Katika kuelekea Kilele
cha Mbio za Uhuru mwaka 2017 na Kumbukumbu ya 18 ya Kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere, Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli leo Oktoba 13,
2017 amefanya ziara ya kutembelea vituo vya kulelea wazee, watoto yatima na
wanaoishi katika mazingira magumu mjini Zanzibar.
Akiwa na Mke wa
Rais wa Zanzibar, Mama Mwanamwema Shein, Mama Janeth Magufuli amekabibidhi zawadi
ya Mchele kilo 7,626, Unga wa Mahindi
kilo 7,626, Sukari kilo 1,068 na Mafuta ya Alizeti lita 576, kwa vituo vya
kulelea watoto yatima vya Mazizini na SOS pamoja na vituo vya kulelea wazee
Welezo na Sebuleni.
Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hizo, Mama Janeth
amesema ameamua kutoa zawadi hizo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Kumbukumbu
ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere, aliyefariki tarehe 14 Oktoba, 1999 ambapo
kesho Oktoba 14, 2017 taifa litaadhimisha miaka 18 tangu kutokea kifo chake.
Ameongeza kuwa
miongoni mwa mambo ambayo Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alikuwa akiyahimiza
wakati wa uongozi na uhai wake ni kutaka wananchi kuchapa kazi kwa bidii na
kujitegemea. Hata hivyo, alitambua kuwa kwenye jamii kuna watu wasiojiweza wenye
uhitaji.
Hivyo, ametoa wito kwa Watanzania, hususan katika kipindi
hiki cha kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, kujitahidi kumuenzi kwa vitendo kwa kutoa
zawadi na misaada mbalimbali kwa watu wenye mahitaji maalum ikiwa ni pamoja na
Wazee wasiojiweza, Watoto wanaoishi katika mazingira Magumu, Walemavu,
Wagonjwa, Yatima na Wajane.
Mama Janeth pia
amewaasa vijana kujiepusha na vitendo viovu ikiwa ni pamoja na kuepuka matumizi
ya dawa za kulevya.
Kwa upande wake,
Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein, amemshukuru Mama Janeth Magufuli
kwa kuwatembelea Wazee na Vijana hao wenye mahitaji maalum na kuiomba jamii
nchini kuunga mkono moyo huo wa kujitolea kwa kuwasaidia watu watu wenye
mahitaji maalum kama alivyofanya Mama Janeth Magufuli.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment