Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.

Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.





Nafasi Ya Matangazo

Friday 18 May 2018

WAZIRI MPINA AJA NA MAGEUZI MAKUBWA SEKTA YA MIFUGO NA UVUVI


WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina,akiwasilisha mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2018/2019 bungeni jijini Dodoma jana.
Na John Mapepele, DODOMA
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amesema kuwa Wizara inafanya mageuzi makubwa kwenye sekta ya Uvuvi, kwa kuanzisha Mamlaka ya kusimamia rasilimali za uvuvi ili kuleta suluhisho la kudumu katika kunusuru rasilimali hizo ambazo kwa sasa zinavunwa kiholela,kutoroshwa nje ya nchi na Serikali kukosa mapato.

Akiwasilisha mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2018/2019 bungeni jijini Dodoma jana, Mpina alisema Serikali pia itahakikisha inafufua Shirika la Taifa la Uvuvi,TAFICO na kufufua vituo vyote vya kuzalisha vifaranga vya samaki ili wananchi wengi zaidi waweze kupata mbegu bora ya samaki na kufuga kibiashara sambamba na kuanzishwa kwa bandari ya Uvuvi.

Mpina alisema Wizara itafufua viwanda vyote vya nyama ili mifugo yote nchini iweze kuuzwa na kuchinjwa kwenye viwanda hivyo na kuliingizia taifa mapato. Alivitaja baadhi ya viwanda vitakavyofufuliwa kuwa ni kiwanda cha nyama cha Shinyanga, Mbeya, Utegi na Mwanza.

Pia alisema wizara imejipanga kulisuka upya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ili liweze kuzalisha kibiashara zaidi tofauti na hali ilivyo sasa ambapo alisema Wizara imeandaa mkakati mpya wa kuvunja mikataba yote isiyo na tija na kuwaondoa wawekezaji ambao wameshindwa kukidhi matakwa ya uwekezaji.BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.

Pia kuweka ulinzi ulinzi imara na kuziba mianya yote ya upotevu wa mapato ambayo itawezesha kuongezeka kwa mapato zaidi ya mara 10 ya ilivyo sasa ambapo Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) na Mamlaka za Serikali za Mitaa zitaendelea kufanya operesheni hadi kuutokomeza uvuvi na biashara haramu.

Akiwasilisha mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2018/2019 bungeni jijini Dodoma jana Waziri Mpina alisema Serikali pia itaendelea uendelea kuzielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza majukumu yao ya kusimamia, kutunza na kuendeleza rasilimali za uvuvi katika maeneo yao na kuweka miundombinu kwa ajili ya shughuli za uvuvi.

Pia kuandaa utaratibu wa kuwezesha Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Idara ya Uvuvi) kusimamia Mialo na Masoko ya Kimataifa ya Samaki badala ya Halmashauri kama ilivyo hivi sasa kuendelea kuwachukulia hatua Watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wanaojishughulisha na uvuvi na biashara haramu kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za Utumishi wa Umma

Pia kushauri Mamlaka husika kuwachukulia hatua viongozi wa kisiasa na watendaji wa Serikali wanaoshiriki na kufadhili uvuvi haramu na kuishauri TRA ifanye makadirio ya kodi kwa wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi waliokwepa kulipa mapato ya Serikali mwaka 2016/2017 ambapo inakadiriwa kuwa mapato ya kiasi cha shilingi bilioni 581.5 hayakufanyiwa makadirio na TRA na hivyo kuikosesha mapato Serikali.

Pia katika mwaka 2018/2019, Wizara kwa kushirikiana na wadau itaendelea kusimamia na kuimarisha usimamizi na ulinzi wa rasilimali za uvuvi kwa kufanya doria za kawaida zenye siku kazi 6,000. Aidha, itawezesha MATT kutekeleza kazi zake kwa kufanya operesheni 12 katika maji bahari na kupanua majukumu ya MATT hadi maji baridi. Vilevile, Wizara itaendelea kutoa elimu na mafunzo kwa wavuvi na wadau wengine kuhusu madhara ya uvuvi haramu na faida za uvuvi endelevu.

Alisema katika mwaka 2017/2018, Wizara kupitia Fungu 64 ilipangiwa kukusanya kiasi cha shilingi19,700,628,051.00 ambapo hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2018 kiasi cha shilingi 21,280,222,364.48 kimekusanywa na Wizara ikiwa ni sawa na 108.02% ikilinganishwa na shilingi 16,019,668,687.00 zilizokusanywa kuanzia mwezi Julai 2016 hadi tarehe 30 Aprili 2017. Katika mwaka 2018/2019, Wizara kupitia Fungu 64 inatarajia kukusanya jumla ya shilingi 21,534,305,600.00.

Pia katika mwaka 2018/2019, Wizara kupitia Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu itakamilisha Sera ya Uvuvi wa Bahari Kuu. Pia, itaendelea kutekeleza Mkakati wa Kuboresha Sekta ya Uvuvi na Programu ya KuendelezaSekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II).

Vilevile, wizara itafanya mapitio ya Mpango Kabambe wa Uvuvi Tanzania (Tanzania Fisheries Master Plan) wa mwaka 2015 na kuendelea na taratibu za kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) ambapo shilingi bilioni 45 zinahitajika kwa ajili ya kuanzisha upya Shirika hili. Kuwepo kwa shirika hili kutawezesha nchi yetu kuwa na meli za kitaifa (National Fleet) kwa ajili ya uvuvi wa Bahari Kuu ili kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi katika pato la Taifa.

Pia, Wizara itakamilisha mapitio ya Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003; Sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Na. 29 ya mwaka 1994 ili kupanua maeneo ya hifadhi kwenye maji baridi na Sheria ya Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi Bahari Kuu Na. 1 ya mwaka 1998 na marekebisho yake ya mwaka 2007 na kuandaa kanuni mpya za kutekeleza Sheria mpya ya Uvuvi.

Alisema katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Aprili, 2018 uzalishaji wa maziwa umefikia lita bilioni 2.4 ukilinganishwa na lita bilioni 2.1 zilizozalishwa katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Aprili, 2017. Aidha, katika kipindi hiki usindikaji wa maziwa umeongezeka na kufikia lita milioni 56.2 ikilinganishwa na maziwa lita milioni 40.1 zilizoshindikwakatika kipindi cha Julai, 2016 hadi Aprili, 2018.

Pia, katika kipindi hiki, jumla ya mitamba 590 ilizalishwa kutoka katika mashamba ya Serikali na ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO). Vilevile, Sekta Binafsi ilizalisha na kuuza kwa wafugaji wadogo nchini jumla ya mitamba 13,145.

Aidha katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Aprili, 2018, uzalishaji wa zao la nyama umeongezeka kufikia tani 679,992 ikilinganishwa tani 558,164 zilizozalishwa katika kipindi Julai, 2017 hadi Aprili, 2018. Aidha, katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Aprili, 2018, jumla ya tani 2,608.93 za nyama ziliuzwa nje ya nchi na jumla ya tani 1,224.55 za nyama ziliingizwa nchini. Pia, uzalishaji wa mayai uliongezeka nchini kutoka mayai bilioni 2.76 mwaka 2016/2017 hadi bilioni 3.16 mwaka 2017/2018.

Pia ulaji wa nyama kwa mwaka 2017/2018 ni wastani wa kilo 15, lita 47 za maziwa na mayai 106 kwa mtu kwa mwaka ikilinganishwa na viwango vya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO, 2011) ambavyo ni kilo 50 za nyama, lita 200 za maziwa na mayai 300 kwa mtu kwa mwaka.

Alisema katika mwaka 2017/2018, Wizara kupitia Fungu 99 (Maendeleo ya Mifugo) ilipangiwa kukusanya shilingi16,404,739,500.00. Hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2018 kiasi cha shilingi 13,677,333,381.24 kimekusanywa, sawa na83.4%, ikilinganishwa na shilingi 10,952,827,50 zilizokusanywa mwaka 2016/2017 kuanzia mwezi Julai, 2016 hadi tarehe 30 Aprili, 2017. Katika mwaka 2018/2019, Wizara kupitia Fungu 99 inatarajia kukusanya jumla ya shilingi18,467,945,100.00.

Hivyo katika mwaka 2018/2019, Wizara itaimarisha mashamba matano (5) ya kuzalisha mitamba ya Sao Hill, Kitulo, Ngerengere, Nangaramo na Mabuki kwa kununua mitamba aina ya boran 1,000 na madume bora aina ya Friesian 200 na boran ili kuongeza idadi ya ng’ombe wazazi na kuboresha malisho na miundombinu ya maji. Aidha, Wizara itaendelea kuhamasisha sekta binafsi kuongeza uzalishaji wa mitamba na kusambaza kwa wafugaji. Pia, Wizara imeanzisha Programu ya uzalishaji wa mitamba 1,000,000 kwa mwaka kutokana na makundi ya ng’ombe wa asili kwakufanya uhimilishaji katika ng’ombe milioni 3.0 kwa ajili ya kuongeza uzalishaji maziwa ili kukidhi mahitaji.

Waziri Mpina alisema katika mwaka 2018/2019, Wizara itaendelea kuimarisha Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji cha NAIC Usa River, Arusha kwa kununua vitendea kazi na kukarabati mabanda ya madume na kuendeleza malisho.

Pia, Wizara itajenga kituo cha NAIC Sao Hill Iringa, itanunua trekta na vifaa vyake na kutoa mafunzo kwa wahimilishaji 200 kutoka mikoa 10 ya Lindi, Mtwara, Dodoma, Singida, Simiyu, Shinyanga, Tabora, Kigoma, Katavi na Geita. Aidha, itaimarisha vituo sita (6) vya Kanda vya uhimilishaji vya Dodoma, Kibaha, Lindi, Mbeya, Mpanda na Mwanza kwa kufanya matengenezo ya mitambo ya kuzalisha kimiminika baridi cha Naitrojeni, pamoja na vituo vidogo vya uhimilishaji vya Tanga na Tabora.

Hata hivyo katika mwaka wa fedha 2018/2019, Heifer International kupitia mradi wa EADD II inatarajia kupanuawigo wa mradi huu ili kufikia maeneo mengi. Pia, itaendelea kushirikiana na Serikali, wafugaji na wadau wengine katika kuanzisha vituo vya kisasa vya kukusanya maziwa ili wafugaji wengi zaidi waweze kuvifikia kwa karibu zaidi. Pia, mradi utaendelea na programu ya unywaji wa maziwa shuleni kwa kuwafikia wanafunzi wengi zaidi katika maeneo ya mradi.

Pia katika mwaka 2018/2019, Wizara kupitia Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) itaendelea kutekelezaMradi wa Kuboresha Mbari za Kuku wa Asili Afrika kwa ufadhili Taasisi ya Bill & Mellinda Gates Foundation ambao unatekelezwa kwa pamoja na nchi tatu za Ethiopia, Tanzania na Nigeria kwa miaka mitano (5) kuanzia mwaka 2015 hadi 2019. Lengo kuu la mradi ni kuongeza tija katika uzalishaji wa kuku wa asili kwa ushirikishwaji wa sekta ya umma na sekta binafsi, hivyo kuongeza upatikanaji wa kuku bora na kuongeza tija; kipato na uhakika wa lishe.

Kuhusu ‘Operesheni Nzagamba’ Waziri Mpina alisema hadi kufikia t Mei, 8 mwaka huu jumla ya shilingi 1,992,804,200 zimekusanywa kama ushuru, tozo na faini mbalimbali katika operesheni hiyo.

Aidha katika mwaka 2018/2019, Wizara itaendelea kuimarisha mikakati ya kulinda rasilimali za mifugo na mazao yake kwa kuboresha vituo 36 vya ukaguzi vya mipakani. Pia, Wizara itashirikiana na TRA, TFDA na taasisi nyingine zaSerikali kudhibiti uingizaji na utoaji holela wa mifugo na mazao yake kwa lengo la kuhakikisha kuwa biashara ya mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi inafanyika kwa mujibu wa sheria na kanuni.

“Wizara yangu imeandaa pendekezo la kuibadilisha NARCO kutoka Kampuni kuwa Shirika la Umma (Public Corporation) ili kuondoa utata uliopo na kupanua wigo wa kutekeleza majukumu yake. Faida za kubadilisha NARCO kuwa Shirika la Umma ni pamoja na kuondoa mkanganyiko wa kisheria uliokuwepo katika muundo na uendeshaji wa Kampuni na kuwa na shirika lenye uwezo, mamlaka na uwanda mpana zaidi wa kuleta tija kwenye sekta ya mifugo hapa nchini na kuwa na dira, malengo na majukumu yanayotekelezeka na kupimika”alisema.

Hivyo NARCO kwa kushirikiana na Msajili wa Hazina na Mwanasheria Mkuu wa Serikali itahakikisha Vitalu 23 vya wawekezaji ambao wameshindwa kuwekeza zaidi ya 50% mikataba yao itavunjwa kabla ya Juni 2018; Pia Vitalu 24 vya wawekezaji ambao wameshindwa kulipa pango la ukodishaji ranchi mikataba yao itavunjwa kabla ya Juni 2018; na wawekezaji waliokidhi masharti na matakwa ambao wamewekeza zaidi ya 50% na kulipa ada za pango mikataba yao itahuishwa mwezi Juni, 2018.

Kuhusu Mkataba kati ya Serikali na Viwanda vya Sukari vya Kagera na Mtibwa, Waziri Mpina alisema timu iliyoundwa ilibaini mambo muhimu ambayo ni pamoja na Makampuni haya kumilikishwa ardhi yenye ukubwa wa hekta 75,000 (sawa na ekari 187,500) bure bila kulipia fidia ya ardhi kwa NARCO.

Pia, hakuna uwekezaji wowote wa mifugo, majengo na miundombinu uliofanyika katika shamba la Dakawa ambapo Kampuni ya Sukari ya Mtibwa ilimilikishwa jumla ya hekta 20,000 kwa ajili ya ufugaji wa kisasa kwa muda wa zaidi ya miaka 15 na kwa upande wa Kitengule na Missenyi kampuni imewekeza ng’ombe 5,307, mbuzi 125 na kondoo 31 ingawa hakuna uwekezaji wowote wa majengo wala miundombinu kinyume na makubaliano ya mkataba.

Hivyo kufuatia changamoto hizo, Wizara yake inaandaa madai kwa makampuni hayo ili yaweze kulipa NARCO fedha yote wanayodaiwa (mapunjo) na pia nimeagiza makampuni hayo kuwasilisha mpango kazi wa uwekezaji wa miaka mitatu katika maeneo hayo.

Aidha katika mwaka 2018/2019, Wizara kupitia Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) itaendelea kufanya uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya wanyama; kufanya uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo na malighafi za kutengenezea vyakula hivyo, na kuzalisha na kusambaza dozi milioni 100 za chanjo ya Mdondo, dozi1,000,000 za chanjo ya Kimeta, dozi 1,000,000 za chanjo ya Chambavu na dozi 500,000 za chanjo ya ugonjwa wa Kutupa Mimba.

Aidha, TVLA itakamilisha majaribio na kuanza kuzalisha chanjo dhidi ya ugonjwa wa Homa ya Mapafu ya Ng’ombe na kuanza majaribio ya kuzalisha chanjo dhidi ya ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na Kondoo na chanjo dhidi ya Kichaa cha Mbwa

Hivyo katika mwaka wa fedha 2018/2019, Wizara yake imeliomba Bunge Bunge likubali kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya jumla ya shilingi 56,455,749,000.00.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Post a Comment