Naibu Waziri wa
Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wachimbaji wadogo kwenye
machimbo ya dhahabu ya Musasa yaliyopo kwenye Kata ya Makurugusi, Wilayani
Chato. Nyuma yake ni baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini.
Baadhi ya wachimbaji
wadogo wa madini kwenye machimbo ya dhahabu ya Musasa katika Kata ya
Makurugusi, Wilaya ya Chato wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati na Madini,
Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani).
Muonekano wa baadhi
ya maeneo ya machimbo ya dhahabu ya Musasa katika Kata ya Makurugusi, Wilaya ya
Chato.
Wachimbaji wadogo wa
madini nchini wametakiwa kufanya shughuli za uchimbaji kwa kuzingatia sheria na
kanuni za usalama migodini ili kuepusha ajali.
Wito huo umetolewa hivi
karibuni na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani alipokuwa
akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu kwenye mgodi wa Musasa
uliopo Kata ya Makurugusi, wilayani Chato.
Dkt. Kalemani alisema
njia bora ya kuepukana na ajali migodini ni kufanya shughuli za uchimbaji kwa
kutii sheria za uchimbaji madini bila shuruti na kuzingatia kanuni za usalama
kwenye maeneo ya machimbo na wakati wa shughuli za uchimbaji.
Aliwaasa wachimbaji
wadogo wa madini kote nchini kujifunza kutokana na ajali mbalimbali zilizotokea
migodini ili kuepuka sababu zilizopelekea kutokea kwa ajali hizo kutojirudia tena
kwenye maeneo mengine.
Aidha, Dkt. Kalemani
aliwasisitiza wachimbaji wa madini kote nchini kuhakikisha wanafanya shughuli
za uchimbaji kwa kutunza mazingira na afya zao pamoja na afya za wengine
wanaozunguka machimbo husika.
Alisema suala la
mazingira linapaswa kupewa kipaumbele wakati wa shughuli husika, na kwamba ni
jukumu la kila mchimbaji na kila anayeishi ama kufanyia shughuli zake maeneo ya
machimbo kuhakikisha anaboresha mazingira ili kuepusha majanga mbalimbali
ikiwemo ya magonjwa ya mlipuko.
“Chimbeni madini kwa
kutunza mazingira na afya zenu ili mpate kufaidi matunda yatokanayo na shughuli
hii, alisema Dkt. Kalemani.
Kwa wakati huohuo,
Naibu waziri huyo aliwakumbusha wachimbaji wadogo wa madini kulipa kodi na
ushuru stahiki ili kuepuka usumbufu.
Aliwahakikishia
wachimbaji wadogo wa madini kufanya shughuli zao bila kubughudhiwa endapo
watafuata maelekezo ya sheria.
“Mkitaka kuishi
salama na kufanya shughuli zenu bila kubughudhiwa, hakikisheni mnalipa kodi na
tozo mbalimbali mnazopaswa kulipa,” alisema.
Dkt. Kalemani
alizipongeza kampuni za watanzania zinazomiliki leseni kwenye machimbo hayo ya
Musasa ambazo ni Godfrey and Partners, Kilimo Kwanza Group na Hapa Kazi Tu Group
kwa kuonesha njia na kutunza usalama kwenye machimbo hayo na hivyo kuwataka
wachimbaji wengine kuiga mfano huo.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment