pombe Magufuli
akihutubia wananchi wa Kibaha Maili moja katika viwanja vya Bondeni Mkoani
Pwani katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tatu Mkoani humo.
Wananchi akionesha hisia
zao wakati Rais, Dkt. John Pombe Magufuli
alipokuwa akihutubia Wananchi wa Kibaha Maili moja katika Viwanja vya Bondeni Mkoani
Pwani.
Rais Dkt. John Pombe
Magufuli amewahakikishia wananchi wa Pwani kuwa Serikali ya Awamu ya Tano
imejipanga kuhakikisha miradi mikubwa ya maendeleo yenye manufaa kwa mkoa huo
na Taifa kwa ujumla inatekelezwa kama alivyoahidi.
Rais Magufuli amesema
hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Bwawani Mjini
Kibaha akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya siku 3 Mkoani
Pwani.
Dkt. Magufuli ameitaja
miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard
Gauge) ambayo imeanza kujengwa, ujenzi wa barabara ya njia sita kati ya Dar es
Salaam na Chalinze yenye urefu wa Kilometa 128, ujenzi wa bandari kavu ya Ruvu
itakayopokea mizigo ya kutoka bandari ya Dar es Salaam na ujenzi wa mradi wa
umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge)
ambao mipango ya utekelezaji kwa kushirikiana na Ethiopia imeanza.
Amebainisha kuwa pamoja
na kutekeleza miradi hiyo Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuchukua hatua
dhidi ya watu wanaolihujumu Taifa ikiwemo kujihusisha na vitendo vya wizi na
rushwa na haitakatishwa tamaa na watu wanaolalamika na kubeza juhudi hizo.
“Stiegler’s Gorge mradi
ambao ulifanyiwa utafiti tangu enzi ya Mwl. Julius Nyerere, tukautelekeza,
nataka tujenge bwawa litakalozalisha umeme utakaotosheleza katika nchi yetu,
nchi ya viwanda, ili Watanzania wasilalamikie tena suala la umeme, nataka
tuachane na umeme wa matapeli wanaokuja hapa wanawekeza kwa lengo la kutuibia.
“Mimi nachukia wezi, na
kwa kweli wezi watakoma tu, awe mwizi wa Tanzania, awe mwizi wa Ulaya, awe
anatoka magharibi, mashariki, kaskazini au kusini, mwizi ni mwizi tu”
Amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli
amewapongeza viongozi na wananchi wa mkoa wa Pwani kwa Mkoa huo kutekeleza
vizuri sera ya ujenzi wa viwanda na ametaka viongozi wa Mikoa mingine waige
mfano huo ili kuwawezesha wananchi kupata ajira na kujiongezea kipato.
Kuhusu mauaji
yanayotokea katika Wilaya za Kibiti na Rufiji Mkoani humo, Rais Magufuli
amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kuwabaini
wanaofanya vitendo hivyo lakini amesema Serikali imeanza kuwashughulikia wanaowahalifu
hao na itahakikisha inakomesha tatizo hilo.
Mapema akitoa taarifa ya
maendeleo ya Mkoa wa Pwani, Mkuu wa Mkoa humo Mhandisi Evarist Ndikilo amesema
mkoa huo una jumla ya viwanda 371 vikiwemo viwanda 9 vikubwa na kwamba ujenzi
wa viwanda hivyo unaendelea katika hatua mbalimbali.
Kesho tarehe 21 Juni,
2017 Rais Magufuli ataendelea na ziara yake Mkoani Pwani ambapo atazindua
viwanda vitatu ambavyo ni kiwanda cha vifungashio cha Global Packaging Co. Ltd,
kiwanda cha matrekta cha Ursus-TAMCO Co. Ltd na kiwanda cha chuma cha Kiluwa
Steel Group.
Pia atazindua mradi wa
maji wa Ruvu na kuzungumza na wananchi.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment