Rais Dkt. John Pombe Magufuli amelifuta
agizo lililotolewa jana Machi 16, 2017 na Waziri wa Katiba na Sheria
Dkt. Harrison Mwakyembe linalotoa sharti la kuwa na cheti cha kuzaliwa kwa watu
wote watakaofunga ndoa kuanzia tarehe Mei 01, 2017.
Rais Magufuli amefuta agizo hilo leo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari
muda mfupi kabla ya kuondoka katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma na kurejea
Jijini Dar es Salaam.
Dkt. Magufuli amesema Serikali haiwezi kuruhusu sharti hilo kutumika kwa kuwa
litawanyima haki ya kuoa na kuolewa Watanzania wengi ambao hawana vyeti vya
kuzaliwa, huku utaratibu wa kupata vyeti hivyo ukiwa bado unakabiliwa na changamoto
nyingi kwa wanaohitaji.
Amesema
mpaka sasa idadi ya Watanzania walio na vyeti vya kuzaliwa ni chini ya asilimia
20 huku wengi wao wakiwa ni wananchi waishio vijijini ambako ni vigumu kupata
vyeti hivyo, na wengine wakiwa ni waliozaliwa kabla ya kuanza kutolewa kwa
vyeti vya kuzaliwa nchini mwaka 1961.
“Kwa
hiyo ndugu zangu Watanzaniamsiwe na wasiwasi wowote, endeleeni na utaratibu
wenu wa kuoa na kuolewa kama kawaida na kama kuna kifungu chochote cha sheria
kinachomlazimisha mtu awe na cheti cha kuzaliwa ndipo aoe ama aolewe
nitamuelekeza Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Harrison Mwakyembe
apeleke Bungeni kikarekebishwe” amesema Rais
Magufuli.
Rais Magufuli ametoa wito kwa wanasheria kuziangalia vizuri sheria
zinazohusiana na kuzaliwa na kifo na kuoa na kuolewa ili zisilete mkanganyiko
kwa wananchi.
Hata
hivyo Rais Magufuli ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kupata vyeti vyao
vya kuzaliwa kama kawaida na amewataka viongozi wote kuwahamasisha wananchi
kuwa na vyeti hivyo.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment