Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.

Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.





Nafasi Ya Matangazo

Monday, 8 January 2018

MKAKATI WA CHUO CHA KODI UMEKUJA KATIKA WAKATI MWAFAKA.

TANZANIA kama ilivyo kwa nchi nyingine za Bara la Afrika inaendelea na juhudi za kukuza mapato ya ndani hatua inayolenga kupunguza utegemezi na kuongeza uwezo wa Serikali katika kutoa huduma za jamii na kiuchumi kwa wananchi wake. Anaandika Ismail Ngayonga wa MAELEZO

Dhamira ya utekelezaji wa Sera ya Uchumi wa Viwanda ambayo ni azma kuu ya Serikali ya Awamu ya Tano, ni agenda inayopaswa kuungwa mkono na wadau mbalimbali wa maendeleo zikiwemo Taasisi za Elimu ya Juu kwa kuzalisha wataalamu wa kada mbalimbali ikiwemo masuala ya kodi.

Ni dhahiri kuwa Maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Serikali yoyote duniani yanatokana na wananchi wake kulipa kodi kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato vitokanavyo na sekta mbalimbali ikiwemo mafuta na gesi, madini, na tozo mbalimbali ikiwa ni pamoja na makampuni ya kimataifa.

Ili kufikia malengo iliyojiwekea, Mamlaka ya Mapato Tanzania kupitia Chuo cha Kodi (ITA) kinaendesha mafunzo ya taaluma ya forodha na kodi hatua inayolenga kuongeza kuongeza ufanisi katika usimamizi wa kodi, au kwa kuwasaidia walipakodi watimize wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiyari kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu husika.

Chuo cha Usimamizi wa Kodi (ITA) kinachosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni miongoni mwa Taasisi za Elimu ya Juu iliyojidhatiti kwa ajili kutoa mafunzo ya masuala mbalimbali ya kodi kupitia nyanja za ushauri na utafiti kwa kuongeza ufanisi katika usimamizi wa kodi.

Akizungumza katika Mahafali ya 11 ya Chuo hicho yaliyofanyika Novemba mwaka jana, Mkuu wa Chuo cha ITA, Prof. Isaya Jairo anasema Kulingana na takwimu Chuo, tangu kianze kutoa kozi ndefu miaka nane iliyopita kimeweza kudaili wanafunzi zaidi ya 6,000 ambapo baadhi ya wahitimu wamekuwa raia wa nchi za nje ya Tanzania.

Anasema ITA imekuwa ikishirikiana na taasisi mbalimbali hususani zinazojihusisha na masuala ya forodha na kodi ikiwemo Mtandao wa kimataifa wa Vyuo Vikuu vinavyotoa mafunzo ya Forodha (INCU).

“Tunashirikiana pia na Chuo Kikuu cha Muenster cha nchini Ujerumani katika kuendesha Shahada ya Uzamili katika mchepuo wa Kodi na Forodha. Programu hiyo iliyoanza kufundishwa katika mwaka wa masomo 2012/13 imeweza kuvutia wanafunzi wengi wa ndani na nje ya nchi ikiwemo Botswana, Malawi, Kenya, China na Uganda” anasema Prof. Jairo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Dkt. Samwel Werema anasema wanafunzi wanaodahiliwa wamekuwa wanaongezeka mwaka hadi mwaka kutoka 676 mwaka 2015/16 hadi 760 mwaka 2016/17, kutokana na chuo hicho kutambulika zaidi ndani na nje ya nchi na wanafunzi wengi kupenda kudahiliwa na chuo hiki kwa kuzingatia ubora wa mafunzo yanayotolewa na chuo chetu.

Dkt. Werema anasema tangu mwaka 2004, Bodi ya Mamlaka ya Mapato ilipoazimia kukipa Chuo hicho mwelekeo mpya, Baraza la Chuo hicho limekuwa likichukua hatua mbalimbali za maboresho kwa lengo la kukifanya Chuo kiwe kituo cha umahiri.

“Chuo kimekuwa kikitekeleza mipango mikakati kuanzia ule wa kwanza uliotekelezwa katika kipindi cha mwaka 2006/2007 hadi mwaka 2008/2009 hadi wa tatu uliokamilika hivi karibuni na Chuo kimepata mafanikio ya kuridhisha, hususan katika uboreshaji wa miundombinu iliyokuwepo na katika kuongeza ufanisi” alisema Dkt. Werema.

Anaongeza kuwa kutokana na mafanikio hayo, Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki tayari imeanza mchakato wa kukifanya Chuo kuwa Kituo cha Umahiri (Yaani “Centre of Excellence”) kwa mafunzo ya Forodha na Kodi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa Dkt. Werema anasema kupitia mipango mikakati hiyo, ITA kimeweza kutoa mafunzo yaliyokidhi mahitaji katika taasisi mbalimbali za umma ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania, Serikali za Mitaa, Bodi ya Mapato Zanzibar, Bodi ya Rufani za kodi, Baraza la Rufani za Kodi, pamoja na Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Anawataja wadau wengine walionufaika na mafunzo hayo ni pamoja na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, washauri wa kodi, mawakala wa forodha pamoja na Mamlaka za Mapato katika nchi za Afrika ya Mashariki na Kusini mwa Afrika.

“Mafanikio ya yaliyopatikana katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Tatu, yanatarajiwa kuendelezwa katika Mpango Mkakati wa Nne unaoanza mwaka 2017/2018 hadi mwaka 2021/2022, ambao utalenga kuoanisha zaidi mbinu na mikakati ya Chuo na mahitaji ya muda mrefu zaidi ya Mamlaka ambaye ndiye mdau mkuu” anasema Dkt. Werema.

Ni wazi kuwa jitihada zinazofanywa na ITA hazina budi kuungwa mkono na wadau mbalimbali hatua inayolenga katika kuongeza mapato ya Serikali pamoja na kupanua uelewa wa masuala ya kodi miongoni mwa wadau wakiwemo walipakodi wenyewe.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Post a Comment