WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepiga marufuku viongozi wa Serikali
kufanya biashara ya pembejeo na vishada kama hawana mashamba ya tumbaku.
“Kuna baadhi ya viongozi wa Serikali hapa mkoani wamejiingiza kwenye
biashara ya vishada na uuzaji wa pembejeo. Hii ni dosari. Hatutaruhusu hili
hata kidogo,” alisema.
Waziri Mkuu alitoa onyo hilo jana jioni (Jumatano, Agosti 9, 2017) wakati
akizungumza na wadau wa zao la tumbaku zaidi ya 600 wakiwemo wabunge, viongozi
wa dini, chama na Serikali kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa
Isike-Mwanakiyungi, mjini Tabora.
Alisema: “Kiongozi wa Serikali ni lazima uwe shamba na ulilime kisasa
ili liwe ni shamba darasa kwa wakulima walio jirani nawe. Usifanye biashara ya
pembejeo kana huna shamba. Nanyi viongozi wa AMCOS msikubali kuuza vishada vya
viongozi wa Serikali, tukikukamata, utaenda jela.”
Alisema endapo viongozi wataamua kulima mashamba ya zao hilo,
watalazimika kujiunga na vyama vya msingi (AMCOS) vya kwenye maeneo yao ili
waweze kuuza kupitia huko kutokana na agizo la Serikali linalokataza makampuni
kununua tumbaku bila kupitia kwenye vyama vya msingi.
Aprili 15, mwaka huu, akiwa katika ziara ya siku moja mkoani Tabora,
Waziri Mkuu aliagiza wakulima wa kujitegemea (Indepenent Farmers) na wale wa
kwenye vikundi (Associations) wote wauzie tumbaku yao kupitia kwenye vyama vya
ushirika ili kuzuia utoroshaji wa zao hilo na wakulima wasio na madeni
kulazimika kuwalipia wenzao.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment