Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) inapenda kutoa taarifa ya makusanyo ya mapato ya kipindi
cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2017/2018. Katika kipindi cha mwezi Julai
hadi Septemba 2017, TRA imekusanya jumla ya Shilingi Trilioni 3.65.
Makusanyo haya
ni sawa na ukuaji wa asilimia 1.2 ikilinganishwa na makusanyo ya kipindi kama
hicho kwa mwaka wa fedha 2016/17.
Katika kipindi hicho cha miezi mitatu, makusanyo
ya kila mwezi yalikuwa kama ifuatavyo;-
Julai, 2017 Shilingi 1,101,193,417,551.91
Agosti, 2017 Shilingi 1,205,008,256,053.51
Septemba, 2017 Shilingi 1,345, 339,916,757.65
Kwa makusanyo haya, Mamlaka
ya Mapato Tanzania, inapenda kuwashukuru wafanyabiashara na wananchi wote kwa
ujumla kwa kuendelea kulipa kodi na kuiwezesha serikali kutimiza majukumu yake
ya kuwahudumia wananchi.
Aidha, Mamlaka inapenda kuwakumbusha wafanyabiashara wote kutoa
risiti za kielektroniki kwa kila mauzo na kudai risiti kwa kila manunuzi kwani
ni njia pekee ya kupata mauzo sahihi yanayoiwezesha TRA kukokotoa kodi sahihi
na kwa haki.
“Napenda
kuwakumbusha wananchi wote kuhakiki risiti zao ili kuona usahihi wa tarehe na
kiasi walicholipa na bidhaa waliyonunua kabla ya kuondoka na risiti hiyo.
Endapo utaona haina vigezo tafadhali ripoti kwenye ofisi ya TRA iliyokaribu
nawe au piga simu kituo chetu cha huduma kwa wateja kwa namba 0800750075 au
0800780078. anasisitiza Richard Kayombo,
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi
Vile vile, Mamlaka inawakumbusha wamiliki wa majengo nchini
kulipa kodi ya majengo mapema badala ya kusubiri mwishoni mwa mwaka wa fedha
ili kuepuka misongamano na usumbufu usio wa lazima.
Pia, wafanyabiashara wa michezo ya kubahatisha wanapewa
wito wa kulipakodi zao kwa mujibu wa sheria ya michezo ya kubahatisha sura
namba 41.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment