Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Januari Makamba (MB) akizungumza na waandishi
wa habari (hawapo pichani) alipokuwa akitoa uamuzi wa kutengua uteuzi wa
wajumbe saba wa Bodi ya Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) na uteuzi wa
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Mkuu wa
Ofisi ya Makamu wa Rais Profesa Faustine Kamuzola.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Januari Makamba (MB) akifafanua jambo
mbele yanwaandishi wa habari (hawapo pichani) akitangaza uamuzi wa kutengua
uteuzi wa wajumbe saba wa Bodi ya Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) pamoja na
uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa NEMC ofisini kwake leo Jijini Dar es Salaam.
Kushoto ni Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais Profesa Faustine Kamuzola na
kulia ni Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Richard
Muyungi.
Baadhi
ya waandishi wa habari wakiwa kazini wakati wa mkutano wao na Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamu wa Rais, Januari Makamba (MB) alipokuwa akitangaza uamuzi wa kusitisha
uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) na wajumbe
saba wa Bodi ya baraza hilo leo Jijini Dar es Salaam.
******************
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais
Muungano na Mazingira Mhe. Januari Makamba (Mb) ametengua uteuzi wa Mkurugenzi
Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi ya Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Wajumbe
wa Bodi ya Wakurugenzi ili kuongeza tija na kutekeleza kwa vitendo dhana ya
Ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Kwa
kuzingatia mamlaka aliyonayo Waziri
chini ya Sheria ya Mazingira kifungu cha 19 (2) anaweza kutengua uteuzi wa
Mkurugenzi wa Baraza hilo na wajumbe wake.
Akizungumza na vyombo vya Habari leo
Jijini Dar es Salaam Waziri Makamba amesema kuwa lengo la mabadiliko hayo ni
kuhakikisha kuwa kunakuwa na usimamizi na uzingatiaji wa Sheria ya
Mazingira na uharakishaji wa miradi ya
maendeleo na uwekezaji hasa ujenzi wa viwanda kama azma ya Mheshimiwa Rais John
Magufuli inavyoelekeza.
Kufuatia mabadiliko hayo Waziri Makamba
amemteua Dkt. Elikana Kalumanga ambaye ni Mhadhiri katika Taasisi ya Usimamizi
na Tathmini ya Rasilimali Asili,Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuwa Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC hadi Rais atakapoteua Mkurugenzi Mkuu.
“Utendaji wa NEMC umekuwa ukilegalega
sana na umekuwa hauridhishi na kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa
wawekezaji wa ndani na nje ya nchi
kuhusu ucheleweshaji na urasimu usiokuwa wa lazima katika mchakato wa tathmini
ya athari kwa mazingira (EIA)” Alisisitiza Mhe. Makamba
Aliongeza kuwa ametengua uteuzi wa
wajumbe wote saba wa Bodi ya NEMC ili baadaye ateue wajumbe wapya ambao
wataendana na kasi na ari ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kuelekea uchumi
wa Viwanda, ambapo Mwenyekiti wa Bodi ambaye mamlaka yake ya uteuzi ni
Mheshimiwa Rais,ataendelea kuwepo hadi Mheshimiwa Rais atakapoteua mwingine.
Akifafanua Makamba amesema kuwa
changamoto nyingine zilizobainika ni kuwaelekeza wawekezaji kwa makampuni ya
kufanya Tathmini ya athari za mazingira ambayo yanamilikiwa au yenye ubia na
watumishi wa NEMC, bila kujali mgongano wa kimaslahi jambo ambalo haliruhusiwi
katika utumishi wa umma.
Jambo jingine ni kuwarundikia maandiko ya
miradi ya tathmini ya athari kwa mazingira (EIA) watumishi wachache wakati
wengine hawana kazi ili waelekeze miradi hiyo katika makampuni ambayo baadaye
huwapatia malipo yasiyo halali.
Hatua nyingine zilizochukuliwa na Waziri
Makamba ni pamoja na kuiagiza NEMC kufuta watu binfsi na Makampuni yote ya
ushauri wa EIA (Consultants) ambayo hayana sifa au yameshindwa kutekeleza kazi
zao vizuri na watangaze kwenye magazeti orodha ya watu na makampuni yanayoruhusiwa
kufanya kazi kama washauri elekezi.
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi
wa Mazingira NEMC ni muhimu katika kuhakikisha ustawi wa mazingira na
mustakabili wa maendeleo endelevu ya nchi tunapoelekea kuwa Taifa la uchumi wa
viwanda lazima usimamizi wa mazingira uwe thabiti.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment