Makamu wa
Rais Samia Suluhu Hassan amelaani na
kukemea vikali vitendo vya ukeketaji wa wanawake na ubakaji vinavyoendelea
katika jamii na amewataka wananchi kote nchini kushirikiana katika kukabiliana
na vitendo hivyo nchini.
Makamu wa
Rais, Samia Suluhu Hassan ametoa kauli
hiyo tarehe 8-March-2017 wakati
akizungumza katika mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji wa Tanzania (TBC) mjini Dodoma kuhusu maadhimisho
ya siku ya wanawake Duniani.
Makamu wa
Rais, Samia Suluhu Hassan amesema vitendo hivyo vya ukeketaji wa wanawake na
ubakaji vinamchukiza sana hivyo ametoa wito maalum kwa wananchi na wadau wote
bila kujadili dini, kabila wala rangi kupambana ipasavyo na vitendo hivyo
ambavyo vinarudisha nyuma jitihada za kumkwamua mwanamke kiuchumi.
Kuhusu maadhimisho ya Siku ya Wanawake
Duniani, Makamu wa
Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema anafurahishwa na hatua na jitihada
zinazochukuliwa na wanawake kote nchini katika kujikwamua kiuchumi kwa
kuimarisha shughuli zao za ujasiriamali katika kuelekea katika uchumi wa
viwanda.
Amesema
jukumu kubwa la serikali ya awamu ya Tano ni kuhakikisha wanawake wanaboreshewa
ipasavyo mazingira ya kufanyia kazi hasa shughuli za ujasiriamali ili waweze
kufikia malengo waliyojiwekea.
“Inapofika
katika shida zetu wanawake ni lazima tuwe na kitu Kimoja na sauti Moja katika
kulinda na kutetea haki zetu bila kujali itikadi za kisiasa”Amesisitiza Makamu wa Rais.
Katika
uundaji wa majukwaa ya kuwawezesha wanawake kiuchumi nchini, Makamu wa Rais,
Samia Suluhu Hassan amesema kazi hiyo inaendelea vizuri na kutaka mikoa na
wilaya ambazo bado haijaunda majukwaa hayo kufanya hivyo haraka iwezekanavyo.
Ameeleza
kuwa lengo la uundaji wa majukwaa hayo katika ngazi ya wilaya na mikoa nchini
ni kuwakutanisha wanawake pamoja katika kujadili na kutafutia ufumbuzi
changamoto zinazowakabili ikiwemo tatizo la masoko za bidhaa wanazozizalisha.
Makamu wa
Rais, Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa majukwaa hayo ambayo yameanza
kuundwa katika mikoa mbalimbali nchini yatakuwa sio ya kisiasa.
Katika Mahojiano
hayo na mtangazaji Shaban Kissu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) mjini DODOMA, Makamu wa Rais Mhe
Samia Suluhu ametumia sehemu ya mahojiano hayo kwa kuwatakia heri na mafanikio
wanawake wote nchini katika kuadhimisha Siku ya wanawake Duniani.
Kauli mbiu
ya mwaka huu ya siku ya wanawake Duniani ni “Tanzania ya Viwanda,Wanawake ni msingi wa mabadiliko ya Kiuchumi”.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment