Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB anayemaliza muda wake, Edmund Mkwawa akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam jana.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB anayemaliza muda wake, Edmund Mkwawa (kulia) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji
mpya wa Benki hiyo ambaye anataraji kuanza kazi rasmi Januari mosi 2018,
Godfyey Ndalahwa. Mkwawa ameiongoza benki hiyo kwa miaka 15 Tangu kuanzishwa
kwake, huku akijivunia mafanikio katika utendaji wake kwa kukuza Amana za wateja kutoka shilingi Bilioni
1.76 mwaka 2002 hadi shilingi bilioni 107 Mwezi Septemba 2017. (Picha na Mroki
Mroki).
MAENDELEO YA BENKI YA BIASHARA YA DCB (DCB COMMERCIAL BANK PLC) TANGU
ILIPOANZISHWA MWAKA 2002
Ndugu Wanahabari
Napenda kumshukuru Mwenyezi
Mungu kwa kutukutanisha hapa leo. Lengo la kuwaiteni ni kutoa taarifa kwa umma
juu ya maendelo ya Benki ya Biashara ya DCB tangu kuanzishwa kwake ikiwemo
mafanikio na malengo yake kwa kipindi kijacho kuanzia mwaka 2018.
Baadhi ya ajenda nitakazozipitia ni kutoa historia fupi ya benki na madhumuni
ya uanzishwaji wake, taarifa ya utendaji kwa kipindi cha miaka 15, mahusiano na
wanahisa wakuu ikiwemo manispaa ikiwemo mafanikio na changamoto
iliyopata/ilizopata benki katika mahusiano hayo, msaada na uhusiano wa baadaye
unaohitajika kutoka kwa wanahisa wakuu ikiwemo manispaa na mipango ya baadaye
ya Benki yetu.
Awali ya yote, napenda kuwataarifu kuwa Benki ya Biashara
ya DCB imekuwa mshindi wa kwanza katika mashindano ya uandaaji na uwasilishaji
wa taarifa za mahesabu ya benki kwa mwaka 2016 kwa sekta za benki ndogo na za
kati kwa ubora. Nafasi hii imeshikiliwa na benki yetu kwa mwaka wa pili
mfululizo tangu mwaka 2015. Tuzo hii huandaliwa kila mwaka na Bodi ya Taifa ya
Wahasibu na Wakaguzi wa Mahesabu (NBAA).
Mashindano haya yalianza tangu
mwaka 2011, na katika kipindi chote hicho DCB Commercial bank imeweza kufanya
vizuri ambapo kwa miaka mitatu mfululizo (mwaka 2012 hadi 2014), Benki imeshika
nafasi ya tatu (3) miongoni mwa benki zote kiujumla kwa ubora wa uandaaji na
uwasilishaji wa taarifa za mahesabu ya kibenki. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.
Hii ni kielelezo kwamba Benki ya
DCB inafuata miongozo ya utawala bora wa fedha ikiwemo uwasilishwaji wa taarifa
sahihi za amana na mikopo, kiwango cha faida kinachotumiwa katika maamuzi ya
uwekezaji na ukusanywaji wa kodi; na kwa kufuata miongozo iliyowekwa na Benki
kuu, Bodi ya uhasibu na viwango vya kimataifa vya uwasilishwaji wa taarifa za
fedha.
Gawio la Jumla; napenda kuwakumbusha kuwa Benki ya
Biashara ya DCB imetimiza miaka 15 ya utoaji huduma bora za kibenki kwa
Wajasiriamali, tangu ianzishwe mnamo mwaka 2002. Ifikapo mwaka 2018 benki yetu
itasheherekea miaka 16 ya utoaji huduma zake kwa wajasirimali na wanachi wenye
vipato vya chini na vya kati. Katika miaka 15 ya utendaji wake, Benki ya
Biashara ya DCB imekuwa ikipata faida mfululizo tangu mwaka 2004 na kutoa gawio kwa wanahisa wake kwa miaka 10 tangu
mwaka 2006 hadi 2015. Hadi kufikia mwaka 2015, jumla ya shilingi bilioni 12.4 zimetolewa
kama gawio kwa wanahisa wote (Dividends) ikilinganishwa na kiwango cha shilingi
milioni 681.3 zilizotolewa kama gawio kwa wanahisa kuanzia mwaka 2002 hadi
mwaka 2006.
Gawio kwa Manispaa; Kama sehemu ya gawio hilo la shilingi
bilioni 12.4, kiasi cha shilingi bilioni 4.4 ni gawio kwa wanahisa wake
waanzilishi ambao ni Jiji la Dar es Salaam likijumuisha manispaa zake za Ilala,
Kinondoni na Temeke ambao waliwekeza jumla ya shilingi Bilioni 1.3 tangu kuanzishwa
kwa benki hii hadi sasa ambazo zilitoka kama asilimia 10 ya mapato ya manispaa
kwa ajili ya mfuko wa wanawake na vijana. Tangu kuwekeza kiasi hicho cha
shilingi bilioni 1.3, benki imekuza mtaji wa manispaa hadi kufikia shilingi 6.3
bilion kwa njia ya hisa bakizi (bonus issue) na hisa stahiki (rights issue).
Chimbuko la Benki; Ndugu wanahabari, ikumbukwe kwamba benki
ya biashara ya DCB ilianzishwa kufuatia wito wa Rais wa awamu ya tatu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Benjamin William Mkapa. Malengo ya
uanzishwaji wake yakiwa ni kuwapatia mitaji wananchi wenye kipato cha chini na
cha kati ambayo itasaidia kuanzisha na kuendeleza biashara zao.
Hivyo basi, benki ya biashara
ya DCB inaendelea kutimiza wajibu wake kwa ufasaha na weledi kwa kuanzisha
huduma mbalimbali za kibenki zinazokidhi mahitaji ya kifedha na hivyo kutimiza
ndoto za wananchi.
Benki imekuwa ikiwakopesha Wanawake na Vijana na vikundi mbalimbali
kupitia mfuko wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Temeke na Ilala ambapo
hadi mwaka 2017 Shilingi bilioni 123.8 zimeshatolewa kwa wanufaika 476,146.
Kati ya hizo, shilingi bilioni 12.7 zinatokana na mfuko wa Manispaa za Dar es
Salaam. Benki inatarajia kuendelea kukuza mikopo kupitia mifuko hii na
inaendelea kushirikiana na kuhamasisha manispaa ziendelee kutunisha mfuko huu
kwa manufaa ya wananchi.
Mtandao wa Benki; Benki imepanua wigo wake wa biashara
kutoka benki inayotoa huduma zake Dar es salaam pekee, na kuwa benki ya
kibiashara inayotoa huduma zake nchi nzima kwa kuanzisha huduma zenye
kurahisisha upatikanaji wa huduma za DCB kupitia wakala (DCB Jirani) na huduma
kupitia simu ya mkononi (DCB Pesa).
Huduma ya DCB Jirani inaendelea
vizuri kwa sasa Benki ina jumla ya mawakala 542 wanaotoa huduma za DCB nchi
nzima. Huduma hizi zitasaidia kuwafikia wateja wengi Zaidi na kwa gharama nafuu
na itaweza kuwafikia jamii ya watanzania wa kipato cha chini na cha kati ambao
ni Zaidi ya asilimia 70. Benki hii pia imejikita katika kusogeza huduma kwa
wateja kupitia matawi, ambapo matawi yameongezeka kutoka matawi 2 mwaka 2005
hadi matawi 8 mwaka 2017. Mwezi April 2017 benki imefungua tawi la 8 makao
makuu ya nchi, Dodoma.
Thamani ya Hisa; Benki ya DCB ndio benki ya kwanza kuorodheshwa katika soko la hisa la
Dar es Salaam mnamo mwaka 2008. Pamoja na mabadiliko ya hali ya soko la hisa la
Dar es Salaam kwa kipindi cha utendaji wa benki, hadi kufikia robo ya tatu ya
mwaka huu (2017) thamani ya hisa kwenye soko imefikia shilingi 380 ikiwa imeongezeka
kutoka shilingi 275 (mwaka 2008). Benki iliongoza kwa kufanya vizuri katika
soko la hisa la Dar es Salaam mwaka 2011 kwa kuwa Benki ya Kwanza Afika Mashariki
na ya tano Afrika.
Mahusiano na
Wanahisa; Benki imeendelea kuwa na mahusiano mazuri
na wanahisa ukiacha changamoto chache zilizojitokeza kuhusiana na pesa za mgao
kutoka manispaa na nafasi ya manispaa katika kuwekeza amana zake katika benki.
Hata hivyo, Benki na manispaa zimefanya vikao mbalimbali vilivyolenga kuondoa
sintofahamu iliyokuwepo na pia kuwaelimisha wadau wapya wa manispaa mafanikio
na malengo ya muda mrefu ya Benki ambayo wengi hawakuwa wakiyafahamu. Tuna
Imani thabiti kuwa mahusiano yataboreka na kusaidia Benki kukua Zaidi
kiutendaji.
Utendaji; Tangu kuanzishwa kwake, benki ya biashara ya DCB
imepata mafanikio ya katika utendaji wake kwa kukuza Amana za wateja kutoka shilingi Bilioni 1.76 mwaka 2002 hadi
shilingi bilioni 107 Mwezi Septemba 2017. Mikopo
ya benki pia imeongezeka kutoka shilingi Bilioni 1.02 mwaka 2002 hadi kufikia
shilingi Bilioni 89.2, mnamo Mwezi Septemba 2017.
Msaada kwa Jamii; Jumla ya shilingi milioni 180.3 zimetumika
kusaidia shughuli mbalimbali kwa manufaa ya Jamii kama vile msaada wa Vitanda, vyandarua, mashine za kupumulia
watoto, vitanda kwa ajili ya akina mama kujifungua katika Hospitali za manispaa
za Dar es salaa, madawati, vifaa vya maabara mashuleni.
Ili kusaidia ukuaji wa uchumi
wa viwanda, Benki imelipa kodi, tozo
na makato mbalimbali serikalini
ambazo zinafikia shilingi Bilioni 23.4 kwa kipindi cha mwaka 2002 hadi 2016.
Changamoto; Mnamo mwaka 2016, benki haikufanikiwa kutoa gawio
kwa wanahisa wake ikiwa ni mrejeo wa changamoto mbalimbali ambazo benki
ilikutana nazo katika utendaji wake. Chache kati ya hizo ni benki kupoteza
wateja wakubwa wa serikali ambao walifunga akaunti na kuzihamishia benki kuu,
idadi kubwa ya mikopo chechefu iliyotokana na watumishi hewa wa serikali ambao
sehemu kubwa walikuwa na mikopo katika benki yetu na pia kuongezeka kwa gharama
zisizotokana na riba zinazohusiana na ushuru katika huduma za kila siku. Sababu
zote hizi zilisababisha matokeo yasiyoridhisha na kupelekea benki kupata hasara
katika mwaka 2016.
Mipango ya baadaye; Benki itaendelea kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazojitokeza
hasa katika mikopo ya wajasiriamali wadogo na wa kati ili kuwainua kiuchumi
kupitia mitaji yenye masharti nafuu na wezeshaji Kwa kuongezea, benki
itaendelea kushirikiana na mifuko mbalimbali maalumu ikiwemo manispaa zote tano
za Jiji katika kusaidia maendeleo ya vikundi vya wajasiriamali wadogo ikiwemo
wanawake na vijana.
Kwa kufanya hayo, benki itakuwa imesaidia ukuaji wa uchumi wa wanyonge
na wasiojiweza ilhali ikitekeleza hatua muhimu ambazo ni muafaka kwa mazingira
yaliyopo. Malengo na maslahi ya wanahisa na wadau wote yatalindwa huku benki
ikiendelea kukuza amana kwa kuwa na amana za kudumu na ambazo ni za gharama
nafuu. Wakati huohuo benki itajikita katika kuhakikisha inakusanya mikopo
chechefu huku ikikuza mikopo yenye ubora ambayo itailetea benki mapato.
Ndugu Wanahabari;
MATARAJIO YA MWAKA 2018
Benki imejipanga kuendeleza
malengo yake na kuhakikisha inakuwa chaguo la kwanza la wateja katika utoaji
huduma za kifedha. Katika kutimiza malengo haya, benki itatumia teknolojia ya
kisasa katika utoaji wa huduma zake kupitia huduma ya DCB Pesa (kupitia simu ya
mkononi) na DCB Jirani (Huduma kupitia wakala) kwa lengo la kuwafikia wateja
wengi walengwa ambao ni wajasiriamali wadogo na wa kati waliosambaa kote nchini
hadi vijijini.
Mojawapo ya malengo ya benki kwa
mwaka unaokuja wa 2018 ni kuhakikisha inaongeza wigo na viwango vya utoaji huduma
na kuwafikia wateja wengi zaidi wanaohitaji huduma za kibenki ikiwemo wamiliki
wa Vikoba na Wafanyabiashara wa kati ambao wamehitimu hatua za mikopo ya awali
katika benki hii. Hii ni kuhakikisha benki inakua pamoja na wateja wake na
haitowaacha kuwahudumia katika mahitaji yao hata wakiongeza wigo wa biashara
zao.
Kwa kuongezea, Benki itaendelea
kukuza amana na mikopo kwa wateja ili kujiwekea mazingira mazuri ya kiutendaji
na kuiwezesha kuchangia maendelo ya nchi kupitia utoaji wa gawio kwa wanahisa,
ulipaji wa kodi za serikali na utoaji wa ajira kwa wananchi. Ili kufanikisha
hayo, benki itawekeza katika rasilimali watu kusaidia uboreshwaji wa huduma za
mikopo ya vikundi vya wanawake na vijana na mikopo ya vikoba.
Benki itaendelea kuwekeza
katika teknolojia ili kuhakikisha inatoa huduma za kisasa kupitia mawakala na
simu za mikononi ili kuwafikia walengwa wa mikoani na vijijini. Kwa
kuhitimisha, benki itajitahidi kudhibiti mikopo chechefu na kukusanya madeni ya
wateja yaliyopitiliza muda ili kusaidia kuimarisha mtaji na kutoa huduma kwa
wateja wengine.
Hitimisho
Uongozi wa benki unapenda kuwataarifu
kuwa Mkurugenzi wa awali aliyeianzisha na kuifikisha hapa benki ya biashara ya
DCB Bw. Edmund Mkwawa anatarajia kustaafu kuanzia tarehe 31 Desemba 2017.
Kuanzia hapo, benki itakuwa chini ya usimamizi wa mkurugenzi anayeshika hatamu
Bw. Godfrey Ndalahwa.
Benki ya Biashara ya DCB
inapenda kuwatakia wateja wake, wadau, wanahisa na wananchi kwa ujumla sikukuu
njema ya Christmas na heri ya mwaka mpya 2018.
EDMUND
P. MKWAWA
MKURUGENZI
MTENDAJI
DCB
COMMERCIAL BANK PLC
DESEMBA
2017.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment