Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (kushoto).
**************
Na Hamza Temba-WMU-Dar es Salaam
Wizara ya Maliasili na Utalii imetangaza rasmi viwango vipya vya malipo ya ada kwa Mawakala wa kusafirisha watalii nchini baada ya kukamilika kwa marekebisho ya kanuni ya ada na tozo za biashara ya utalii yaliyofanyika mwezi Desemba mwaka jana, 2017.
Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Maj. Gen. Gaudence Milanzi, imeeleza kuwa baada ya kukamilika kwa marekebisho hayo ya kanuni, Tangazo la Serikali namba 506 la tarehe 29 Desemba, 2017, limeweka viwango vipya vya ada kwa mawakala wa kusafirisha watalii (Tour Operators na Safari Outfitters).
Taarifa hiyo imeeleza viwango hivyo kuwa ni shilingi sawa na dola za Kimarekani 500 kwa kampuni za wazawa zenye umiliki mkubwa wa raia wa Tanzania na zinazomiliki gari 1 hadi 3.
"Shilingi sawa na dola za Kimarekani 2,000 kwa kampuni zenye gari 4 hadi 10, shilingi sawa na dola za Kimarekani 3,000 kwa kampuni zenye gari 11 hadi 50 na shilingi sawa na dola za Kimarekani 5,000 kwa kampuni zenye kumiliki gari 51 na kuendelea", imeeleza taarifa hiyo.
Kwa upande wa kampuni za kigeni zenye umiliki mkubwa wa raia wa kigeni na zinazomiliki gari 10 hadi 30 zitalipa ada ya shilingi sawa na dola za Kimarekani 5,000, kampuni zenye gari 31 hadi 50 zitalipa shilingi sawa na dola za kimarekani 7,500 na na kampuni zenye gari 51 na kuendelea zitalipa shilingi sawa na dola za Kimarekani 10,000.
Kufuatia marekebisho hayo, muda wa kutumika kwa leseni za mwaka 2017 za Wakala wa kusafirisha watalii (Tour Operators na Safari Outfitters) umesogezwa mbele hadi tarehe 31 Januari, 2018 ili kuwezesha maandalizi ya kuingia kwenye mabadiliko ya viwango hivyo vipya.
Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa maombi ya usajili na leseni za biashara ya utalii na leseni za waongoza watalii kwa mwaka 2018 kwa wafanyabiashara wapya na wanaoendelea na biashara yanaendelea kupokelewa.
Waombaji wote wametakiwa kufuata masharti ya uombaji wa leseni hizo ikiwemo kuwasilisha nakala za hati za usajili wa magari zilizothibitishwa kisheria kwa Wakala wa kusafirisha watalii (wapya na wanaoendelea na biashara) na kivuli cha leseni ya mwaka 2017 kwa wafanyabiasbara wote.
"Ni kosa kisheria kuwasilisha taarifa za uongo na adhabu yake ni pamoja na kufutiwa leseni", imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Desemba 10 na 11 mwaka 2017, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla alikutana na wadau wa sekta ya utalii jijini Arusha kwa lengo la kuwashirikisha katika mapendekezo ya viwango vipya vya ada kwa Wakala wa kusafirisha watalii ambavyo vilivyotolewa na Wizara yake. Mapendekezo ya viwango hivyo yalilenga kuongeza mapato na kuwawezesha wafanyabiashara wadogo wenye gari kuanzia moja kuingia katika biashara hiyo.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment