Waziri
wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) akielezea mikakati ya usimamizi wa
miradi ya umeme nchini mbele ya Watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la
Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala
wa Nishati Vijijini (REA), Kampuni ya
Undelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC) Wakandarasi wa Miradi ya Umeme pamoja
na Wasambazaji wa nyaya, tansfoma na nguzo (hawapo pichani) Katikati ni Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo na kulia ni Kaimu Kamishna wa
Nishati na Masuala ya Petroli, Mhandisi
Innocent Luoga
Naibu
Waziri wa Nishati, Subira Mgalo (kushoto) akifafanua jambo katika kikao hicho.
Wengine kutoka kulia ni Kaimu Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli,
Mhandisi Innocent Luoga, Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo na Waziri wa Nishati, Dkt.
Medard Kalemani.
Sehemu
ya washiriki wa kikao hicho wakifuatilia maelekezo yaliyokuwa yanatolewa na
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani. (hayupo pichani). BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.
Na Greyson Mwase
Waziri
wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)
kuhakikisha linashughulikia haraka tatizo la kukatika kwa umeme katika mkoa wa
Mtwara ili wananchi waweze kuendelea na shughuli zao za kiuchumi kama kawaida.
Waziri
Kalemani alitoa agizo hilo jana (tarehe
12 Oktoba, 2017) alipofanya kikao na
Watendaji wa Wizara ya Nishati, Wenyeviti wa Bodi na Watendaji wa Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati
Vijijini (REA) na Kampuni ya Undelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC).
Wengine
waliohudhuria kikao hicho walikuwa ni pamoja na Naibu Waziri, Subira Mgalo, Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo, Kaimu Kamishna wa Nishati na Masuala
ya Petroli, Mhandisi Innocent Luoga, wakandarasi
wa miradi ya usambazaji wa umeme
vijijini inayosimamiwa na TANESCO na REA pamoja na wasambazaji wa nyaya,
nguzo na transfoma nchini.
Lengo
la kikao hicho lilikuwa ni kujitambulisha, kujadili namna ya kutekeleza miradi ya umeme nchini pamoja na changamoto zake.
Alisema
kumekuwepo na tatizo la kutopatikana kwa umeme wa uhakika katika mkoa wa Mtwara
ambapo ndio chanzo cha gesi asilia inayotumika kuzalisha umeme.
Alimtaka
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Dkt. Tito Mwinuka kuhakikisha unapatikana
umeme wa dharura kwa namna yoyote na kuongezwa katika mkoa wa Mtwara hivyo kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme kwa mara kwa
mara.
Alisema
mbali na kuweka umeme wa dharura, shirika hilo linatakiwa kuhakikisha mitambo
iliyoharibika inakarabatiwa mapema ipasavyo na kuendelea na mchakato wa ununuzi
wa mitambo mipya kwa kasi kubwa ili hatimaye tatizo la umeme katika mkoa wa
Mtwara liwe historia.
“Wananchi
wa Mtwara wanateseka sana kutokana na tatizo la kukatika kwa umeme la mara kwa
mara linaloukabili mkoa wao, ni jukumu la TANESCO kuhakikisha wananchi wanapata
umeme wa uhakika, na utekelezaji uanze mara moja,” alisema Dkt. Kalemani.
Katika
hatua nyingine, Waziri Kalemani alisema kuwa Shirika la Tanesco linatarajiwa
kuanzisha vituo vidogo vidogo kwenye kata na tarafa ambavyo vitakuwa kwa ajili ya kuunganishia wakazi umeme.
Alisema
vituo hivyo vitakuwa rasmi kwa ajili ya wateja kuhudumiwa kwa kukutana na
watumishi wa Tanesco moja kwa moja badala ya kukutana na vishoka wanaojifanya
ni watumishi wa Tanesco ambao huwatoza gharama kubwa na kuwalaghai.
Aidha
aliwataka wananchi kufuata taratibu za kuunganishiwa umeme kwa kuwa wameondoa
ada ya maombi hivyo wasiogope kuleta maombi wakidhani kuwa watatozwa bili
yoyote.
Akielezea
mikakati yake tangu kuteuliwa kuwa
Waziri wa Wizara Mpya ya Nishati, Dkt. Kalemani alisema ameweka mikakati
mbalimbali ya kuhakikisha kuwa umeme wa
uhakika unapatikana kwa gharama nafuu nchi nzima.
Alitaja
mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa umeme unaozalishwa unafikia
Megawati 5000 ifikapo mwaka 2020 ikiwemo ujenzi
wa njia za kusafirisha umeme za kilovolti 400 kwenye kanda zote nchini.
Wakati
huohuo, Waziri Kalemani aliwataka wakandarasi waliokabidhiwa miradi ya REA Awamu
ya Tatu kuanza kazi mara moja na kuhakikisha kuwa miradi inakamilika kwa wakati.
Naye
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalo alitoa pongezi wa serikali kujali watoa
huduma wa ndani wa usambazaji wa vifaa vya umeme kama vile nguzo, nyaya na
transfoma na kuwaomba kujikita kwenye uzalishaji wa bidhaa hizo hapa nchini na kuimarisha sekta ya viwanda
nchini.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano inaunga mkono
uwekezaji wa viwanda ili kuhakikisha kuwa sekta ya viwanda inakuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi
wa nchi na kuwa miongoni mwa nchi zenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment