Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.

Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.





Nafasi Ya Matangazo

Wednesday 18 January 2017

WAZIRI MKUU AMALIZA MGOGORO WA MIPAKA KATI YA KILINDI NA KITETO

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameumaliza mgogoro wa mpaka wa ardhi baina ya vijiji vya wilaya za Kiteto na Kilindi uliodumu kwa muda mrefu.

Mgogoro huo ambao ulianza kusuluhishwa tangu mwaka 1997, umepata suluhu kwenye mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Waziri Mkuu na kuwajumuisha Wakuu wa Mikoa hiyo miwili, Wabunge wa Kiteto na Kilindi, wenyeviti wa Halmashauri na madiwani wa kata mbili za mpakani pamoja na wananchi wa kata hizo.

Waziri Mkuu pia amewataka wanasiasa na viongozi wengine kutowavuruga wananchi na badala yake wawaongoze vizuri na kutoa maelekezo kwa mujibu wa sheria za nchi.

Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Januari 18, 2017)  wakati akizungumza na wananchi wa wilaya za Kiteto na Kilindi katika kijiji cha Lembapili wilayani Kiteto, mkoani Manyara ambako ni kuna mpaka wa  wilaya hizo mbili alipokwenda kutatua mgogoro huo.

Amesema viongozi wa wilaya hizo lazima wafuate sheria na wawaelekeze wananchi umuhimu wa kuzingatia sheria za nchi ikiwa ni pamoja na kuheshimu mipaka iliyowekwa kwa mujibu wa sheria ili kuepusha migogoro.

Akizungumzia kuhusu mgogoro huo wa mpaka, Waziri Mkuu amesema nchi ilishaweka mipaka ya mikoa na wilaya zake yote tangu zamani na kumbukumbu zipo zikiwemo za mpaka wa  wilaya hizo tangu mwaka 1961 kwa  tangazo la Serikali namba 65 na hakuna mabadiliko. Hivyo, aliwasisitiza wauheshimu na kuufuata.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itakwenda kuweka alama vizuri na viongozi wa wilaya hizo watashirikishwa. Alama hizo zitawekwa na kifaa maalumu, hivyo amewataka wahusika watoe ushirikiano.

Waziri Mkuu amesema katika kipindi ambacho Serikali itakuwa ikiweka alama hizo, wananchi waendelee na shughuli zao hadi hapo zoezi litakapokamilika na wala wasibughudhiwe.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa siku nane kwa watu wote wanaomiliki silaha katika wilaya za Kilindi na Kiteto wazipeleke kwenye vituo vya Polisi ili zisajiliwe upya na kisha Wakuu wa Mikoa wafanye operesheni maalum na atakayekutwa anamiliki silaha kinyume cha sheria achukuliwe hatua.

“Wakuu wa Mikoa fanyeni ukaguzi maalum na atakayekutwa anamiliki silaha kinyume na utaratibu achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria. Pia kuna watu wana mitambo ya kutengenezea bunduki hapa, nao pia waisalimishe haraka,” amesisitiza. 

Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. William Lukuvi amesema mwanzoni mwa Februari wataalamu wake watakwenda katika mpaka huo ili kuanza kuweka alama vizuri.

Amesema baadhi ya viongozi huwa wana tabia ya kuzuia watendaji kutekeleza majukumu yao, hivyo ametumia gursa hiyo kuwaomba viongozi wa wilaya hizo watoe ushirikiano.

Amesema moja ya majukumu aliyopewa na Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli ni kuhakikisha ndani ya miaka hii mitano anamaliza migogoro ya ardhi nchini ukiwemo huo wa Kilindi na Kiteto.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Post a Comment