Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya
Makazi imesema kuwa Shirika la Nyumba
nchini(NHC) limeweka mkakati wa
kuhakikisha nyumba zote zilizo katika hali ya uchakavu zinafanyiwa ukarabati
mkubwa na zile ambazo kiwango cha uchakavu ni kikubwa zinavunjwa na kuendeleza
upya viwanja hivyo.
Naibu Waziri wa Ardhi,Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula
amesema Bungeni mjini Dodoma leo
kuwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeshafanya uhakiki wa nyumba zake zote
na kubaini hali halisi ya kila nyumba na kuweka mpango wa kuzifanyia ukarabati
nyumba hizo kwa awamu.
Amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha
2016/17 shirika lilitenga takribani shilingi bilioni 11 kwa ajili ya kuzifanyia
ukarabati nyumba zake ambapo hadi mwezi Machi, 2017 jumla ya nyumba 2451
zilikuwa zimekwishafanyiwa ukarabati kupitia bajeti hiyo.
Aidha amesema kuwa shirika hilo linatarajia
kumaliza ukarabati wa nyumba zote katika mwaka wa fedha 2017/18 na kusisitiza
kuwa matengenezo ya nyumba hizi ni kazi endelevu kwa shirika hivyo bajeti ya
matengenezo itaendelea kutengwa kila mwaka ili wapangaji wa nyumba za shirika
waendelee kuishi katika nyumba na mazingira bora.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment