Rais
wa Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Balozi wa China hapa nchini Dkt. Lu Youqing
mara baada ya kuweka jiwe la Msingi katika Kiwanda kikubwa cha kutengeneza
Vigae(Tiles ) cha Good Will kilichopo katika kijiji cha Mkiwa, Mkuranga mkoani
Pwani. Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha vigae laki nane kwa siku na
mwekezaji ametumia zaidi ya Dola mil.50 katika uwekezaji huo.
Rais
Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na Balozi wa China hapa nchini Dkt. Lu
Youqing akikata utepe kuashiria uzinduzi
rasmi wa Kiwanda hicho cha vigae kilichopo Mkiwa Mkuranga mkoani Pwani.
Rais
Dkt. John Pombe Magufuli akisikiliza maelezo kutoka kwa Mwakilishi wa Kiwanda
hicho cha y Vigae cha Good Will, Huang Heng Chao kutoka kwa Kiwandani hapo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, ameweka jiwe la msingi la kiwanda cha
kutengeneza vigae (Tiles) cha Kampuni ya Goodwill Tanzania Ceramic Limited
kilichopo katika Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani.
Kiwanda hicho kikubwa Afrika
Mashariki na Kati ambacho ujenzi wake umegharimu Dola za Marekani Milioni 50
kwa awamu ya kwanza kitakuwa na uwezo wa kuzalisha mita za mraba 80,000 za
vigae kwa siku, kitazalisha ajira za moja kwa moja 1,000 na ajira zisizo za
moja kwa moja 2,000.
Akizungumza kabla ya kuweka
jiwe la msingi la kiwanda hicho Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na
uwekezaji Dkt. Adelhelm Meru amesema pamoja na kiwanda hicho, tangu Serikali ya
Awamu ya Tano iingie madarakani jumla ya viwanda 2,169 vinavyojumuisha viwanda
vidogo, vya kati na vikubwa vimesajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC)
na vipo katika hatua mbalimbali za kukamilika.
Nae Balozi wa China hapa
nchini Mhe. Dkt. Lu Youqing amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kutilia mkazo
juhudi za kukuza uchumi zilizowezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye
uchumi unaokuwa kwa kasi kubwa Barani Afrika na amebainisha kuwa China
itaendelea kushirikiana na Tanzania kuendeleza uwekezaji nchini Tanzania
ikiwemo kujenga viwanda.
"Mhe. Rais kwa mujibu wa
takwimu za TIC mpaka mwisho wa Juni 2016 uwekezaji wa moja kwa moja kutoka
China umefikia Dola za Marekani Bilioni 6.6 na umezalisha ajira za moja kwa moja
kwa Watanzania 150,000 na zisizo za moja kwa moja 450,000 na kiwanda hiki cha
Goodwill Tanzania Ceramic Limited kimejengwa na wawekezaji kutoka China, vipo
viwanda vingine vingi vinajengwa, Mbunge wa Mkuranga ameniambia kuwa kuna
viwanda zaidi ya 50 vya Wachina vinavyojengwa hapa Mkuranga, nimefurahi sana
kuona karibu kila sekta Watanzania wanafurahia ushirikiano wa Tanzania na
China" Amesema Balozi Dkt. Lu Youqing.
Akizungumza baada ya
kutembelea kiwanda hicho, Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Menejimenti ya kiwanda
hicho kwa uwekezaji huo na ameelezea kufurahishwa kwake na kutumika kwa
teknolojia ya kuyeyusha mchanga wa kutengenezea vigae.
Kufuatia kujionea mwenyewe
teknolojia hiyo, Dkt. Magufuli amepiga marufuku usafirishaji wa mchanga wa
madini nje ya nchi na ametaka mchanga wote ufanyiwe uyeyushaji hapa hapa
nchini.
"Nchi hii tumechezewa vya
kutosha, sasa nyinyi hapa mnayeyusha mchanga kwa kuuchemsha hadi nyuzi joto
1,000 wakati wengine wanasafirisha mchanga nje ya nchi wakati uchemshaji wake
hauhitaji kufika hata nyuzi joto 1,000, naiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na
Uwekezaji na Wizara ya Nishati na Madini kuwa kuanzia sasa ni marufuku kusafirisha
mchanga nje ya nchi" amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Baada ya kuweka jiwe la msingi
la kiwanda cha kampuni ya Goodwill Tanzania Ceramic Limited Mhe. Rais Magufuli
ameendelea na ziara yake kwa kuzungumza na wananchi wa Ikwiriri na kupokea kero
zao ambapo amewaagiza Mamlaka ya Maji katika Mji huo kuhakikisha mradi wa maji
uliojengwa na kukamilika tangu mwaka 2015 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 5,
unaanza kutoka maji kabla ya mwisho wa Mwezi huu na pia amepiga marufuku
utozaji wa ushuru kwa wafanyabiashara wadogowadogo wa mazao.
Mhe. Rais Magufuli pia
amepokea kero za wananchi wa Somanga, Nangurukuru na Mchinga Moja na huko kote
amewataka wananchi kufanya kazi kwa bidii ikiwemo kuzalisha mazao ya chakula
cha kutosha huku akiweka bayana kuwa Serikali haitatoa chakula cha msaada kwa
watakaopatwa na njaa ilihali wanaweza kuzalisha chakula katika maeneo yao.
"Najua mmezoea kusikia
maneno mazuri mazuri kuwa hakuna atakayekufa kwa njaa, sasa mimi nasema
usipofanya kazi, usipolima mazao na kupata chakula wakati mvua inanyesha
Serikali haitatoa chakula cha bure kwa wenye njaa, ni lazima tufanye kazi, sasa
hivi mvua zinanyesha limeni mazao ya chakula" amesisitiza Mhe. Rais
Magufuli.
Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli
amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Lindi kushughulikia migogoro ya wakulima na
wafugaji iliyoanza kuibuka mkoani humo, ameahidi kutoa Shilingi Milioni 20
kusaidia ujenzi wa Zahanati ya Somanga, amewaagiza Viongozi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Kilwa kujenga kituo cha mabasi cha Nangurukuru na pia amemuagiza
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Mchinga
Mhe. Hamidu Bobali kuhakikisha anapeleka Daktari katika kijiji cha Mchinga Moja
ili kutatua kero ya wananchi kukosa huduma ya matibabu.
Mhe. Rais Magufuli ataendelea
na ziara yake kesho Machi 03, 2017 Mkoani Lindi.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment