Meneja Rasilimali Watu wa
Kampuni ya Saruji Tanga (TCPLC), Diana Malambugi (wa pili kulia), na Meneja
Mawasiliano na Mahusiano ya Nje wa Kampuni hiyo, Mtanga Noor (kulia), pamoja na
baadhi ya wanawawake wafanyakazi wa Kampuni ya Saruji Tanga pamoja na wake wa
wafanyakazi, wakishiriki mbio za mzoezi kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani
zilizoanza eneo la Kange na kumalizikia katika kiwanda cha kampuni hiyo,
Pongwe, nje kidogo ya mji wa Tanga mwishoni mwa wiki.
*************
WITO umetolewa kwa wafanyakazi
wanawake nchini kuwa na utaratibu wa kupima afya zao kwani mwanamke mwenye afya
bora ndiye atakayeweza kumudu vyema majukumu yake mahali pa kazi hivyo kuongeza
idadi kubwa ya wafanyakazi wanawake katika Tanzania ya viwanda.
Wito huo umetolewa na Kaimu
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk. Amina Mchalaganya wakati wa sherehe za
maadihimisho ya Siku ya Wanawake Duniani zilizoandaliwa na kampuni ya Saruji
Tanga (TCPLC) na kufanyika kiwandani hapo, Pongwe Tanga mwishoni mwa wiki.
Alisema wanawake hawana budi
kuwa mstari wa mbele katika kupima afya zao mara kwa mara hususan dhidi ya
magonjwa ya saratani yanayotishia afya za wanawake wengi hivyo kuathiri kiwango
cha cha uzalishaji mali.
“Natoa wito kwa wanawake wa
Tanga Cement pamoja na wanawake wote wa Mkoa wa Tanga kujitokeza kupima
afya hasa saratani ya shingo ya kizazi
katika Hospitali ya Mkoa ya Bombo tatizo
linaongoza kuathiri afya za wanawake wengi mkoani humu”, alisema.
Akizungumza katika hafla hiyo
Meneja Mawasiliano na Mahusiano ya Nje wa kampuni hiyo, Bi. Mtanga Noor alisema
wameazimia kudhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kufanya matembezi na kupima
afya zao kuunga mkono wito wa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kwamba
tufanye mazoezi kuepuka magonjwa ya kumbukiza.
“Mwanamke mwenye afya ndio
mchapa kazi, mwanamke mwenye afya ndiye atakayehakikisha familia yake ina afya,
familia ikiwa na afya taifa zima litakuwa na afya na watu tutaweza kuchapa kazi”,
alisema.
Akizungumzia ushiriki wa
wafanyakazi wanawake katika shughuli za uzalishaji kiwandani hapo Bi. Mtanga
alisema kama ambavyo watu wangetegemea kuona idadi ndogo ya wanawake wakifanya
kazi katika kiwanda cha kuzalishaji saruji kwao ni tofauti kwani wapo wanawake
wengi wanaofanya kazi katika idara za uhandisi, migodini na katika utawala.
Pamoja na hayo meneja mahusiano
huyo alitoa wito kwa wazazi wawahamasishe watoto wao wasiogope kusoma masomo ya
sayansi kwani baadhi yao huwaandaa watoto wao ili waje wafanye kazi wanazoona
ni nyepesi nyepesi pamoja na kuwa tayari wapo wanawake wahandisi, marubani,
madaktari lakini akasema bado idadi yao ni ndogo.
Tanzania iliungana na nchi
mbalimbali duniani kote kuadhimisha Siku ya Wanawake huku kauli mbiu ikiwa ni
‘Chochea Mabadiliko kuleta Usawa wa Kijinsia’.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment