Na Basil Msongo
RAIS John Magufuli ameagiza
kwamba, ikifika Jumatano wiki ijayo, mazungumzo kati ya Wizara ya Nishati na Madini na
bilionea Aliko Dangote yawe yamekwisha ili gesi ipatikane kwenye kiwanda cha
saruji cha mfanyabiashara huyo.
Ameagiza kwamba, Wizara hiyo
ijadiliane na Dangote mwenyewe badala ya kupitia kwa watu aliowaita kuwa ni
matapeli.
Ametoa maagizo hayo leo kabla
ya kuzindua magari 580 ya Dangote yatakayotumika kusambaza saruji kutoka
kiwandani hapo.
Amewatuhumu baadhi ya
wawakilishi wa mfanyabiashara huyo kuwa wanachelewesha uwekezaji na huenda wanashirikiana
na viwanda vingine vya saruji kuihujumu Serikali.
“Inawezekana watu wako
wanaokuwakilisha wana matatizo, hii ni meseji kwa mheshimiwa Dangote mwenyewe,
ni lazima awe mwangalifu kwa watu wake”amesema Rais Magufuli.
Amesema, mfanyabiashara huyo
ni mwekezaji muhimu sana Tanzania kwa kuwa amewezesha maelfu ya Watanzania
kupata ajira na pia Serikali inapata mapato kupitia kodi.
Amemshukuru Dangote kwa
kuwekeza Tanzania na pia amemshukuru Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kwa
kusimamia mchakato uliowezesha kujengwa kwa kiwanda kikubwa cha saruji mkoani
Mtwara.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment