Kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya
Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Bw. Lazaro Kitandu akizungumza na waandishi
wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu mfumo mpya wa ununuzi wa mbolea kwa
pamoja (Bulk Procurement System). Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Bw. Richard Kasuga.
**************
Na Fatma Salum (MAELEZO)
Serikali kupitia Mamlaka ya
Udhibiti wa Mbolea nchini (TFRA) imeanzisha mfumo mpya wa ununuzi wa mbolea kwa
pamoja (Bulk Procurement System) kutoka nje ya nchi utakaosaidia kupunguza bei
na kuhamasisha matumizi ya mbolea kwa wakulima.
Akizungumza na Waandishi wa Habari
leo Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Bw. Lazaro
Kitandu alisema uamuzi huo wa kuanzisha mfumo mpya umekuja baada ya Serikali
kugundua kuwa kwa muda mrefu matumizi ya mbolea hapa nchini si ya kuridhisha
kutokana na bei ya mbolea kuwa juu.
“Serikali kupitia Wizara ya
Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na wadau wa masuala ya mbolea imeanzisha
mfumo huu baada kupitia tafiti mbalimbali zilizofanywa na wataalam waelekezi wa
ndani na nje ya nchi na kutumia uzoefu wa taasisi nyingine zinazofanya ununuzi
wa bidhaa kwa pamoja” Alisema Kitandu.
Kitandu alieleza kuwa katika nchi
zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara (SSA), Tanzania ni mojawapo ya nchi zenye matumizi
ya chini ya mbolea kwa kutumia kilo 19 za virutubisho hivyo kwa hekta katika
ngazi ya wakulima wadogo ambapo kiasi hicho hakiendani na malengo ya azimio la
Maputo la nchi za SADC linalotaka kufikia angalau kilo 50 kwa hekta moja.
Alisema kuwa kwa msimu wa
mwaka 2017/2018 mfumo huo utaanza na aina mbili tu za mbolea ambazo ni mbolea
ya kupandia (DAP) na mbolea ya
kukuzia (UREA) na mbolea nyingine
zitafuata baadaye kadri itakavyoonekana mfumo huo kuleta manufaa kwa wakulima.
Akifafanua kuhusu faida za
mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja, Kitandu alisema utasaidia kuimarisha
utaratibu wa usambazaji wa mbolea ambapo wadau wote watakuwa na uhakika wa
upatikanaji wa mbolea kwa bei ya ushindani.
Kwa mujibu wa Kitandu pia mfumo
huo utawezesha wafanyabiashara wadogo kukua na kushiriki katika biashara ya
mbolea na kuimarisha mtandao wa usambazaji hadi ngazi ya mkulima.
“Ununuzi wa mbolea kwa pamoja
pia utasaidia kudhibiti bei ya mbolea iwapo kutajitokeza ongezeka lisilokuwa na
sababu (soko holela) kwa kuwa bei itatangazwa kwa kuzingatia bei halisi ya
mbolea, gharama halisi za usafirishaji wa mbolea, tozo mbalimbali na kiwango
stahiki cha faida ya mfanya biashara” alibainisha Kitandu.
Serikali kupitia mfumo huu
inatarajia matokeo chanya katika kupunguza bei ya mbolea kwa wakulima hivyo
kuongezeka kwa matumizi ya mbolea na uzalishaji wenye tija ili kuchochea
maendeleo ya uchumi wa viwanda.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment