Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania,Dkt. John Pombe Magufuli ametoa siku 7 kwa Wizara ya
Nishati na Madini kumega eneo lenye makaa ya mawe katika eneo la Ngaka lililopo
Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma na kuipatia kampuni ya Dangote ili iweze
kuzalisha yenyewe makaa ya mawe kwa ajili ya kiwanda chake cha saruji kilichopo
Mkoani Mtwara.
Mhe. Rais Magufuli
ametoa agizo hilo leo tarehe 05 Machi, 2017 wakati wa uzinduzi wa magari 580 ya
kusafirishia saruji ya Kampuni ya Dangote uliofanyika kiwandani hapo na
kuhudhuriwa na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo,
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango na Mmiliki wa kiwanda cha
Dangote Alhaji Aliko Dangote.
Pamoja kuagiza
kampuni ya Dangote ipatiwe eneo la kuchimba makaa ya mawe, Mhe. Dkt. Magufuli
ameitaka Wizara ya Nishati na Madini kuhakikisha inafikisha gesi katika kiwanda
hicho haraka iwezekanavyo lengo likiwa kuondoa vikwazo vya uhaba wa makaa ya
mawe na ukosefu wa gesi ambavyo vimekuwa vikisababisha uzalishaji wa saruji
kusimama mara kwa mara.
Mhe. Rais Magufuli
pia ameitaka kampuni ya saruji ya Dangote kuwasiliana moja kwa moja na Serikali
pale inahitaji huduma yoyote badala ya kuwatumia watu wa kati ambao wamekuwa
wakisababisha kuongezeka kwa gharama za uendeshaji na bidhaa na hivyo kuathiri
uzalishaji wa saruji wa kiwanda hicho.
Kabla ya kuzindua
rasmi magari hayo Mhe. Rais Magufuli amepokea kero za madereva ambao walifanya
usaili wa kuomba kazi ya kuendesha magari hayo tangu miezi miwili iliyopita,
ambapo wamemueleza kuwa menejimenti ya kiwanda hicho haijawaita kazini mpaka
leo licha ya kuwepo kwa malori mapya wanayopaswa kuendesha, huku Menejimenti
ikiendelea kutumia malori ya watu binafsi kupitia kampuni za kati ambazo ndizo
zimekuwa zikitumika kutoa huduma nyingi kwa kiwanda.
Kufuatia
malalamiko hayo Mhe. Dkt. Magufuli amemshauri mmiliki wa kiwanda hicho Alhaji
Aliko Dangote kuiangalia vizuri Menejimenti yake na kuitaka iachane na
wafanyabiashara wa kati ikiwemo kampuni moja iliyotaka kupewa zabuni ya kupokea
gesi kutoka Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kisha kuzalisha umeme na
kuiuzia Dangote.
"Ndugu Alhaji
Aliko Dangote, iangalie vizuri Menejimenti yako, inawatumia watu wa kati na
ndio hao wanaosababisha matatizo, na mimi nimeshaiagiza wizara hakuna kuuza
gesi kwa watu wa kati, tunataka tukuletee gesi wewe mwenyewe na uzalishe umeme
wewe mwenyewe" amesisitiza Rais Magufuli.
Kwa upande wake
Alhaji Aliko Dangote ameelezea kufurahishwa kwake na uwekezaji wa kiwanda hicho
uliogharimu Dola za Marekani Milioni 650 na kwamba kiwanda hicho
kitakachozalisha tani Milioni 2 za saruji mwaka huu kinatarajia kufikia
uzalishaji wa tani Milioni 3 mwaka ujao, kuzalisha ajira 20,000 huku kikiwa
kimesaidia kupunguza bei ya saruji nchini kutoka Shilingi 15,000/- kwa mfuko
mmoja kilo 50 hadi kufikia Shilingi 10,000/-.
Alhaji Aliko
Dangote ameongeza kuwa tangu kampuni yake ianze kuuza saruji bei ya bidhaa hiyo
sokoni imeshuka kutoka Shilingi 15,000/- kwa mfuko mmoja wa kilo 50 hadi
kufikia Shilingi 10,000/- na kwamba imeamua kununua magari ya kusafirisha
saruji ili iweze kusambaza saruji hiyo nchi nzima kwa gharama nafuu ambayo
watanzania wengi wataimudu.
Nae Waziri wa
Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amesema licha ya kuzalisha ajira, tangu
kampuni hiyo ianze shughuli zake imeshalipa kodi kiasi cha Shilingi Bilioni
46.139 na kodi inatarajiwa kuongezeka kadiri uzalishaji unavyopanda.
Wakati
huo huo, Mhe. Rais Magufuli amezindua kituo cha kupooza
umeme cha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kilichopo mjini Mtwara ambacho
kinajengwa kwa fedha na wataalamu wa TANESCO kwa gharama ya Shilingi Bilioni 16,
mradi ambao utahusisha ujenzi wa njia ya umeme ya kilovoti 132 kutoka Mtwara
hadi Lindi na hivyo kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme katika Mji wa Lindi.
Mhe. Dkt. Magufuli
amempongeza Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo,
Menejimenti na wafanyakazi wa TANESCO kwa kazi nzuri wanayofanya iliyowezesha
usambazaji wa umeme kuongezeka hadi kufikia asilimia 46 ya nchi nzima, lakini
ametoa maagizo kwa TANESCO kuwakatia umeme wote wenye madeni bila kujali kama
ni taasisi ya umma ama binafsi.
Mapema leo asubuhi
Mhe. Rais Magufuli amesali ibada ya Diminika ya kwanza ya Kwaresma katika
Kanisa la Watakatifu wote, Jimbo Katoliki la Mtwara ambako amechangia Shilingi
Milioni 1 na mifuko 200 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa Kanisa na ukarabati
wa Kanisa na amewataka wananchi wa Mtwara kushikamana kuiombea nchi na kufanya
kazi kwa ajili ya maendeleo ya mkoa na Taifa zima.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment