Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)
ofisini kwake kuhusu hali ya ufaulu kwa Mkoa wa Singida. Kushoto kwake ni Afisa
Elimu Mkoa Florian Kimolo.
Mwandishi wa habari
wa Azam Tv Doris Meghji akirekodi maelezo ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema
Nchimbi kuhusu hali ya ufaulu kwa Mkoa wa Singida. Kulia kwa Mkuu wa Mkoa ni
Afisa Elimu Taaluma, Eva Mosha.
*********************
Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi amewahakikishia wazazi, walezi, wanafunzi na wadau
wa elimu Mkoani hapa kuwa Singida haitapata ufaulu mbaya kielimu kama
ilivyokuwa mwaka huu kutokana na mikakati iliyowekwa.
Dkt Nchimbi ametoa
hakikisho hilo mapema jana ofisini kwake alipokutana na waandishi wa habari
mara baada ya kikao cha wadau wa elimu kilichoweka mikakati ya kuinua ufaulu wa
kielimu mkoani hapa.
Dkt Nchimbi amesema baada
ya Mkoa wa Singida kufanya vibaya katika matokeo ya darasa la saba yaliyotoka
hivi karibuni, wadau muhimu walikutana kutafakari changamoto na suluhisho ili
ufaulu uwe mzuri katika mitihani ijayo.
"Mwaka jana
tulikuwa wa 12 kati ya mikoa 26 tukiwa na ufaulu wa asilimia 69 lakini mwaka
huu tumekuwa wa 26 na ufaulu umeshuka hadi asilimia 61, ufaulu huu
haumfurahishi mtu yoyote yule", amesema na kuongeza kuwa,
"Kama Mkoa
tumejua sehemu tulipokosea hivyo tumeweka mikakati, kwanza tutahakikishwa
wanafunzi wa shule zote za Msingi wanapata chakula shuleni, pili walimu wote
watapewa motisha ya viwanja kwa utaratibu ulio rafiki na mishahara yao, tatu
tumeipatia Tume ya Utumishi wa Waalimu (TSC) miezi mitatu iweze kusikiliza kesi
na malalamiko ya waalimu", amefafanua Dkt Nchimbi.
Ameongeza kuwa Mkoa
utaongeza ukaguzi pamoja na kuwakutanisha wathibiti ubora na maafisa elimu ili
waweze kushirikiana vizuri katika kuhakikisha elimu bora inatolewa mashuleni.
Dkt Nchimbi ameeleza
kuwa baadhi ya changamoto ambazo zimeonekana kuwa kikwazo kikubwa katika kuinua
ubora wa elimu ni pamaoja na kutokuwa na usimamizi na ukaguzi wa karibu wa
elimu Singida huku waalimu wakiachiwa jukumu la kusimamia elimu bila kukaguliwa
mara kwa mara.
Ameongeza kuwa
waalimu wamekuwa na malalamiko mbalimbali lakini maafisa utumishi wameshindwa
kuwasaidia hivyo kuwakatisha tamaa huku akiwataka waalimu kufundisha mada zote
na zile wanazopata ugumu kutakuwa na utaratibu wa walimu 'tembezi' kutoka shule
nyingine watakaowasaidia kwa kipindi hiki.
Aidha Dkt Nchimbi
ameishukuru serikali kuleta mkakati wa kuboresha elimu 'EQUIP' utakaodumu kwa muda wa miaka miwili kwakuwa
utasaidia kutatua baadhi ya changamoto za elimu Mkoani hapa.
Naye Afisa Elimu Mkoa
wa Singid Florian Kimolo amesema amesikitishwa na hali ya ufaulu kwa matokeo ya
darasa la saba mwaka huu na kueleza kuwa hali hiyo haipendezi na haikubaliki.
Kimolo amesema idara
yake itaimarisha ufatiliaji pamoja na kufanyia kazi taarifa za ukaguzi kutoka
kwa wadhibiti ubora wa elimu pamoja na kusimamia ufanisi wa wanafunzi katika
kuzijua K. K. K tatu ambazo ni kusoma, kuhesabu na kuandika.
Ameongeza kuwa
jitihada nyingine zitawekwa katika kuwaelimisha wazazi/walezi waweze
kuwasimamia watoto wao katika masomo pamoja na kuwahamasisha kupenda elimu .
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment