Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama picha za nyumba wakati
alipotembelea Maonyesho ya Mpango wa ujenzi wa Nyumba za Gharama Nafuu
kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Mei 30, 2017. Maonyesho hayo
yameandaliwa na Muungano wa Vikundi Vya Vicoba Tanzania (VIGUTA)
.Kushoto ni Mwenyekiti wa Taifa wa VIGUTA, Dkt. Salmin Ibrahim
Dauda.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amezitaka Halmashauri za wilaya nchini ziangalie uwezekano wa kuwapatia
watumishi wake nyumba za bei nafuu kwa malipo kidogo kidogo.
Amesema Halmashauri za
wilaya kupitia mapato ya ndani, japo si makubwa zinaweza kuandaa mazingira
yatakayowawezesha watumishi wake kupata nyumba kupitia mpango wa ujenzi wa
nyumba za gharama nafuu unaofanywa na Muungano wa Vikundi vya Vicoba Tanzania
(VIGUTA).
Ametoa wito huo leo (Jumatano,
Mei 31, 2017) mara baada ya kutembelea maonyesho ya Mpango wa Ujenzi wa Nyumba
za Waheshimiwa Wabunge (Low Cost Housing) yanayoendelea kwenye viwanja vya
Bunge mjini Dodoma.
Waziri Mkuu aliwashauri
viongozi wa VIGUTA wafanye mawasiliano na Halmashauri zote na akawataka
watenge muda wa kuzitembelea Halmashauri hizo ili kuonyesha nia na uwezo
wao wa kujenga nyumba za gharama nafuu ambazo malipo yake hulipwa kidogo kidogo
kwa lengo la kuboresha maisha ya Watanzania.
“Watanzania wengi hivi sasa
wanapendelea nyumba ndogo, nzuri na ambazo zimekamilika. “Wengi wao, na
hasa wafanyakazi, siku hizi wana shughuli nyingi na hawana muda wa kujenga
nyumba na kuzisimamia wenyewe kama zamani. Hivyo, wanahitaji makampuni
yanayoweza kuwanjengea nyumba na wao wakalipa kidogo kidogo,” amesisitiza.
Aliwaaasa viongozi wa
VIGUTA wahakikishe kuwa wanajenga nyumba zenye ubora unaokubalika ili waweze
kuaminika hali ambayo itawawezesha kupata wateja wengi zaidi.
“Katika kipindi hiki
ambacho Serikali inahamia Dodoma, Muungano wa Vikundi vya VICOBA au VIGUTA unayo
nafasi kubwa ya kuwapatia watumishi wanaohamia nyumba za kuishi kupitia mpango
wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu,” Waziri Mkuu alisema.
Alisema watumishi wengi
wanaoingia gharama kubwa kwa kuishi katika nyumba za kupanga huku wakilipa kodi,
sasa wamepata kimbilio kwani wanaweza kujengewa nyumba kwa muda mfupi na kwa
bei nafuu na wakalipa kidogokidogo kwa kipindi cha hadi miaka 15.
Naye, Mwenyekiti wa VIGUTA
Taifa, Dkt. Salmin Ibrahim Dauda alimweleza Waziri Mkuu kwamba wana uwezo
wa kujenga nyumba kwa gharama ya shilingi milioni 12, milioni 15, milioni 25 na
milioni 60 kutegemeana na ukubwa wa nyumba.
Alisema wameweka viwango
tofauti ili kuwawezesha Watanzania wenye kipato cha chini kumiliki nyumba zao
wenyewe.