Rais
wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni amewasili hapa nchini leo kwa
ziara rasmi ya kiserikali ya siku 2 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.
Katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam Mhe. Rais
Museveni amepokelewa na mwenyeji wake Mhe. Dkt. Magufuli pamoja na viongozi
wengine wa Tanzania Bara na Zanzibar wakiwemo Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu
Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Akiwa
Uwanjani hapo Mhe. Rais Museveni amepokea heshima ya kupigiwa mizinga 21
iliyokwenda sambamba na nyimbo za mataifa yote mawili na wimbo Jumuiya ya
Afrika Mashariki na kisha akakagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa ajili yake
na baadaye akashuhudia burudani ya vikundi vya ngoma na matarumbeta.
Baada
ya mapokezi hayo rasmi, Mhe. Rais Magufuli amefanya mazungumzo na mgeni wake
Mhe. Rais Museveni Ikulu Jijini Dar es Salaam na baadaye viongozi wote wawili
wamezungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari.
Katika
hotuba yake Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Museveni kwa kukubali
mwaliko wake wa kuitembelea Tanzania na kueleza kuwa Serikali yake ya Awamu ya
Tano itaendeleza ushirikiano na uhusiano wa kidugu uliopo kati ya Tanzania na
Uganda huku akitilia msisitizo wa uhusiano huo kujikita katika kuongeza
biashara na kuharakisha miradi ya maendeleo inayoziunganisha nchi hizi mbili.
Mhe.
Rais Magufuli amesema japo kuwa biashara kati ya Tanzania na Uganda imekua
kutoka Shilingi Bilioni 178.19 mwaka 2015 hadi kufikia Shilingi Bilioni 193.59
mwaka 2016 bado nchi hizi zinapaswa kuongeza zaidi na ametoa wito kwa
wafanyabiashara wa nchi zote mbili kushirikiana zaidi katika biashara na
uwekezaji.
“Uwekezaji
wa wafanyabiashara wa Uganda hapa nchini Tanzania una thamani ya Dola za
Marekani Milioni 46.05 na umezalisha ajira 1,447”
“Watanzania
wanaoishi Uganda ni wengi kuliko wanaoishi katika nchi nyingine yoyote duniani,
hii ina maana tunapaswa kushirikiana zaidi na kufanya biashara zaidi”
amesema Rais Magufuli.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli amesema ili kukuza biashara na Uganda, Tanzania imeanza
kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo kujenga reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) ambayo itakwenda pamoja
na ujenzi wa bandari kavu Mkoani Mwanza ili wafanyabiashara wa Uganda
wasilazimike kuja mpaka bandari ya Dar es Salaam kuchukua mizigo yao inayotoka
nje ya nchi kwa meli, kukarabati meli ya MV Umoja itakayovusha mizigo mpaka
bandari ya Port Bell kupitia ziwa Viktoria, kununua ndege 6 za kusafirisha kwa
ajili ya Shirika la ndege la Taifa (ATCL) na kupunguza vizuizi vya barabarani
hadi kufikia 3.
Kuhusu
mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga
nchini Tanzania, Mhe. Rais Magufuli amesema Tanzania ipo tayari ujenzi huo
uanze baada ya kukamilisha mazungumzo ya masuala machache yaliyokuwa yamebaki
na ametaka wawekezaji waanze kazi ya ujenzi badala ya kuleta visingizio.
Kwa
upande wake Mhe. Rais Museveni amemshukuru Rais Magufuli kwa mapokezi mazuri
aliyoyapata na amesema Uganda itaendelea kuwa ndugu na rafiki wa kweli wa
Tanzania huku akisisitiza kuwa rafiki na ndugu wa kweli ni lazima wawe wamoja
katika maamuzi na mipango mbalimbali ikiwemo maendeleo na biashara.
Mhe.
Rais Museveni amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kufuata nyayo za Hayati Baba
wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kutokana na juhudi zake za kujenga
reli ya kati, kununua ndege, kufufua biashara kati ya Tanzania na Uganda na
msimamo wake kuukataa mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Ulaya ambao umeoneka kutokuwa na
manufaa ya kiuchumi kwa Afrika Mashariki ikiwemo kutishia mpango wa ujenzi wa
viwanda.
“Nimefurahi
kuwa Mhe. Magufuli unafuata nyayo za Mwalimu Nyerere, mimi pia ni mfuasi wa
Mwalimu Nyerere, hata nilipokuja Tanzania kusoma nilikuwa namfuata Mwalimu
Nyerere” amesema Mhe. Rais Museveni.
Mhe.
Rais Museveni ametoa wito kwa nchi za Afrika Mashariki na Afrika nzima
kuzungumza lugha moja na ziwe na msimamo wa pamoja ili
kukabiliana na ukoloni ambao huko nyuma ulitawala kutokana na watawala wa
Afrika kukosa umoja.
Kuhusu
bomba la Mafuta, Rais Museveni amesema atafuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa
mradi huo hasa baada ya uamuzi kufanyika kuwa bomba la mafuta yaliyogundulika
Hoima nchini Uganda litapitia Tanzania hadi bandari ya Tanga.
Jioni
hii Mhe. Rais Museveni atahudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima
yake na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment