Mkuu wa Oparesheni Maalumu za Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa
Polisi Liberatus Sabas akionesha moja ya silaha zilizopatikana katika mapambano hayo.
**************
Jeshi la
Polisi nchini limefanikiwa kuwaua watu wanne wanaosadikiwa kuwa miongoni
mwa wahalifu wanaoendesha mauaji katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na
Rufiji katika mapambano yaliyodumu kwa
zaidi ya nusu saa katika kijiji cha Pagae wilayani Kibiti mkoani Pwani. Anaandika Frank Geofray-Jeshi la Polisi.
Akielezea
tukio hilo Mkuu wa Oparesheni Maalumu za Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa
Polisi Liberatus Sabas alisema tukio hilo lilitokea siku ya Alhamisi juni 29
majira ya saa tatu usiku kwenye barabara ya vumbi itokayo Pagae kuelekea
Nyambunda ambapo Askari Polisi wakiwa doria walikutana na kikundi cha watu
kinachokadiriwa kuwa na watu sita ambapo wahalifu hao baada ya kuona gari la
Polisi walikimbilia vichakani na kuanza kuwarushia risasi Polisi.
Sabas
alisema baada ya hali hiyo kutokea Askari nao kwa ujasiri walijibu na mapambano hayo yalidumu kwa zaidi ya nusu
saa ambapo Polisi walifanikiwa kuwajeruhi wahalifu wanne kwa risasi ambao
baadaye walifariki dunia wakiwa wanapelekwa hospitali.
“Katika
tukio hilo tumefanikiwa kupata silaha mbili aina ya SMG na magazine mbili
pamoja na risasi 17 zilizokuwa zinatumiwa na wahalifu hao na hii ni dalili kuwa
tunaendelea vizuri na oparesheni yetu ambayo inashirikisha vyombo vingine vya
ulinzi na Usalama katika wilaya hizi tatu za Mkuranga, Kibiti, na Rufiji” Alisema
Sabas.
Aidha Sabas
ametoa wito kwa wahalifu wengine kuacha mara moja kufanya vitendo hivyo kwa
kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kufanya jitihada zote za
kuhakikisha kuwa maeneo hayo yanakuwa salama na wananchi wanaishi katika hali
ya amani na usalama.
Vilevile
amewataka wananchi kutoa taarifa zitakazowezesha kupatikana wahalifu wengine
ili kuhakikisha kuwa kila mmoja anaishi kwa usalama ambapo kwa ambaye
atakayetoa taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa wahalifu hao kiasi cha
shilingi milioni kumi kitatolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon
Sirro.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment